Katuni: Mwalimu wa watoto anayepaswa kuchunguzwa

February 14, 2022 9:52 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Watoto wanaotazama katuni kwa saa tatu hadi nne wanaweza kuathirika kiakili
  • Wasipodhibitiwa wanaweza kuiga tabia zisizofaa za wahusika wa katuni hizo.
  • Mbali na vurugu, watoto wanaweza kuongezeka uzito na kupata magonjwa ya macho.

Dar es Salaam. Ni muda mfupi tu tangu jogoo awike na kuamsha baadhi ya watu kwenye familia hii iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam. Kati ya waliojaliwa kuamka siku hiyo, ni Jaden, mtoto wa pekee mwenye miaka mitatu katika famili hiyo yenye watu wanne.

“Niwekee Disney” ni maneno ya Jaden akimwambia dada yake mlezi ambaye alikuwa akifanya usafi wa nyumba. Kwa kuwa hakusikia, amri ya mtoto huyo, Dativa aliendelea kudeki sakafu hadi aliposikia ombi la pili.

“Niwekee Disneeeey!” sauti ya Jaden ilitoka huku mtoto huyo akiwa katika msimamo wa “mguu sawa” kichwa chake kikielekea mbele kidogo kana kwamba alitaka Dativa asikie kwa usahihi ombi lake la kumwekea chaneli hiyo maarufu kwa kuonyesha katuni za watoto.

Taratibu, Dativa aliweka dekio lake chini na kuchukua rimoti ya king’amuzi na kuweka chaneli ya Disney. 

Jaden akiwa amesuuzika nafsi alikaa akiangalia katuni zake pale, kidole mdomoni huku rimoti akiwa ameishikilia na kutomruhusu mtu yeyote kubadili stesheni, hata mgeni aliyekuwa naye sebuleni hapo.

Zaidi ya saa tatu, Jaden alikuwa kitazama katuni kwenye televisheni bila kupumzika. 

“Jaden njoo unywe uji” alisikika Dativa akiita. Mgeni alisikia mwito huo lakini Jaden hakuitika. 

“Jaden… Jaden… Jaden” Dativa aliita tena lakini hakuna “naam” iliyosikika kutoka kinywani mwa Jaden.

“We Jaden, si unaitwa” alisema mgeni na taratibu, Jaden alinyanyuka na kuenda kule sauti ilikokuwa ikitokea. 

Licha ya kuondoka, mtoto huyo alibeba rimoti ya king’amuzi ili mgeni asibadilishe chaneli iliyokuwa ikionyesha shujaa akipambana na maadui waliokuwa wakimfukuza.

Kwa baadhi ya watoto, katuni zinaathiri tabia zao. Picha| Tribune India.

Jaden ni mmoja kati ya watoto wengi ambao huamka wakiwa na furaha ya kukaa mbele ya TV kutazama katuni zao pendwa, jambo linalowasaidia kujifunza mambo mengi.

Hata hivyo, tabia hiyo ya kutazama katuni muda mrefu ina madhara mbalimbalimbali kwa watoto hasa katika makuzi yao.  

Kwa nini ujali ?

Kwa watoto wa miaka ya zamani kabla televisheni au simu janja hazijawa maarufu, kuamka asubuhi kulifuatiwa na ruti za kukimbizana na watoto wa majirani mitaani.

Kwa sasa, mambo yamebadilika. Mtoto anaweza kutokuona mfanano wa jua tangu aamke kwani anakuwa mbele ya skrini akifurahia maudhui ambayo huenda mzazi wake hajaweka umakini wa kuyafuatilia.

Hiyo inamuondolea mtoto uwezo wa kuchangamka na mazoezi ya michezo na hata kutengeneza marafiki wa utotoni.

Licha ya katuni kuwa sehemu ya kuelimisha watoto, kwa baadhi ya wazazi ni sehemu ya kuondoa usumbufu wa watoto wao na kukwepa majukumu.

“Siyo kwamba katuni ni mbaya, hapana. Ni nzuri lakini mzazi naye anatakiwa kushiriki wajibu wake wa kumfundisha mtoto,” amesema Monica Meshack, mkazi wa Shinyanga.

Mathalan, katika kipindi mgeni yupo na familia hii, alishuhudia Jaden akitumia mafunzo aliyokuwa akijifunza kwenye katuni zake kwa dada yake. Alipopata mwiko na kuhisi ni visu vilivyotumiwa na mashujaa, alikuwa akimpiga dada yake, japo siyo kwa kumuumiza.

Kwa baadhi ya nyakati, mtoto huyo alikuwa akiiga maneno aliyokuwa akiyasikia kutoka kwenye katuni zile. “No” akimaanisha hapana, “stop” akimaanisha acha na mengine. 

Ni kweli Jaden alikuwa akiongea maneno ya kingereza ilhari alikuwa hajaanza hata shule.

Hata hivyo, mbali na mafunzo yake, upo upande wa Jaden ambao huenda wazazi wanatakiwa kuuzingatia.

Burudani yenye kiulizo

Kutazama televisheni ni jambo la kawaida kwenye jamii lakini bado kwa watoto linahitaji uangalizi wa karibu wa wazazi ili kuwaepusha na athari hasi vifaa hivyo vya kielektroniki. 

Mwandishi wa tovuti ya Azernews.Az, Aynur Aliyeva ameandika kuwa, watoto huanza kupenda maudhui ya televisheni wakiwa na miezi 18. 

Wanapofika miaka 2 tayari wanaweza kuwa watazamaji mashuhuli wa televisheni huku wakiwa na uwezo wa kuiga baadhi ya tabia zinazoonyeshwa na wahusika walio mbele ya macho yao.


Soma zaidi:


Hivyo ni muhimu kuelewa kuwa, wahusika wanaowatazama kila siku, wanaweza kuwa mifano hai na waalimu wa watoto hawa wasipoongozwa vyema na wazazi.

Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Neema Simbo ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa ni muhimu mzazi kutazama filamu ya katuni kabla hajaruhusu mtoto wake kuitazama.

Hiyo itampatia uhakika wa maudhui ambayo mtoto wake anachangamana nayo.

“Pale unapoona mhusika mbaya na anafanya sicho, kama mzazi, mwambie mtoto kuwa kufanya hili siyo sawa,” amesema Neema mwenye mtoto mmoja.

Usikose makala ijayo kuelewa sayansi iliyopo kati ya katuni na tabia za watoto.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks