Wilaya 23 zinazokabiliwa na usikivu hafifu wa redio Tanzania

July 16, 2022 6:46 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni redio za TBC Taifa na TBC FM za Shirika la Utangazaji Tanzania.
  • Serikali yaahidi kuboresha usikivu. 

Dar es Salaam. Licha ya redio kuwa chombo muhimu cha wananchi kupata taarifa za maendeleo, wilaya 23 ikiwemo Tabora Vijijini bado zinakabiliwa na changamoto ya usikivu hafifu wa redio za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC). 

TBC ambayo ni shirika kongwe la utangazaji Tanzania kwa takriban miaka 22 lina vituo viwili vya redio vya TBC Taifa na TBC FM ambavyo hurusha matangazo yake katika maeneo mbalimbali nchini.

Hata hivyo, redio hizo hazijafika kikamilifu katika baadhi ya wilaya,  jambo linalofanya baadhi ya maeneo kutokuwa na usikivu kabisa au kuwa na usikivu hafifu wa redio za shirika hilo.

Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa mwaka wa fedha wa 2022/23, wilaya 23 hazina usikivu mzuri wa redio na nyingine hazina usikivu kabisa wa redio za TBC.

Redio ni moja ya aina ya vyombo vya habari vinavyowafikia watu wengi zaidi nchini kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za hivi karibuni.

Wilaya zilitajwa kupata changamoto hiyo ni Kibiti na Mafia za mkoani Pwani, Mvomero, Gairo, Kilosa, Ulanga, Malinyi (Morogoro), Mafinga (Iringa), Rungwe na Busekelo (Mbeya), Tabora Vijijini na Urambo mkoani Tabora.

Wilaya nyingine ni Biharamulo mkoani Kagera, Simanjiro (Manyara), Iramba, Ikungi, Mkalama na Singida Vijijini (Singida), Mbinga na Sumbawanga Vijijini (Rukwa), Shinyanga Vijijini na Kishapu (Shinyanga), na Mkinga mkoani Tanga.


Zinazohusiana:


Kati ya wilaya zilizotajwa, Mkoa wa Morogoro ndiyo una wilaya nyingi Tanzania ambazo zina changamoto ya usikivu wa redio za TBC.

Kwa mujibu wa hotuba hiyo Morogoro imetoa wilaya nne sawa na asilimia 17.4 ya wilaya zote zenye changamoto ya usikivu wa redio.

Ripoti hiyo inaeleza zaidi kuwa kwa sasa ni wilaya 107 ndiyo zenye uwezo wa kupata usikivu mzuri wa redio za TBC.

Hata hivyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema wizara inatarajia kutumia Sh13.1 bilioni kufanya upanuzi wa vituo vya usikivu nchi nzima na kuboresha miundombinu ya habari na mawasiliano itakayowezesha ubora wa  tasnia ya habari na mawasiliano ikiwemo redio.

Licha ya changamoto hizo za usikivu, redio bado ni chombo muhimu kinachotegemewa na Watanzania wengi hasa wa vijijini kupata taarifa za maedneleo.

Ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Repoa wa Afrobarometer kwa mwaka 2017 inabainisha kuwa redio ndiyo chanzo maarufu cha habari miongoni mwa Watanzania baada ya matokeo kubainisha watu 45 kati 100 hupata habari kupitia redio kila siku. 

Hata hivyo, vituo vya redio vinakabiliwa na changamoto za uzalishaji wa maudhui bora, jambo linaloweza kuwakosesha wananchi taarifa za uhakika kuhusu maisha yao.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaeleza katika ripoti mpya ya mawasilino ya robo ya mwisho ya mwaka 2021 kuwa hadi Desemba mwaka 2021  kulikuwa na vituo vya redio 210 kutoka vituo 193 mwaka 2020.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW