Zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi hawajaripoti kidato cha kwanza Magu

January 24, 2024 4:49 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • 3,337 pekee kati ya 8,827 ndio waliowasili.
  • Hali ni mbaya zaidi katika Wilaya ya Sengerema.

Mwanza. Ikiwa ni wiki ya tatu toka kufunguliwa kwa muhula wa kwanza wa masomo, mwaka 2024 nchini Tanzania, zaidi ya wanafunzi 5,090 wa kidato cha kwanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu hawajaripoti shule.

Jumla ya wanafunzi 8,827 walifaulu na kupangiwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza wilayani humo, ambapo mpaka jana, Januari 22, 2024  ni wanafunzi 3,337 pekee sawa na asilimia 37 ndio wameripoti kuanza masomo.

Mkuu wa wilaya ya Magu, Rachel Kasanda aliyekuwa akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani la kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 amesema wanakusudia kufanya oparesheni ya kuwasaka wazazi ambao hawajawapeleka watoto wao shule ili wachukuliwe hatua stahiki.


Soma zaidi: Maumivu vifaa vya shule vyapanda bei Mwanza


“Tutaanzisha msako wa nyumba kwa nyumba kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanaenda shule, hatutaangalia familia ina changamoto gani tunachoangalia kwa sasa ni kwamba elimu ni bure na mwanafunzi anatakiwa aripoti shule hata kama hana sare,” amesema Kasanda.

Hata hivyo, wakati idadi ya wanafunzi wanaoripoti kidato cha kwanza ikichechemea wilayani Magu hali ni ya ahueni kiasi katika wilaya nyingine za jiji la Mwanza ikiwemo Ilemela ambapo mpaka sasa wanafunzi 7,738 kati ya wanafunzi 10,971 sawa na asilimia 70.5  ya waliofaulu wameshaanza masomo.

Hali ni ya kusikitisha zaidi katika Halmashauri ya Wilaya Sengerema, ambapo hali ya wanafunzi kuripoti inasua sua kwa kiwango kikubwa, ambapo kwa mujibu wa Binuru Shekidele, ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri hiyo, mpaka Januari 21, 2024 ni asilimia nane tu ya wanafunzi waliofaulu walikuwa wameripoti.

Mkuu wa wilaya ya Magu Rachel Kasanda akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani wilayani Magu. Picha na Mariam John/ Nukta

Aidha, kwa upande wao baadhi ya wazazi mkoani Mwanza wametaja sababu zinazochangia wanafunzi kutoripoti shule ikiwa ni pamoja na ugumu wa maisha pamoja na mahitaji mengi ya vifaa vinavyotakiwa shuleni.

Rachel Cosmas Mkazi wa Magu, ameiambia Nukta Habari kuwa mahitaji ya wanafunzi wanayotakiwa kwenda nayo shule ni mengi kuliko uwezo wa wazazi sababu inayochangia kwa wale wasiokuwa na uwezo kushindwa kumpeleka mtoto kwa wakati.

“Hakuna mzazi ambaye hapendi mtoto wake asome ila changamoto ni uchumi tu na kutokamilisha mahitaji yake kwa wakati, hivyo ni vizuri iwapo Serikali ikalitazama hili itasaidia kuwapa nafasi wazazi wajikusanye ili kupata fedha ya kuwapeleka shule,” amesema Cosmas.


Soma zaidi:  How pottery boost women incomes in Iringa region


Hussein Hassan, Mkazi wa Nyamagana, ameiambia Nukta Habari kuwa hali ya uchumi hususani kipindi hiki cha mwezi wa kwanza ni miongoni mwa sababu iliyochochea wanafunzi kutoripoti shule kwa wakati.

Hata hivyo, wakati wazazi wakitoa sababu ya ukosefu wa fedha ya ununuzi wa mahitaji mbalimbali, kama miongoni mwa sababu iliyowakwamisha kupeleka watoto shule kwa wakati, uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa nyakati tofauti umewataka walimu kuwapokea wanafunzi hata kama hawana sare na vifaa hitajika kwa wakati huo ili kuwapa wazazi muda wa kutafuta vifaa hivyo.

Mapema mwezi Januari 2024, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala, aliwataka walimu wilayani humo, kuwapokea wanafunzi hata kama watakuwa hawana mahitaji yaliyoainishwa ikiwemo sare na michango ili kuwapa nafasi wazazi wao kukamilisha mahitaji hayo.

Masala aliyekuwa akizungumza na wadau wa elimu wilaya humo alibainisha kuwa anataarifa za baadhi ya wakuu wa shule kuandika mambo yasiyo ya muhimu kwenye fomu za kujiunga na shule hali inayosababisha wanafunzi kushindwa kujiunga na masomo kwa wakati.

“Tunaposema elimu bure sio kumrundukia mzazi mahitaji mengi ambayo yanasababisha ashindwe kumpeleka mtoto shule na kwa sababu hiyo watoto wengi wanachelewa kuripoti shule hivyo kuwe na utaratibu maalum wa kuwapokea watoto wanapoenda kuanza shule,” alisema Masala.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW