Yaliyojificha nyuma ya mikopo ya vikundi vya wajasiriamali

February 17, 2022 5:09 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya wanufaika wabadili matumizi yake.
  • Wengine walalamika ugumu wa kuipata na kutokukidhi mahitaji.
  • Serikali yasema inafuata sheria utoaji mikopo hiyo na si vinginevyo. 

Mwanza. Alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa na hamasa kubwa ya kujiajiri ili kujipatia kipato cha kuendesha familia.

Hata hivyo, changamoto ilikuwa mtaji wa kuanzisha biashara yake ya  kuchomelea vyuma pamoja na utengenezaji wa madirisha aina ya ‘aluminium’.

Joseph Mkulu (jina siyo halisi), mkazi wa Mtaa wa Mirongo jijini Mwanza, ni mmoja wa wanufaika wa mikopo inayotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa maarufu kama “Mikopo ya Halmashauri”. 

Mikopo hiyo inatolewa chini ya kifungu cha 37A cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, sura 290 na kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019.

Kupata mikopo hiyo, inahitajika wanawake na vijana waunde kikundi cha watu wasiopungua watano huku watu wenye ulemavu wakitakiwa kuwa wanakikundi wasiopungua wawili.

Kikundi hicho kinatakiwa kiwe kimesajiliwa, kina akaunti ya benki yenye jina la kikundi na kijishughulishe na ujasiriamali au kiwe na kusudi la kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati.

Mkulu aliyeanza biashara hiyo mwaka 2000, yeye na wenzake tisa walifanikiwa kuunda kikundi na kuwasilisha andiko la mradi kuhusu kupanua ofisi yao ya uchomeleaji na utengenezaji wa madirisha ya ‘aluminium’.

Walifanikiwa kupata mkopo wa Sh12 milioni kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza lakini hawakuitumia fedha hiyo katika andiko waliloombea fedha kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo utofauti wa malengo baina yao.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kupata mkopo huo kutokana na mlolongo mrefu ikiwemo mambo ya kisiasa na baadhi ya watu kutaka sehemu ya hizo fedha kwa sababu walifanikisha upatikanaji wake. 

“Kabla ya kuandika mradi huo kuna kiongozi alituambia tuunde kikundi tutapatiwa fedha, tulifanya hivyo na kweli fedha zilipatikana japo kwa makato makubwa,” anasema Mkulu. 

Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanslaus Mabula (mwenye shati la njano) akiwasikiliza wafanyabiashara wa nyanya katika soko la Buhongwa alipotembelea hivi karibuni. Picha| BMG.

Viunzi walivyovuka

Mkulu anadai mikopo hiyo haitolewi kirahisi kama watu wanavyofikiria. Baadhi ya viongozi waliwapa masharti ambayo siyo rasmi ikiwemo kujihusisha na masuala ya kisiasa ikiwemo kuwa na kadi ya chama fulani cha siasa.

“Niliingiwa na uoga kwa kuwa sikuwa na kadi ya chama, lakini kwa kushirikiana na uongozi wa chama hicho ilitulazimu kufoji kadi hizo na kufanikisha jambo hilo,” anasema mjasiriamali huyo.

Walifanikiwa kuruka kihunzi hicho cha kwanza ambapo barua zao zilipokelewa na mchakato wa kusubiri mkopo uliendelea.

Mtihani wa pili ulikuwa kutoka kwa mmoja wa maafisa wa Serikali ambaye baada ya kuidhinisha fedha kwenye kikundi hicho, aliwaeleza kuwa hawezi kuingizia fedha benki kabla hajamwachia kiasi fulani cha fedha.

“Alituuliza mnaniachaje fedha tayari zimeshaidhinishwa kiasi cha Sh12 milioni, nitoeni Sh500,000 hapo nikawawekee mzigo wenu,” anasema Mkulu akimnukuu afisa maendeleo huyo ambaye jina lake hakuweza kulikumbuka.

Anasema viongozi kwenye kikundi chao ambao ni watia saini walitazamana na kukubaliana kumpatia Sh200,000 ili kufanikisha suala hilo.

Kuhusu urejeshaji wa fedha hizo anasema mwanzoni walitia mkazo kuhakikisha fedha hizo wanazirudisha lakini baadaye waliacha na sasa ni mwaka wa tatu wanadaiwa deni.

Takwimu za Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zilizotolewa na Waziri Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha bajeti yake ya 2021/22 bungeni hivi karibuni alisema imetenga Sh64.5 bilioni kwa ajili ya mikopo kwa vikundi 18,244 vya wanawake, vijana na Watu wenye ulemavu. 

“Kati ya fedha hizo, Sh25.8 bilioni zilitengwa kwa ajili ya vikundi 8,223 vya wanawake, Sh25.8 bilioni kwa ajili ya vikundi 6,966 vya vijana na Sh12.9 bilioni kwa ajili ya vikundi 3,055 vya watu wenye ulemavu,” alisema Mwalimu Aprili, 2021.

Matumizi ya mikopo hiyo nayo changamoto

Licha ya kuwa mikopo hiyo inalenga kuwainua vijana, wanawake na walemavu kupitia shughuli za kiuchumi katika maeneo yao, baadhi ya waombaji wakishirikiana na viongozi wasio waaminifu hubadili matumizi ya fedha hizo na kuzipeleka katika shughuli binafsi.

