Zahanati itakayookoa maisha ya maelfu ya wanawake, watoto Geita

December 13, 2021 3:34 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Wakazi wa Isebya wilayani Mbogwe wasubiria Serikali imalizie walipoishia.
  • Itakuwa ni zahanati ya kwanza katika kata ya Isebya tangu nchi ipate uhuru.

Geita. Agness Enock, mkazi wa kijiji cha Isebya mkoani Geita bado anaishi na huzuni moyoni mwake baada ya kupoteza watoto wawili ndani ya kipindi kifupi. 

Watoto hao wa Agness walifariki wakati wa kujifungua kutokana na kuchelewa kupata huduma baada ya kupata uchungu akiwa nyumbani na kuchelewa kufika zahanati ya Ilolangulu iliyopo kata ya Ilolungulu.

Kijiji anachoishi mama huyo kilichopo kata ya Isebya wilayani Mbogwe hakina zahanati hivyo kuwakosesha wanawake wengi huduma za haraka za afya ya mama na mtoto.

“Kwa miaka miwili nimepoteza watoto wawili,” anasema mama huyo huku uso wake ukianza kubadilika na kutandwa na huzuni.  

Agness (32) alipoteza mtoto wa kwanza mwaka 2019 na wa pili mwaka jana katika zahanati ya Ilolangulu wakati wauguzi wakijitahidi kumsaidia kujifungua. 

Sababu kubwa iliyofanya mama huyo anayejishughulisha na kushona ngua kupoteza watoto wake ni kuchelewa kufika katika zahanati hiyo iliyopo umbali wa kilomita nane kutoka kijini kwake.

“Zahanati ingekuwepo kijijini ningeweza kuokoa watoto wangu kwa sababu hapa ni karibu na ningeweza kufuatilia hali ya watoto tumboni na afya yangu,” anasema Agness. 

Ili kufika katika zahanati hiyo inayohudumia wakazi wa vijiji 12 vya tarafa ya Ilolangulu, Agness na wajawazito wengine hupakizwa kwenye pikipiki au kutembea kwa miguu kupita kwenye barabara ya vumbi na mashimo, jambo si rafiki kiafya kwao. 

Agness na wakazi wa Isebya hulazimika kwenda zahanati iliyopo kata ya Ilolungulu ili kupata matibabu lakini kufika katika zahanati hiyo ni changamoto kutokana na ubovu wa miundombinu ya usafirishaji. Picha| Gift Mijoe.

“Sitakuja kusahau matukio hayo mawili katika maisha yangu,” anasema mama huyo ambaye pia alinusurika kifo baada ya kukimbizwa na kupata matibabu katika kituo cha afya cha Ushirombo kilichopo Wilaya ya Bukombe mkoani Geita. 

Agness ni miongoni mwa wanawake wengi wanaopata changamoto za kiafya ikiwemo kupoteza maisha yao na watoto kutokana na kukosa huduma za afya za uhakika katika maeneo yao nchini Tanzania. 

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wastani wa vifo 562 vya uzazi katika kila vizazi hai 100,000 hutokea kila mwaka katika nchi zinazoendelea duniani ikiwemo Tanzania. 

Mwanga wa matumaini waanza kuonekana

Huenda hofu ya kupoteza mtoto mwingine ikaondoka kwa Agness baada ya wananchi wa kijiji cha Isebya kukamilisha ujenzi wa boma la zahanati ambalo limeshaezekwa paa katika kijiji chao. 

Kukamilika kwa zahanati hiyo ambayo mpaka sasa ujenzi wake umefikia Sh23 milioni utakuwa mkombozi kwa wakazi wapatao 20,000 wa Isebya ambao hawajawahi kuwa na huduma ya afya kwenye eneo lao.

Mkazi wa kijiji cha Isebya, Charles Tabu amesema zahanati hiyo imejengwa kwa nguvu za wananchi mpaka hatua iliyofikia ya paa na kutoa matumaini makubwa ya kupata huduma za uhakika za afya kwenye kijiji chao.

“Kutokupatikana kwa huduma ya zahanati mahali hapa imetuathiri sana, kwa mfano, mtoto anapoumwa inabidi usafiri umbali mrefu kwenda kufuata huduma.

“Hii inaathiri shughuli za mashambani. Mtu unapompeleka akiwa mgonjwa maana yake lile jua linampiga kama ni mtoto anaathirika sana,” amesema Tabu ambaye ni baba wa watoto wanne. 

                   

Sera ya Afya ya Taifa ya mwaka 2007 inaielekeza Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na wananchi kuhakikisha inajenga na kuboresha miundombinu rafiki ya afya ili kuwawezesha wanawake wajawazito na watoto wachanga kufikiwa kirahisi na huduma hizo. 

Mkazi mwingine wa kijiji cha Isebya, Suzana Katuga anasema kukamilika kwa zahanati hiyo kutasaidia kupunguza vifo vya wanawake na watoto ambao wamekuwa waathirika wakubwa wa kutopatikana kwa huduma za afya.

“Tutakua tumenusuru mauti kwa wazazi na watoto,” anasema Suzana ambaye ameishi kwenye kijiji hicho tangu mwaka 1986 bila kuwa na zahanati wala shule ya sekondari. 

Tabu na Suzana wanasema wanaamini Serikali itawasaidia kumalizia sehemu iliyobaki ili zahanati hiyo ifunguliwe na kuanza kufanya kazi.

Ujenzi zahanati hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2017 kwa nguvu za wananchi kwa kiasi kikubwa imechangiwa na elimu ya ushawishi kutoka Mtandao wa Waraghibishi katika Wilaya ya Mbogwe (MBODANET) kwa kushirikiana na Shirika la Tamasha na Twaweza.

Taasisi hizo chini ya mradi wa uraghabishi wilayani humo waliwajengea wananchi uwezo wa kujisimamia na kutekeleza miradi ya kijamii inayogusa maendeleo yao bila kusubiri Serikali. 

Diwani wa kata ya Isebya, Delton Mackyao anasema ni wakati sasa Serikali kukamilisha zahanati hiyo kwa sababu ujenzi wake umedumu miaka minne na imebakia sehemu ndogo ya kuweka sakafu, milango na madirisha na miundombinu ya maji na umeme.

 “Niwaombe Serikali wajaribu kutuangalia katika eneo hili kwa sababu wananchi kuna kazi ambayo waliifanya katika Sh23 milioni iliyotolewa si haba. Basi Serikali ikamilishe na kutuletea wataalam zahanati ianze kufanya kazi,” anasema Mackyao.  

Boma la zahanati ya kijiji cha Isebya lililojengwa kwa nguvu za wananchi wakati wakisubiri Serikali kukamilisha sehemu iliyobaki ili ianze kutoa huduma. Picha| Gift Mijoe.

Serikali yakubali kukamilisha zahanati 

Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe imesema inatambua kazi kubwa iliyofanywa na wananchi kuchanga fedha na vifaa kujenga maboma ya zahanati katika maeneo yao na wanafanya jitihada kuyakamilisha ili kupunguza changamoto za afya katika eneo hilo.  

“Kila mwaka Serikali tunajitahidi kupunguza au kukamilisha hayo maboma ili yaweze kutoa huduma,” anasema Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Pastory Mukaruka. 

Hata hivyo, Mukaruka amesema mkakati uliopo sasa hivi ni kuwawezesha na kuwashirikisha wananchi kujenga zahanati mpaka hatua ya mwisho bila kuishia kwenye hatua ya maboma, jambo litakaloongeza kasi ya zahanati kukamilika haraka. 

Enable Notifications OK No thanks