Rais Samia atengua uteuzi wa mganga mkuu wa Serikali, ahamisha wawili

January 17, 2025 7:41 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Atenguliwa siku tatu baada ya WHO kuripoti uwepo wa ugonjwa wa Marburg Tanzania

Arusha. Rais wa Tanzania  Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Mganga Mkuu wa Serikali Prof Tumaini Nagu na kumteua Elias Magembe kushika nafasi hiyo.

Prof Nagu aliyeitumikia nafasi hiyo kwa miaka mitatu tangu Oktoba, 2022 ametenguliwa ikiwa ni siku tatu tangu Shirika la Afya Duniani (WHO) kuripoti uwepo wa ugonjwa unaohisiwa kuwa ni marburg mkoani Kagera ambapo watu nane wamefariki.

Hata hivyo, Serikali ilikanusha madai hayo kwa kubainisha kuwa vipimo bya maabara vya wahisiwa havikuthibitisha uwepo wa ugonjwa huo ambao umewahi kutokea mkoani humo mwaka 2023.

Nafasi ya Prof Nagu sasa itashikiliwa na Dk Magembe ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akishughulikia masuala ya afya.

Aidha, taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk Moses Kusiluka iliyotolewa leo Januari 17, 2025 imebainisha kuwa Rais Samia amefanya uhamisho wa viongozi kutoka wizara nyingine mbili na uhamisho na uteuzi huo utaanza mara moja.

“Dk Seif Abdallah Shekalaghe amehamishwa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya…

…Dk John Anthony Jingu amehamishwa kutoka Wizara ya Afya kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, imesema taarifa ya Kusiluka.

Hii ni mara ya tatu kwa Rais Samia kufanya uteuzi ndani ya mwaka 2025, Januari 10 alifanya uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Wenyeviti wa Bodi na kumpangia kituo cha kazi balozi.

Uteuzi mwingine aliufanya Januari 15 mwaka huu akifanya uteuzi wa viongozi watano akiwemo Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Masoud Lwamo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks