Jinsi ya kuepuka kutapeliwa kwenye Forex 

January 17, 2025 6:49 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kwa kufanya utafiti wa kina pamoja na kujielimisha kila siku.
  • Inashauriwa kuepuka kununua ‘signals’ pamoja na ‘auto trading’.

Dar es Salaam. Forex ni biashara inayovutia watu wengi kwa sababu ya uwezekano wa kupata faida kubwa, ingawa kwa upande mwingine ni eneo linalovutia matapeli kwa sababu ya ukosefu wa uelewa wa kutosha kwa baadhi ya wawekezaji hasa wale wanaofanya biashara hiyo kwa mara ya kwanza.

Mara baada ya kuangazia maana ya biashara ya Forex na jinsi ya kuifanya kwa mafanikio, makala hii inaangazia jinsi unavyoweza kuepuka kutapeliwa pesa zako kupitia Forex.

Forex inaweza kuwa bora kama tu ukiwa makini na kujifunza Picha | Shutterstock

Utapeli kwenye Forex ni nini?

Utapeli kwenye Forex unahusisha mbinu za udanganyifu kutoka kwa mawakala au watu wanaojitanabaisha kuwa wakufunzi, wawekezaji au wenye uzoefu na uelewa mpana wa Forex zinazolenga wawekezaji wasio na uelewa wa kina wa soko.

Wageni wa Forex hutapeliwa kwa huahidiwa faida kubwa na ya haraka, bila kuelezwa hatari halisi zinazohusiana na biashara ya Forex.

Kwa mfano, ripoti ya FX Scouts ya mwaka 2020 ilionyesha kuwa matapeli hutumia mitandao ya kijamii kujenga uaminifu kabla ya kuwashawishi waathirika kujiunga na mipango ya biashara ya kitapeli. 

Matukio kama haya yameathiri maelfu ya Watanzania, hasa vijana waliovutiwa na ahadi za pesa za haraka.

Juma (sio jina lake halisi), kijana wa Kitanzania, alijikuta kwenye mtego wa programu inayojulikana kama Inclusive. Programu hii iliahidi mara mbili ya kiasi alichowekeza ndani ya siku 30 au 60. 

Kwa kuwa alikuwa mwanafunzi wa chuo na alitaka kuongeza kipato chake, Juma aliwekeza TZS 200,000, fedha alizopata kupitia boom.

Awali, Juma alishawishika zaidi baada ya kuonyeshwa video za watu waliodai kufanikiwa kupitia programu hiyo.

 Pia, alijiunga na kundi la WhatsApp ambalo lilidaiwa kuwa na wanachama waliokuwa wawekezaji wa Inclusive. Lakini, baada ya wiki chache, programu hiyo ilisitisha kazi ghafla, na Juma pamoja na wawekezaji wengine wakapoteza pesa zao.

Jinsi ya kuepuka utapeli 

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya fedha na mawakala wa Forex kama FxScouts Group Tanzania,  njia mojawapo ya kuepuka kutapeliwa ni pamoja na Hakikisha Uhalali wa Wakala ambapo kabla ya kuwekeza, unapaswa kuhakikisha wakala wako amesajiliwa na mamlaka zinazotambulika kama Financial Conduct Authority (FCA) au CFTC jambo linalotoa uhakika wa kuwa unafanya kazi na taasisi inayodhibitiwa kisheria.

Hata hivyo, kwa sasa Tanzania bado haina wakala rasmi anayetambuliwa na kusimamiwa na Serikali kwa kuwa bado Forex haijarasimishwa hivyo wengi wao ni kutoka nchi za jirani kama Kenya na Afrika Kusini, hivyo ni vyema kujiridhisha ikiwa wakala wako anatambulika na mamlaka za kisheria za nchi husika.

Mawakala feki wa Forex hawapatikani tanzania tu bali sehemu zote ulimwenguni kwani biashara hii huunganishwa na intaneti Picha | Feepic.com

Aidha, wapo baadhi ya mawakala wa ndani ya Tanzania ambao hujinasibisha kama wawakilishi wa kampuni kubwa za Forex, unaweza kutumia tovuti rasmi za wakala ili kuthibitisha taarifa zao pamoja na kupitia leseni yake na kusoma maoni ya watu wengine kuhusu wakala huyo ambapo unaweza kuona kama kuna malalamiko.

