Miamala ya kifedha simu za mkononi yafikia Sh7.8 trilioni kwa mwezi Tanzania

July 5, 2019 11:04 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Thamani ya fedha hizo ni kwa miamala yote iliyofanyika kupitia huduma za simu za mkononi Machi 2019.
  • Kampuni tatu za Vodacom, Tigo, na Airtel zilifanikisha miamala yenye thamani ya Sh7.66 trilioni Machi 2019 pekee ikiwa ni sawa na asilimia 98 ya thamani ya miamala yote. 

Dar es Salaam. Hapana shaka kasi ya Watanzania kutumia simu za mkononi katika huduma za kifedha inazidi kuongezeka siku hadi siku baada ya Ripoti mpya ya Takwimu za Mawasiliano ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuonyesha kuwa miamala inayofanywa katika huduma hiyo imeongezeka kwa zaidi ya Sh1 trilioni ndani ya mwezi mmoja.

Ripoti hiyo ya robo ya kwanza ya mwaka 2019, inabainisha kuwa mwezi Machi pekee miamala ya fedha iliyofanywa katika simu za mkononi sasa imefikia Sh7.82 trilioni kutoka Sh6.7 trilioni iliyorekodiwa Februari mwaka huu.

Katika mwezi huo wa Machi watumiaji wa huduma hiyo walifanya miamala milioni 243.5 ikiwa ni juu kidogo kutoka miamala milioni 215 ya Februari.

Hata hivyo, thamani ya miamala ya Machi mwaka huu licha ya kuongezeka kidogo ndani ya mwezi mmoja bado haijafikia kiwango cha thamani ya miamala iliyofanywa Januari 2019 cha Sh7.84 trilioni.

Kati ya kampuni sita zinazotoa huduma za kifedha katika simu za mkononi, kampuni kubwa tatu za Vodacom kupitia M-pesa, Tigo (Tigo-Pesa) na Airtel kupitia Airtel Money kwa pamoja zilifanya miamala yenye thamani ya Sh7.66 trilioni sawa na asilimia 98 ya thamani ya “mpunga” wote.

Hii ina maana kuwa kila miamala yenye thamani ya Sh100 iloiyofanywa kwenye simu za mkononi Machi mwaka huu, Sh98 ilifanywa na mitandao hiyo mikubwa ya Vodacom, Tigo na Airtel. Mitandao iliyosalia ya Zantel (Ezy Pesa), TTCL (TTCL PEsa) na Halotel kupitia Halo Pesa inagawana kiwango kilichosalia.


Soma zaidi: Watumiaji wa huduma za simu benki wazidi kupaa Tanzania, wafikia milioni 23


Huduma za kifedha kwenye simu za mkononi zimekuwa mkombozi katika nchi zinazoendelea kuwapa huduma za fedha watu ambao ilikuwa ni ngumu kufikiwa na huduma za benki hususan waishio vijijini. Miongoni mwa huduma zinazotumika zaidi kupitia simu za mkononi ni pamoja na kutuma na kupokea pesa, mikopo midogo midogo, bima, na huduma za akiba.

“Huduma za fedha za simu zinawasaidia watumiaji kupata fursa ya kukopa na kuweka akiba hasa kwa watu wasiopata huduma za benki.

“Hii ni inawapa fursa watumiaji kufungua fursa nyingine za kupata mikopo benki katika baadhi ya nchi baada ya kuwa na kuwa na rekodi nzuri katika ukopaji kwa kuunganisha mtandao wa simu na akaunti za beni kama M-Shwari (Kenya), MTNQuikloan (Ghana) na Tigo Nivushe nchini Tanzania,” inasomeka ripoti ya GSMA mwaka 2018.  

Takwimu hizo za TCRA zinabainisha kuwa Machi 2019 kulikuwa na watumiaji wa huduma za kifedha katika simu za mkononi milioni 22.76 ikiwa ni juu kidogo ya watumiaji milioni 22.29 waliokuwepo Januari mwaka huu.

Enable Notifications OK No thanks