Wizara ya Afya : Kuna ongezeko la visa Uviko-19, mafua Tanzania

December 13, 2023 4:59 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Visa vya Uviko – 19 vyaongezeka kutoka 37 mwezi Oktoba hadi 65 mwezi Disemba.
  • Wizara ya Afya yawataka Watanzania kuendelea kuzingatia kanuni za afya hata kama hali ya Uviko -19 ipo chini.

Dar es Salaam. Wizara ya Afya nchini Tanzania imebainisha uwepo wa ongezeko la visa vya homa ya Uviko-19 pamoja na visa vya mafua yanayotokana na influenza katika kipindi cha mwezi Oktoba mpaka Disemba.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya na kusainiwa na  Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu imebainisha kuwa takwimu za ufualitiliaji (surveilance) za Wizara ya Afya zinaonesha ongezeko la visa vya ugonjwa wa UVIKO-19 toka visa 37 mwezi Oktoba 2023 na hadi visa 65 mwezi Disemba 2023.

“Aidha, ongezeko hili ni sambamba na ongezeko la visa vya mafua yanayotokana na influenza kutoka visa 34 hadi 49 katika kipindi hicho hicho,” imebainisha taarifa hiyo.

Taarifa ya wizara inakuja siku chache mara baada ya uwepo wa tetesi za ongezeko la homa ya Uviko -19 ambapo baadhi ya vyombo vya habari viliripoti vikinukuu Shirika la Afya Duniani WHO.

Hata hivyo, taarifa hiyo imebainisha kuwa kuwa ongezeko kama hilo liliripotiwa mwaka 2022 kipindi kama hiki ambapo  visa vya Uviko-19 viliongezeka toka 15 (Oktoba) hadi kufikia 65 (Disemba), wakati Influenza vilikuwa visa 2 hadi 59 katika kipindi hicho hicho.

Wizara ya Afya imewatoa hofu Watanzania ikibainisha kuwa Uviko -19 umeendelea kuwepo kwa kiwango cha chini kama magonjwa mengine ya mfumo wa njia ya hewa ukiongezeka na kupungua kwa nyakati tofauti za majira ya mwaka ambapo virusi vya Influenza vilivyobainika hapa nchini havina madhara makubwa ndio sababu iliyopelekea kuitwa ugonjwa wa majira (Seasonal Influenza).


Soma zaidi : 25 wajeruhiwa, mmoja afariki gari ikitumbukia mtoni Mwanza


“Ndugu Wananchi, Wizara inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa na inaelekeza wataalam katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya kuendelea kufanya utambuzi kwa njia ya vipimo vya maabara na kutoa matibabu stahiki… 

…Vilevile, Wizara inashauri wananchi kuwahi kwenye Vituo vya kutolea huduma mara wapatapo dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa zikiwemo mafua, kikohozi, kuwashwa koo, kupumua kwa shida, homa na kuumwa kichwa,” imebainisha taarifa ya wizara

Pamoja na hayo Watanzania wametakiwa kuendelea kuzingatia kanuni za afya ikiwa ni pamoja na kutoshikana mikono ikiwa si lazima kufanya hivyo, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi mara kwa mara na kuzingatia usafi binafsi na mazingira.

Kanuni nyingine ni pamoja na kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya pamoja na kuvaa barakoa pale inapohitajika na kupata chanjo kamili ya Uviko-19 kwa wote ambao hawajachanja au kukamilisha chanjo.

Enable Notifications OK No thanks