Epuka ahadi za faida kubwa

Matapeli mara nyingi huahidi faida kubwa ndani ya muda mfupi, kumbuka, biashara ya Forex ni ina changamoto nyingi na faida si ya uhakika, hivyo unapaswa ujiulize maswali kila unapokutana na ofa ya ‘hakuna hasara’ au ‘faida ya haraka’ jiulize ikiwa ina mantiki na uchukue tahadhari.

Usikubali kuahidiwa pesa kubwa na wakala bila kujua hatari zake Picha | Donate.com

Fanya utafiti wa kina

Pamoja na kujifunza kuhusu Forex tumia muda wako kusoma maoni kutoka kwa wawekezaji wengine kuhusu wakala au programu ya biashara unayotaka kutumia na hakikisha unapata mapendekezo kutoka vyanzo vya kuaminika.

Unaweza kuchunguza historia ya kampuni kwa kuangalia muda ambao kampuni imekuwepo sokoni na jinsi ilivyoshughulikia malalamiko ya wateja wake aidha unaweza kuwauliza wafanyabiashara wa Forex wanaoaminika kwa maoni na ushauri kuhusu wakala unayetaka kumtumia.

Tumia demo akaunti kwanza

Ni muhimu kabla hujaamua kuwekeza kwenye akaunti halisi kufanya majaribio ya kutosha kwenye akaunti ya majaribio ‘demo account’ ili kuwa na uelewa mpana wa jinsi jukwaa linavyofanya kazi.

Aidha, unatakiwa ujihadhari ikiwa wakala atakushinikiza uwekeze hela yako mara moja kwenye akaunti halisi bila akaunti ya majaribio, hiyo inaweza kuwa ishara unatayarishwa kuibiwa.

Epuka kununua signals (ishara)

Kutokana na wengi wanaoingia kufanya biashara ya Forex kutokuwa na uelewa nayo, hukutana na watu wanaojitanabaisha kuuza ishara zitakazowasaidia wawekezaji kupata faida, hiyo ni aina nyingine ya utapeli.

Ukitaka kununua signals hakikisha chanzo kimeidhinishwa na unaweza kutumia akauti yako ya majaribio kujaribu ishara hizo kabla ya kuzitumia kwenye akauti ya pesa halisi.

Ishara za uongo zinaweza kuchangia kupoteza uwekezaji wako. Picha | Digital market

Epuka ‘Auto-Trading Bots’

Matapeli mara nyingi huuza programu za biashara zinazodai kuwa na uwezo wa kufanya biashara yenye faida bila uangalizi maarufu kama  ‘Auto-Trading Bots’, kama muwekezaji unatakiwa kufanya utafiti wa kina kabla ya kununua roboti yoyote.

Usitumie roboti bila uangalizi, unatakiwa kuhakikisha unadhibiti biashara zako hata kama unatumia programu za kusaidia.

Angalia ada na masharti ya biashara

Unapaswa kupiitia kwa kina mkataba wa biashara baina yako na wakala uliyeamua kumtumia, hakikisha unajua ada zote zinazotozwa na wakala kabla ya kuanza biashara kwa kuwa wakala waaminifu huwa na ada zilizo wazi na masharti yanayofahamika.

Elimika kila siku

Matapeli hutegemea ukosefu wa uelewa wa soko na kisha huja na mbinu mpya za kuibia watu, ili kuepuka kutapeliwa tenga muda wa kujielimisha mara kwa mara kuhusu mbinu za biashara, hatari zinazohusiana, na jinsi ya kudhibiti biashara yako.

Unaweza pia kuipata elimu hiyo kupitia mafunzo yanayotolewa na taasisi zinazotambulika ili kuboresha ujuzi wako.

Hata hivyo, jihadhari na kutegemea ahadi za mitandao ya kijamii pekee kama chanzo cha kuaminika kwa kuwa matapeli wengi hutumia mitandao ya kijamii kujenga uaminifu na kushawishi wawekezaji kwa kuonesha mafanikio yao kama magari, nyumba pamoja na vitu vya thamani.

Kujifunza kutakusaidia kuweza kujua njia za kufanya ili kulielewa soko na kujua nikipi cha kufuata. Picha | Digital Market

Tumia zana za usalama wa mtandaoni

Unaweza kutumia VPN kuzuia wavamizi kufuatilia taarifa zako au kuhakikisha faragha na usalama wa shughuli zako za mtandaoni aidha unaweza kulinda nywila zako kwa kutumia programu za kudhibiti nywila (password managers) na hakikisha nywila zako ni imara mapoja na kuweka mfumo wa Kuthibitisha Utambulisho kwa Hatua Mbili (2-factor authentication).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks