Zaidi ya Sh10 bilioni kuwakomboa vijana kiuchumi Tanzania
- Fedha hizo zitatumika kuwawezesha vijana waliohitimu programu mbalimbali ikiwemo BBT kujiajiri.
- Naibu Waziri Katambi aagiza usimamiizi mzuri wa fedha hizo ili ziwanufaishe walengwa.
Mwanza. Serikali ya Tanzania imetenga zaidi ya Sh10 bilioni kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha ili kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na changamoto za ajira kwa vijana.
Hayo yamebainishwa jijini Mwanza na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Ajira kazi na wenye ulemavu, Patrobas Katambi wakati wa kuhitimisha mafunzo ya uvuvi na ukuzaji viumbe majini kwa vijana 300 ambapo pamoja na mambo mengine amewataja baadhi ya wanufaika kuwa ni pamoja na wanaohitimu mafunzo kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kupitia program ya jenga kesho iliyobora BBT.
“Fedha hizi ni kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi pekee, bado kuna fedha zingine kutokana Ofisi ya Waziri Mkuu, kwenye halmashauri zile za asilimia mbili kwa vijana, kwa hiyo fedha zote hizi zinaenda kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi kupitia program walizojifunza,” amesema Katambi
Kwa mujibu wa Katambi lengo la.mafunzo hayo ni kupunguza Wimbi la vijana wasio na ajira hivyo kigezo cha ngazi ya elimu sio cha muhimu sana.
Itakumbukwa kuwa Serikali ilianzisha mradi wa BBT lengo likiwa kuongeza ujumuishi wa vijana katika shughuli za kilimo na baadae kwenye shughuli za ufugaji ambapo afua mbalimbali zimeendelea kutekelezwa na Serikali.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega aliwaambia wabunge Mei 13, 2024 wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2024/2025 kuwa jumla ya vituo 15 vya mradi huo vimejengwa na wanufaika wamefikia 300.7
Soma zaidi:Dk Biteko awataka Makatibu Mahsusi kujiendeleza kitaaluma
Fedha ziwafikie vijana
Katika kuhakikisha lengo la Serikali linatekelezwa Katambi amemwagiza, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ridhiki Shemdoe kuhakikisha fedha hizo zilizotengwa zinawafikia vijana hasa waliopata mafunzo.
“Nikuagize sasa katibu mkuu kuhakikisha fedha zote hizi zinawafikia vijana hasa waliopata mafunzo kwenye sekta mbalimbali, mfano hawa wa uvuvi wataenda na kuliingizia Taifa fedha za kigeni kwa kuwa hivi sasa fedha hizo zimepungua nchini, lakini pia wataenda kusaidia katika suala la lishe na virutubisho mbalimbali,” amesema Katambi
Awali, Katibu Mkuu wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ridhiki Shemdoe amesema tayari wizara hiyo imetenga fedha kwa ajili ya kununulia vizimba, na boti kwa ajili ya vijana hao na kuwataka kujiunga kwenye makundi ili kuweza kunufaika na mikopo hiyo.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo hayo pamoja na kupongeza Serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo pia wamesema wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitendea kazi ambavyo vingerahisisha utendaji kazi katika vituo atamizi vilivyotengwa.
Latest