Yaliyomo kwenye vitambulisho vipya vya wamachinga
- Vitakuwa na picha ya muhusika na baadhi ya kumbukumbu binafsi.
- Vimeboreshwa ili kuwawezesha kupata huduma mbalimbali zikiwemo za kifedha.
- Vitadumu kwa miaka miwili hadi mitatu.
Dar es Salaam. Serikali inatarajia kutoa vitambulisho vipya vya wamachinga vilivyofanyiwa maboresho vitakavyokuwa na picha ya muhusika na baadhi ya kumbukumbu binafsi zitakazomtambulisha na kumuwezesha kupata huduma katika maeneo mbalimbali zikiwemo taasisi za kifedha.
Vitambulisho hivyo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ni tofauti na vile vilivyoanza kutolewa mwishoni mwa mwaka 2018 kwa Sh20,000 kila kimoja ambavyo vilikuwa vinadumu kwa mwaka mmoja.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema vitambulisho hivyo vitaanza kutolewa Aprili Mosi mwaka huu baada ya kukamilika mchakato wa kuvitengeneza.
Amesema vitambulisho hivyo vitakuwa na picha ya mhusika, hivyo haitawezekana kutumiwa na mtu mwingine na pia vitadumu kwa miaka miwili hadi mitatu tofauti na vya sasa ambavyo vilikuwa vya mwaka mmoja.
“Serikali kupitia Mheshimiwa DkJohn Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kutoa vitambulisho rasmi ambayo vitawatambulisha popote na kupata huduma muhimu kama vile kutambulika na taasisi za fedha na maeneo muhimu,” amesema Majaliwa.
Majaliwa alikuwa akizungumza Januari 28, 2021 wakati alipofunga mkutano wa viongozi wa wamachinga kutoka mikoa yote Tanzania Bara, viongozi wa mabenki na baadhi ya mawaziri na watendaji wa Serikali katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Zinazohusiana:
- Flyover ya Tazara ilivyoleta maumivu, faida kwa wafanyabiashara ndogondogo
- Serikali kuwalipa wafanyabiashara marejesho ya VAT
- Rais Magufuli atoa vitambulisho maalum kwa wafanyabiashara wadogo
Aidha, Mtendaji huyo mkuu wa Serikali amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe wamachinga wanaendelea kufanya shughuli zao bila ya bugudha katika kipindi hiki ambacho muda wa matumizi ya vitambulisho vyao umekwisha.
Ili kurahisisha zoezi la utoaji wa vitambulisho vipya, amewaagiza viongozi wa wamachinga wahakikishe wanakuwa na takwimu sahihi za idadi ya wamachinga ili iwe rahisi kuwahudumia.
“Mkijiunga pamoja na kutambuliwa ni rahisi kwa taasisi za kifedha kuwafikia na kuwapatia huduma za mikopo itakayowawezesha kukuza mitaji yenu,” amesema Majaliwa.
Amesema Serikali imedhamiria kumuhudumia na kumtumikia kila mwananchi wakiwemo wamachinga kwa lengo la kuwawezesha kukuza biashara zao na kujikwamua kiuchumi, hivyo aliwataka wafanye kazi kwa bidii.
Latest