Bajeti Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi yapungua kwa asilimia 2
- Upungufu huo umeathiri bajeti ya miradi ya maendeleo ya wizara hiyo.
- Bajeti ya matumizi ya kawaida yaongezeka kamati ya Bunge yasema itaongeza motisha.
- Jumla ya kilomita 3,934.7 za barabara za lami kujengwa mwaka ujao.
Dar es Salaam. Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeomba kuidhinishiwa jumla ya Sh3.5 trilioni ili kutekeleza majukumu yake kwa mwaka 2023/24 ambapo bajeti hiyo imepungua kwa asilimia 2 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka huu.
Bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2022/23 unaoisha Juni 30 mwaka huu ilikuwa Sh3.8 trilioni.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa aliyekuwa akisoma hotuba ya bajeti ya wizara hiyo leo Mei 22, 2023 jijini Dodoma, amewaambia Wabunge kuwa kati ya fedha hizo, Sh1.4 trilioni ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi na Sh 2.08 trilioni zitaenda sekta ya uchukuzi.
“Katika fedha inayoombwa sekta ya ujenzi, Sh48.3 bilioni itatumika kwa matumizi ya kawaida na Sh1.4 ni kwa ajili ya maendeleo na katika sekta ya uchukuzi Sh118 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku Sh1.9 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo,” amesema Mbarawa bungeni Jijini Dodoma.
Pamoja na bajeti ya jumla kupungua, bajeti ya miradi ya maendeleo nayo imepungua kwa asilimia 5.7 katika sekta ya ujenzi na asilimia 3.5 katika sekta ya uchukuzi.
Zinazohusiana
-
Miradi 9 itakayobadilisha sura ya mawasiliano, habari Tanzania
-
Latra kuwatumia mawakala kufanikisha huduma za usafirishaji
Bajeti matumizi ya kawaida yaongezeka
Licha ya kupungua kwa bajeti ya miradi ya maendeleo neema imeonekana kwenye bajeti ya matumizi ya kawaida ambapo imeongezeka kwa asilimia 35 katika sekta ya ujenzi na asilimia 25 kwa sekta ya uchukuzi.
Seleman Kakoso ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu aliyekuwa akisoma uchambuzi wa bajeti hiyo amewaambia wabunge kuwa hatua hiyo itaongeza motisha kwa watumishi kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
“Kamati inaipongeza Serikali kwa kuongeza fedha za matumizi mengineyo kwa kuwa hatua hiyo itaongeza motisha kwa watumishi kutimiza majukumu yao kwa ufanisi ingawa kamati haikubaliani na uamuzi wa Serikali kupunguza bajeti ya miradi ya maendeleo,” amesema Kakoso.
Vipaumbele vya Wizara mwaka ujao
Prof Mbarawa amebainisha kuwa katika sekta ya ujenzi miongoni mwa vipaumbele watakavyovitekeleza ni pamoja na ujenzi wa miradi saba ya barabara yenye urefu wa kilomita 2,035, ujenzi wa barabara ya Kibaha, Chalinze – Morogoro yenye urefu wa km 205 na ujenzi wa miradi mikubwa ya barabara nchini.
“Tutaendelea miradi ya ujenzi wa barabara iliyosainiwa mwaka 2022/23 yenye jumla ya kilomita 393.6 na kuendelea na ujenzi wa madaraja makuu mawili yaani Kigongo- Busisi, Mwanza na Pangani Tanga na kujenga madaraja maeneo mbalimbali nchini,” amesema Mbarawa.
Kwa mujibu wa waziri huyo, miradi hiyo ikikamilika itakuwa na jumla ya kilomita 3,934.7 za barabara za lami ambazo zitaongeza mtandao wa barabara za lami nchini Tanzania kufikia kilomita 15,522.52 .
Katika sekta ya uchukuzi Mbarawa amesema miradi itakayotekelezwa ni pamoja na mradi wa uboreshaji usafiri Ziwa Victoria, mradi wa uwezeshaji taasisi, mradi wa kuboresha bandari ya Dar es Salaam, ukarabati wa njia ya reli, ujenzi wa reli mpya ya kisasa pamoja na ununuzi wa rada.
Maombi ya fedha kwa mwaka 2023/24 pic.twitter.com/Yb6cuuXyyl
— Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (@WizarayaUJnaUC) May 22, 2023
Latest
