Waokaji bidhaa za ngano wapata jukwaa kusemea kero zao

June 7, 2022 6:47 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Litatumika kuwasilisha na kutatua changamoto za waokaji Tanzania.
  • Ni baada ya kuzinduliwa kwa Umoja wa Waokaji Tanzania ( TBA).
  • Serikali yasema iko tayari kufanya nao kazi.

Dar es Salaam. Huenda waokaji wa bidhaa mbalimbali za ngano nchini Tanzania wakapata ahueni ya utatuzi wa changamoto zao zilizokuwa zikiwakabili mara baada ya kuzinduliwa kwa Umoja wa Waokaji Tanzania ( TBA), jambo lililoshindikana kwa miongo kadhaa.

Uzinduzi wa umoja huo ulifanyika katika ukumbi wa maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hivi karibuni na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Viwanda Uwekezaji na Biashara, Exaud Kigahe.

Mwenyekiti wa TBA Fransisca Lyimo amesema lengo la kuanzishwa kwa umoja huo ni kuwaleta pamoja waokaji, kutengeneza mtandao, kujadili fursa, kusaidiana katika utatuzi wa changamoto zinazowakabili pamoja na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya uokaji kwa wanachama.

Amesema pamoja na juhudi za serikali katika kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara na kulinda viwanda vya ndani bado wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo mrundikano wa kodi ambapo kiwanda cha uokaji ili kianze kinapaswa kutembelewa na taasisi zaidi ya 10 ambazo zote hutoza kiasi cha fedha na kusababisha watu wengi kushindwa kusajili viwanda vyao.

Changamoto nyingine ni kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ambayo zamani haikuwepo, mabadiliko ya bei za malighafi kama ngano, mafuta na sukari, kutokuwepo kwa uhalisia katika ushindani wa bei na uhaba wa vifungashio.

Mlolongo katika uagizaji wa viungo vya uokaji ambavyo havizalishwi nchini na kusababisha baadhi ya watu kuingiza bidhaa hizo bila kufuata utaratibu, ni miongoni mwa changamoto zinazowatesa waokoji.

Lyimo amewataka waokaji ambao bado hawajajiunga na umoja huo kujiunga ili kupata nguvu ya kushughulikia matatizo yanayowakabili kwa pamoja akisisitiza zaidi kwa vijana ambao wanafanya shughuli za uokaji.

“Kipekee napenda kuchukua nafasi hii kuwahamasisha waokaji ambao bado  hawajajiunga na chama hiki wajiunge ili waweze kuwa na nguvu ya pamoja katika kusimama…..sisi tuliosimama mbele yenu ni waasisi tu lakini tunategemea kuna vijana ambao wapo kwenye tasnia ya uokaji na bado wana nguvu nyingi wataendelea kupokea kijiti na kusimamisha tasnia ya uokaji,” amesema Lyimo.

Mwenyekiti wa TBA Fransisca Lyimo Akizindua nembo ya TBA na Naibu Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara Exaud Kigehe. Picha | Daudi Mbapani.

Naibu Waziri wa Uwekezaji,Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema umoja huo ni muhimu sana kwani utakwenda kuisaidia Serikali katika upatikanaji wa chakula kwani historia zinaonesha mataifa mengi yalipinduliwa madarakani kwa kukosekana kwa mkate 

Hivyo ameziagiza taasisi ambazo zipo chini ya wizara yake kama Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Shirika la viwanda vidogo Tanzania (SIDO) kuhakikisha wanatatua changamoto ambazo zinawakabili waokaji na kuacha urasimu mara moja bali watoe elimu kwa waokaji juu ya namna gani wanaweza kurasimisha bidhaa zao. 

“Nichukue nafasi hii kwa niaba ya Serikali nizielekeze taasisi zetu ambazo ndiyo zina wajibu wa kusaidia maendeleo ya sekta binafsi nahasa kwenye tasnia hii ya uokaji ikiwemo Tantrade, Sido, Tbs na taasisi nyingine tuongeze juhudi kwanza kuhakikisha tunatatua changamoto ambazo zipo leo,” amesema Kigahe.


Zinazohusiana


Waziri Kigahe ameongeza kuwa juhudi za Serikali zinalenga kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara ili ziweze kukua na kuchangia pato la Taifa ambapo inaendelea kufanya maboresho kwa kufuta kodi ambazo sio rafiki na zinazokwamisha biashara nchini.

“Hii tunalenga kodi ambazo zinatozwa kwa wafanyabiashara ambazo zinafanana fanana, yaani kodi moja inatozwa na taasisi mbili tatu hii si sahihi…kwa hiyo lazima tuangalie namna ya kumsaidia mfanyabiashara mdogo kurasimisha biashara yake,” amesema Kigahe.

Kwa upande wao waokaji waliofika katika uzinduzi wa taasisi hiyo wanasema wanaamini kuanzishwa kwa umoja huo umekuja wakati muafaka kwani utasaidia waokaji wachanga ambao wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali.

“Kama mwanachama wa Tanzania Bakers Association kitatusaidia sisi kutatua changamoto mbalimbali kuanzia kwenye upatikanaji wa masoko hata nje ya nchi pamoja na kupata mafunzo yanayotolewa na taasisisi za Serikali kama mamlaka ya Udhibiti wa Viwango vya Ubora (Tbs),” amesema Liliani Aroni, muokaji binafsi.


Tangazo:


Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW