Wizara ya Elimu yatangaza fursa ya ufadhili wa masomo nje ya nchi
- Ufadhili huo utahusisha ada ya masomo, tiketi za ndege za kimataifa pamoja na malazi.
- Mwisho wa kutuma maombi ni Oktoba 1, 2025.
Arusha. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza fursa ya ufadhili masomo kwa wanafunzi wa kitanzania katika vyuo vikuu viwili vilivyopo nchini Ujerumani na Misri.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa leo Septemba 26,2025 ufadhili huo wa masomo utatolewa kupitia Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Ujerumani (GIU) na Chuo Kikuu cha Ujerumani huko Cairo (GUC) ambapo kigezo kikuu cha ufadhili huo ni ufaulu wa juu.
“Ufadhili wa masomo haya hutolewa kwa wanafunzi waliopata matokeo ya juu zaidi katika Mitihani ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) ya Cheti cha Elimu ya juu ya Sekondari (ACSEE), hususani wale waliopata matokeo bora zaidi ya Daraja la I,” imesema taarifa ya Wizara ya Elimu.
Ufadhili huo utahusisha ada ya masomo, tiketi za ndege za kimataifa pamoja na malazi katika katika mwaka wa masomo wa 2025/2026
Kwa mujibu wa wizara hiyo waombaji hao wenye ufaulu wa juu watapata nafasi ya kuchagua kati ya kozi 20 zinazopatikana katika vyuo vyote viwili ambapo katika Chuo cha GUC waombaji wanatakiwa kuchagua kati ya kozi za uhandisi wa Vyombo vya habari na teknolojia, uhandisi wa Habari na Teknolojia,
Nyingine ni Sayansi ya Uhandisi na Nyenzo, Famasi na Bioteknolojia, Sheria, Teknolojia, Biashara, Udaktari wa meno, Usanifu, Uhandisi na Sayansi na Sanaa.
Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Ujerumani kozi zinazotolewa ni pamoja na Uhandisi, Tehama, na Sayansi ya Kompyuta, Utawala wa Biashara, Uhandisi wa Dawa, Bayoteknolojia na Tiba ya mwili.
Sifa za maombi
Mbali na sifa kuu ya kuomba ufadhili huo kuwa ni ufaulu wa juu Wizara ya Elimu imeanisha sifa yinginezo ikiwemo kusomea sayansi, sanaa au michanganyiko ya biashara inayolingana na programu iliyochaguliwa ya masomo.
Muombaji pia anatakiwa kuwasilisha nakala zilizoidhinishwa za vyeti vya kitaaluma pamoja na kufaulu vizuri mitihani ya awali ya vyuo vya GUC/GIU ikiwemo majaribio katika taaluma maalumu kama vile uhandisi, Usanifu na Sanaa Inayotumika.
Aidha, muombaji anatakiwa pia kuonesha uwezo thabiti wa Lugha ya Kiingereza huku akitakiwa kuhahakisha anapata ufaulu wa juu wa hadi wastani wa ufaulu (GPA) wa 3.0 (katika mfumo wa kijerumani) katika kila muhula wa masomo.
Waombaji wanatakiwa kuwasilisha barua rasmi ya maombi, pamoja na nakala zilizoidhinishwa za vyeti vya kitaaluma kupitia barua pepe ps@moe na dhe@moe.go.tz. kabla ya Oktoba 1, 2025.
Latest
