Waziri Kanyasu ataka tathmini ifanyike ajira hoteli za kitalii Tanzania

March 26, 2019 3:53 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema ipo haja ya kuufanyia tathmini mfumo wa elimu kufuatia nafasi za juu katika hoteli nyingi za kitalii nchini kushikwa na raia wa kigeni wakati wazawa wana uwezo kuendesha hoteli hizo.
  • Amesema mtindo wa hoteli hizo kutumia Mameneja wa kigeni unalenga kuficha taarifa muhimu hususan taarifa  za kodi.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amesema ipo haja ya kuufanyia tathmini mfumo wa elimu kufuatia nafasi za juu katika hoteli nyingi za kitalii nchini kushikwa na raia wa kigeni. 

Akizungumza mara baada kufanya ukaguzi katika hoteli tano zikiwemo za Lobo na Soronera zilizopo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti; Wildlife (Hifadhi ya Ngorongoro) na Manyara iliyopo ndani ya Hifadhi ya Manyara, Kanyasu amesema imebainika kuwa hoteli zote alizokagua zinaongozwa na Mameneja wa kigeni ambao wote hawawezi kuzungumza  lugha ya Kiswahili.

Amesema kuwa  mfumo  wa elimu uliopo siyo kwamba unashindwa  kuandaa  Mameneja kushika nafasi katika hoteli hizo lakini Tanzania ina wasomi wengi waliosomea masomo ya hoteli lakini wengi wao wako mtaani wanatafuta ajira.

“Tatizo langu si kwa sababu nafasi hizo zimeshikwa na wageni, lazima tujiulize kwa nini kila hoteli Meneja wake  ni wa kigeni,” amehoji Kanyasu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii, tathmini hiyo inalenga kupitia ubora wa wataalamu wanaozalishwa na uwezo wao katika  kushika nafasi hizo pia kuangalia elimu inayotolewa kama inakidhi  mahitaji yaliyopo.

Kanyasu amesema mtindo wa hoteli hizo kutumia Mameneja wa kigeni unalenga kuficha taarifa muhimu hususan taarifa  za kodi na kuwadumaza wazawa badala yake wanajikuta hawajui chochote kuhusiana na uendeshaji wa  hoteli hizo.

“Mwanzo ilidaiwa kuwa nafasi hizo haziwezi kushikwa na Wazawa kwa vile hawajui kuongea vizuri kiingereza ila kwa sasa wapo wanaojua kuzungumza na kuandika lugha ya Kiingereza vizuri kuliko baadhi ya  Mameneja wa kigeni,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa leo (Machi 26, 2019).

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu (kulia) akiongea na Meneja wa hoteli ya Manyara, Bahram Aswart. Picha|Wizara ya Maliasili na Utalii.

Kanyasu ambaye ametembelea hoteli hizo kwa nyakati tofauti amesema nafasi hizo za juu zinazoshikwa na wageni siyo za kitaalamu kiasi kwamba zikishikwa na wazawa utendaji utasimama badala yake wazawa wamekuwa wakifanya kazi za daraja la chini kwa malipo kidogo ikilinganishwa na wageni.


Zinazohusiana: 


Katika hatua nyingine, Kanyasu amewashauri wamiliki wa hoteli hizo wapunguze bei kipindi cha msimu wa watalii wachache ili kuwawezesha watalii wa ndani kuweza kumudu gharama badala ya kuzifunga wakati wa msimu huo.

Wamiliki hao wameshauriwa waangalie namna ya kutofautisha bei za malipo ya hoteli kwa watalii wa ndani na watalii wa nje ili kukuza utalii wa ndani.

Meneja wa hoteli ya Lobo, Asram Anuary amesema suala la kushusha bei kwa watalii wa ndani kipindi cha watalii wachache wa kutoka nje ni wazo zuri hivyo watashauriana menejimenti ili waweze kuona uwezekano huo.

Enable Notifications OK No thanks