Watalii, mapato yapaa hifadhi ya Taifa Ngorongoro
- Katika mwaka wa fedha wa 2021/22, Serikali iliingiza Sh73.8 bilioni kutoka Sh31.5 bilioni za mwaka 2020/21.
- Watali nao waanza kuongeza baada ya Uviko-19.
- Serikali yaendelea kuwahamisha wakazi wa eneo hilo kupisha uhifadhi.
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea na zoezi la kuwahamisha wakazi wa Ngorongoro kwenda mkoani Tanga, mapato yanayotokana na shughuli za utalii yameongezeka zaidi ya mara mbili ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita katika hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.
Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dk Christopher Timbuka hadi kufikia Juni 23, kaya zilizohama kwa hiari yao kutoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga katika awamu ya kwanza na ya pili ni 48 zenye jumla ya watu 233 na mifugo 899.
Wananchi hao wanahama ili kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo ambalo ni hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ambayo ni kivutio kikubwa cha watalii duniani.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, katika mwaka wa fedha wa 2021/22, Serikali iliingiza Sh73.8 bilioni zilizotokana na shughuli za utalii kutoka Sh31.5 bilioni zilizopatikana mwaka 2020/21.
Hilo ni sawa na ongezeko la Sh42.4 bilioni au sawa na kusema zaidi ya mara mbili ya fedha zilizozalishwa mwaka uliopita.
Ongezeko hilo la mapato limechangiwa na kuongezeka kwa watalii ambapo mwaka huu ambao unaisha Juni 30 idadi ya watalii waliotembelea hifadhi hiyo walikuwa 347,328 kutoka 191,614.
Takwimu za mapato na watalii za mwaka 2021/22 ni hadi Aprili 2022.

Hata hivyo, idadi ya mapato na watalii waliotembelea hifadhi hiyo iliyopo mkoani Arusha katika miaka miwili iliyopita ni ndogo ikilinganishwa na miaka ya nyuma kwa sababu katika kipindi hicho shughuli za utalii zilipungua kwa sababu ya Uviko-19.
Mathalan, mwaka 2018/19, watalii 700,710 walitembelea Ngorongoro lakini mwaka uliofuata idadi iliongezeka hadi 707,051 kabla haijaporomoka zaidi katika miaka miwili iliyofuata.
Hata hivyo, idadi ya watalii na mapato ya hifadhi hiyo inayosifika kuwa na wanyamapori mbalimbali wakiwemo nyumbu huenda vikaanza kuongezeka kwa sababu ya hatua zilizochukuliwa kudhibiti Uviko-19 ikiwemo kutoa chanjo.
Soma zaidi:
Mikakati ya Serikali kuendeleza hifadhi Ngorongoro.
Moja ya mkakati wa Serikali kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii katika hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 8,300 ni kuwahamisha wakazi wa eneo hilo kuwapeleka Tanga.
Serikali kwa kushirikiana na Uongozi wa mikoa ya Arusha na Tanga imekamilisha ujenzi wa nyumba 103 katika eneo la Handeni ambazo ni awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 500 kwa ajili ya wananchi wenyeji waishio ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Licha ya zoezi hilo kuibua mijadala mingi, miongoni mwa wabunge na wananchi juu ya kuhamishwa wananchi wa eneo hilo, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa zoezi hilo limezingatia haki za binadamu na wanaondoka.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao amesema wanaendelea kuboresha na kutumia njia za kidigitali ikiwemo Ngorongoro “live streaming” kutangaza mubashara vivutio na matukio mbalimbali kutoka hifadhini.
Mikakati mingine ni kujenga barabara kilomita moja kutoka makutano ya Seneto na Kreta ya Ngorongoro kwa kiwango cha tabaka gumu la mawe, kuboresha nyanda za malisho kwa kudhibiti mimea vamizi kupitia moto mpango, kung’oa, kufyeka na kuwezesha utafiti mbalimbali.
Latest