Wizara ya Utumishi yapokea asilimia 60 bajeti ya 2022-23
- Uchambuzi wabaini upatikanaji wa fedha katika wizara hiyo si wa kuridhisha.
- Serikali yatakiwa kutoa fedha zote zilizoidhinishwa kabla ya mwaka wa fedha kuisha.
- Huenda bajeti ya wizara hiyo ikaongezeka mwaka ujao wa fedha na kufikia Sh1 trilioni.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Dk Joseph Mhagama amesema utoaji wa fedha za bajeti kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora si wa kuridhisha, jambo linaloweza kuchelewesha utekelezaji kazi za wizara hiyo.
Hadi Februali 23, 2023 wizara hiyo ilikuwa imepokea Sh515.8 bilioni sawa na asilimia 60.8 ya bajeti yote ya wizara hiyo kwa mwaka 2022/23.
Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/23 ni Sh851 bilioni. Kati ya fedha hizo, Sh670 bilioni zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kiasi kilichobaki kilikuwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, hadi kufikia Februali 23 wizara hiyo imepokea asilimia 77.7 ya fedha zote za maendeleo.
“Kwa uchambuzi huo kamati ina maoni kwamba mwenendo wa upatikanaji wa fedha kwa ujumla si wa kuridhisha, kamati inaishauri Serikali kwamba fedha zote zilizoidhinishwa na bunge kwa ajili ya taasisi zilizo chini ya ofisi hii zinapatikana kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2022/23,” amesema Mhagama.
Mhagama aliyekuwa akisoma taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo kwa mwaka 2022/23 na mapendekezo ya bajeti ya mwaka ujao amesema ni taasisi tatu pekee kati ya saba zilizo chini ya ofisi ya Rais ndiyo zimepata zaidi ya asilimia 66.6 ya fedha zilizoidhinishiwa hadi Februali 23, 2023.
Taasisi hizo ni ofisi ya Rais Ikulu iliyopata asilimia ya 61.1 ya fedha iliyotengewa, Sekretarieti ya baraza la mawaziri iliyopata asilimia 60 na Menejimenti ya Umma na Utawala bora iliyopata asilimia 75.7.

George Simbachawene Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora alipokuwa akisoma mapendekezo ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 bungeni jijini Dodoma. Picha l Uhondo Tv.
Bajeti yapanda
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeliomba Bunge kuidhinishiwa bajeti ya Sh1 trilioni kwa mwaka 2023/24.
Kati ya fedha hizo, Sh200.45 bilioni ni za miradi ya maendeleo na kiasi kilichobaki kitatumika kwa matumizi ya kawaida
Bajeti hiyo imepanda kutoka Sh851,08 bilioni ya mwaka 2022/23.
“Jumla kuu ya Bajeti ninayoomba kwa mafungu yote yaliyo chini ya Ofisi ya Rais (Ikulu na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora) kwa mwaka 2023/24 ni Sh800.65 bilioni kwa matumizi ya kawaida na Sh200.45 kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” amesema Waziri wa wizara hiyo Simbachawene wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake leo Aprili 19, 2023 Bungeni jijini Dodoma.
Soma zaidi
-
Serikali yatoa kauli Watanzania waliopo Sudan, yalaani mapigano
-
Watalii waongezeka kwa asilimia 25.4 Tanzania
-
Ahueni, maumivu: Bei za vyakula zikianza kushuka Mwanza
Ikiwa bajeti hiyo itapitishwa fedha ya matumizi ya kawaida itakuwa imeongezeka kwa asilimia 17.18 huku ile ya maendeleo ikiongezeka kwa asilimia 8.5 pekee ikilinganishwa na ya mwaka 2022/23.
Vipaumbele vya Wizara
Waziri Simbachawene amesema mwaka ujao wizara yake itajikita kuongeza matumizi ya Tehama ili kuwafikia wananchi kiurahisi pamoja na kuimarisha uwajibikaji wa pamoja miongoni mwa viongozi wa umma hasa katika suala la viongozi kukinzana.
Vipaumbele vingine ni kuwezesha upatikanaji wa wataalam katika utumishi wa umma pamoja na kuendesha na kusimamia michakato ya ajira kwa ajili ya kuwezesha waajiri kupata watumishi wenye sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa miundo ya utumishi husika.
Latest