WHO: Mtu aliyepona COVID-19 asimchangie damu mgonjwa anayeugua ugonjwa huo
- Ni kwa sababu damu hiyo haimsaidii mgonjwa.
Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limewashauri watu waliougua Uviko-19 na kupona kutochangia damu hususan wagonjwa wanaougua ugonjwa huo kwa sababu tafiti zinaonyesha damu hiyo haimsaidii mgonjwa.
Ushauri huo umetolewa na WHO baada ya jopo lake la kimataifa la wataalamu wa miongozo kuchambua matokeo ya majaribio 16 yaliyohusisha wagonjwa 16,236 ambao wana maambukizi lakini hawako mahututi na wale wagonjwa wa Uviko-19 walio mahututi.
Ingawa hatua za awali za utafiti huo zilionyesha matumaini, lakini utafiti wa sasa unaonyesha dhahiri kuwa mtu aliyeugua na kupona ugonjwa huo akimuongezea damu mgonjwa anayeugua sasa Uviko-19 haimsaidii kupata nafuu wala kupunguza uhitaji wake wa kuwekwa kwenye mashine ya kusaidia kupumua na zaidi ya yote unaongeza gharama na kuchukua muda mrefu kumuwekea damu mgonjwa.
WHO imepinga vikali matumizi ya damu kwa mtu aliyeugua na kupona kuwekewa wagonjwa wanaugua sasa wasio mahututi na wale walio mahututi, isipokuwa tuu damu hiyo inaweza kutumika katika muktadha wa kufanya majaribio yaliyodhibitiwa bila mpangilio (RCT).