Mama lishe katika eneo la Buhongwa jijini hapa, Ratifa Mgozya anasema yeye pamoja na wajasirimali wengine 17 walifanikiwa kupata mkopo wa halmashauri lakini baadaye waligawana kila mtu kwenda kufanya shughuli zake.

“Mara ya kwanza kikundi tulipata kiasi cha Sh1 milioni, mara ya pili tukapa Sh2 milioni na mara ya tatu tulipata Sh3 milioni,” anasema Ratifa ambapo andiko la mradi walilowasilisha ni lilikuwa kupata fedha za kuendeshea duka la nafaka. 

Hata hivyo, Ratifa na wenzake hawakuweza kuendesha mradi waliokusudia badala yake waligawana fedha hizo na kila mmoja kufanya shughuli yake.

“Ni ngumu kufanya shughuli ya pamoja wakati huo tuna familia inatutegemea mahitaji ni mengi yakiwemo ya wanafunzi, fedha hizo tuligawana na kila mmoja kufanya anayoona inamwingizia kipato kisha kuweka mkakati wa kuchangia kiasi kwa ajili ya marejesho na tumefanikiwa na hii ni mara ya tatu sasa tunapata mkopo,” anasema Ratifa.

Mikopo hiyo ni sehemu ya asilimia 10 ya mapato inayotengwa na kila halmashauri ya Tanzania Bara kwa ajili ya vijana ambao hupata asilimia nne, wanawake (asilimia nne) na walemavu asilimia mbili.

Mjasirimali wa kufuma vikapu na mikeka katika mtaa wa Rufiji jijini Mwanza, Veneranda Joseph anasema hamasa ya kuomba mikopo ilikuja baada ya viongozi wa Serikali kuwashawishi kuomba ili kujikwamua kiuchumi.

“Tulikuwa na kikundi cha watu 20 tukakisajili, lengo ni kuboresha sehemu ya kufumia vikapu na kuongeza mitaji, kiasi tulichoomba ni Sh5 milioni lakini tukapata Sh1 milioni kiasi ambacho hakitoshelezi,” anasema Veneranda.

Anasema kiwango cha mikopo kinachotolewa tofauti na kinachoombwa ni kidogo kiasi kwamba hakiwezi kutosheleza lengo mahususi.

“Huwa tunaishia kugawana tu kila mmoja anaenda kufanya shughuli yake ambayo inaweza kumwingizia kipato kisha tunawekeana mikakati ya kurudisha hadi mkopo utakapoisha,” anasema  Dotto Amos mfanyabiashara wa nguo za watoto jiji hapa.

Wafanyabiashara wa dagaa wakiwa katika mwalo wa Mswahili jijini Mwanza wakiandaa dagaa kwa ajili ya kuuza. Picha| Mariam John.

 

Serikali yashikilia msimamo wa sheria

Licha ya malalamiko ikiwemo wanawake na vijana kupewa kiasi kidogo cha fedha, Serikali mkoani Mwanza imesema mikopo hiyo hutolewa kulingana na fedha walizonazo na hawawezi kukidhi mahitaji ya waombaji wote.

Afisa Maendeleo ya Jamii jijini Mwanza, Adily Mrema anasema katika utoaji wa mikopo hiyo huzingatia zaidi andiko la mradi, uhalisia wa utekelezaji wake kutoka kwa wanakikundi. 

Mrema anasema wanazingatia sheria ya utoaji wa mikopo hiyo na si vinginevyo ikiwemo kuwapatia watu mikopo walio kwenye vikundi bila kujali itikadi zao za vyama. 

Anasema mikopo ikitolewa, wana utaratibu wa kuwafuatilia wahusika kupitia maafisa wa maendeleo ya jamii katika kata ili kujua kama miradi iliyoombea fedha ipo na inajiendesha.

“Hatua tunazochukua kwa vikundi ambavyo havijarejesha mikopo ni kuwafuatilia  kujua changamoto yao na kuwashauri kubadilisha biashara nyingine ili waweze kufanya marejesho,” anasema Mrema.

Hata hivyo, anasema mchakato wa marekebisho ya sheria inayosimamia mikopo hiyo unafanyika ili kushughulikia changamoto mbalimbali ambazo zimejitokeza ikiwemo uchepushaji wa matumizi ya mikopo hiyo.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Mwanza, Seleman Sekiete anasema kila mwananchi mwenye sifa ya kupata mikopo hiyo anakaribishwa kupeleka maombi bila kujali itikadi ya chama chake wala kabila.

“Serikali iliweka fedha hizi ili kuhakikisha mjasirimali anakuza kipato chake na Taifa kwa ujumla, hivyo kwa yeyote anayetaka kupata mkopo huo hana budi kuomba ili aweze kuongeza kipato cha familia,” anasema Sekiete na kuongeza kuwa,

“Tuhuma hizo si za kweli, tunaotoa fedha kwenye vikundi vyote viwe vya kijasiriamali viwe vya chama au siyo.”

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV