Wanufaika wa bima ya afya waongezeka, Serikali ikijiandaa kutunga sheria mpya

July 30, 2019 12:18 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni wale wanaotumia mifuko ya NHIF na CHF iliyoboreshwa.
  • Idadi yao imeongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2015 hadi asilimia 33 mwaka 2019. 
  • Serikali iko mbioni kupitisha Sheria ya Bima ya mwaka 2019. 

Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Tanzania ikiwa katika hatua ya kutunga sheria mpya  itakayowafanya wananchi wote kuwa katika mfuko wa bima ya afya, idadi ya wananchi wanaotumia mifuko mwili ya bima ya afya ya umma imeongezeka  kwa asilimia 33. 

Mifuko hiyo ambayo imekuwa ikitumika kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF iliyoboreshwa). 

Ripoti ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu  ya Tanzania (Voluntary National Review (VNR) ya mwaka 2019 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaeleza kuwa NHIF na CHF vimekuwa vyombo muhimu katika upatikanaji wa huduma bora za afya na kuisaidia Tanzania kutekeleza malengo hayo kikamilifu ifikapo 2030. 

Ripoti hiyo iliyowasilishwa hivi karibu Umoja wa Mataifa (UN) inaeleza kuwa hadi kufikia Machi 31, 2019, NHIF ilikuwa na wanachama milioni 4.21 sawa na asilimia nane ya Watanzania wote. 

CHF iliyoboreshwa mpaka sasa imeweza kuwahudumia wanachama milioni 13.03 ambao ni sawa na asilimia 25 ya idadi ya watu wote Tanzania. 

“Kwa pamoja NHIF na CHF ufikiaji wa watu kati ya mwaka 2015 na 2019 umeongezeka kutoka asilimia 20 hadi 33,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.


Soma zaidi:


Licha ya mafanikio hayo, wadau wa sekta ya afya watakuwa na kibarua kigumu cha kuongeza idadi ya watu wanaotumia bima ya afya ikizingatiwa kuwa theluthi moja tu ya idadi ya watu Tanzania ndiyo imefikiwa walau kwa aina moja ya bima ya afya. 

Ripoti hiyo inaeleza kuwa Serikali ya Tanzania ipo katika hatua ya kutaka kupitisha Sheria ya Bima ya mwaka 2019 itakayowafanya watu wote kuwa katika mfuko mmoja wa bima ya afya (SNHI). 

Ikiwa sheria hiyo itapitishwa na kuanza kutekelezwa itawalazimisha watu wote kuwa na bima ikiwa ni hatua ya kuchagiza upatikanaji wa huduma za pamoja za afya kwa watu wote bila ubaguzi. 

Huenda hiyo itakuwa hatua kubwa ya kuiwezesha Serikali kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo 2030. 

Enable Notifications OK No thanks