Umemejua ulivyoboresha maisha ya wanakijiji Lindi
- Ni wakazi wa kijiji cha Namtumbwa kata ya Mbaya Wilaya ya Liwale.
- Wanautumia katika shughuli za uzalishaji na kiuchumi.
- Maisha yao yabadilika na kuwa bora zaidi.
Lindi. Ni Jumatatu tulivu majira ya saa 4 asubuhi nafika katika kijiji cha Namtumbwa kata ya Mbaya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi. Baadhi ya wenyeji wanaendelea na shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato.
Wapo vijana wanaofanya shughuli za uchomeleaji katika karakana iliyopo kijijini hapo, lakini pia wapo wanawake wanaoendelea na shughuli ya kukanda na kuoka mikate ambayo huuzwa kijijini hapo na vijiji jirani.
Shughuli hizo na nyingine zinaendelea kijijini hapo kwasababu wakazi wake wamefikishiwa nishati mbadala ya umemejua. Nishati hiyo ambayo ni safi na salama kwa afya na mazingira inasambazwa a kampuni ya PowerCorner Tanzania.
Ujio wa umeme huo kijijini hapo ni matokeo ya kutopitiwa na gridi ya Taifa ya umeme, jambo lililowafanya wanakijiji hao kuangazia nishati mbadala ili kuendeleza shughuli za maisha.
Mjasiriamali Ashura Hemed ni miongoni mwa wanufaika wa nishati hiyo ambayo imerahisisha biashara yake ya kuoka mikate ambayo imekuwa sehemu muhimu kukuza kipato cha familia.
“Nafanya shughuli za kuoka na kuuza mikate katika kijiji hiki na vijiji jirani vitatu, biashara ambayo kwa kiasi kikubwa imenisaidia kukuza kipato changu na mafanikio haya ni baada ya kijiji chetu kupata mradi wa umeme jua toka kampuni ya PowerCorner Tanzania,” anasema Ashura, mama watoto watatu.
Anasema kabla ya ujio wa mradi wa umemejua, yeye na wenzake walikuwa wakikanda unga wa mikate kwa kutumia mikoni na hivyo kupelekea kuchoka sana na isiyo na ubora.
“Kabla ya kupata mashine ya umeme tulikuwa tunatengeneza mikate ya kawaida ambayo haikuwa na ubora wala muonekano mzuri kwani tulikuwa tunatengeneza kienyeji na kukanda unga kwa kutumia mikono na ilihitajika muda wa kutosha na nguvu,” anasema Ashura na kuongeza;
“Sasa tuna mashine ya kukanda unga unakuwa laini kwa muda mfupi kisha tunaweka kwenye oveni na kuoka, kwa kweli mikate imekuwa bora yenye muonekano nzuri na yenye ladha ya kupendwa na wateja wengi zaidi kutoka vijiji vya Barikiwa, Nduruka na Kichonda na Namtumbwa,” anasema Ashura.
Mikate inayozalishwa na kikundi cha Ashura kwa kutumia umemejua huuzwa kati ya Sh500 hadi Sh1,000 ikilinganishwa na bei ya awali ya Sh100 hadi Sh200 ambapo mikate hiyo ilikuwa ikitengenezwa kienyeji na ilihitajika nguvu na muda mwingi kutengeneza.
Ashura anasema mbali na mradi wa mikate ana mradi wa karakana ya kuranda mbao na kuchomelea vitu mbalimbali na hivyo kuongeza kipato zaidi.
“Ingawa siingizi fedha nyingi sana lakini bado nashukuru kwa sababu watoto wangu wanasoma, nimeajiri vijana siyo chini ya watano na kipato nachopata nakipeleka kwenye shughuli nyingine kama kilimo ambapo naweza kuendelea na ujenzi wa nyumba yangu ya kisasa kutokana na fedha nazopata kwenye kilimo baada ya kuuza mazao,”anasema mama huyo ambaye umemejua umekuwa fursa kwake.
Ashura Hemed, mkazi wa kijiji cha Namtumbwa wilaya ya Liwale Mkoa wa Lindi akionyesha baadhi ya mikate wanayooka kwa kutumia umemejua baada ya kijiji hicho kupatiwa mradi huo na kampuni ya PowerCorner Tanzania. Picha| Haika Kimaro.
Kwa mujibu wa Wakala wa Nishati vijijini (REA), idada ya wateja waliounganishwa na umeme katika Mkoa wa Lindi hadi kufikia Februari 2022 ni wateja 5,306 walioungwa kwa njia moja na walioungwa njia tatu ni 131.
Fundi wa samani, Hassan Ally anasema kwa sasa ana mudu gharama za maisha kutokana na kipato anachokipata kutokana na kazi hiyo ambacho kinamuwezesha kuhudumia familia yake ya watu wanne.
“Sasa hivi mtu yeyote anaweza kutengeneza kitanda au kabati hapa kijijini haina haja jwenda tena mjini kama zamani na hii imekuwa na faida kwetu sote kwa sababu kama fundi napata fedha na mteja anapunguza gharama za kwenda mjini lakini pia usafirishaji nao haukuwa wa usalama sana,” anasema Hassan na kuongeza;
“Sasa naweza kutumia umemejua kuranda au kuchana mbao nayotoka kutumia ikanyooka na situmii nguvu nyingi kama ile kufanya kienyeji, pia naweza kuweka urembo kwenye bidhaa zangu kama kuchora maua kwenye vitanda au kabati ambapo mteja akileta kazi inachukua wiki moja au chini yake kukamilika kutegemeana na anataka nini,”anasema
Nassoro Mpitage, shughuli yake kwa miaka yote ilikuwa kilimo lakini sasa anaweza kujiongezea kipato kwa kuuza vinywaji baridi kijiji hapo tofauti na awali havikuwahi kupatikana.
Anasema baada ya kuunganishiwa umemejua aliona fursa kwenye uuzaji wa vinywaji hasa msimu wa kiangazi na hivyo kununu jokofu ambalo hulitumia kupozea vinywaji vya aina mbalimbali na maji.
“Kabla ya umemejua kijijini kwetu kulikuwa hamna vinywaji baridi na mimi nilianzisha biashara hii baada ya kuvutiwa na uwepo wa umeme, sasa naweza kuuza hadi chupa 15 za vinywaji baridi aina tofauti tofauti pamoja na bidhaa nyingezo ambazo nauza hata usiku kwa sababu ya mwanga,” anasema Nassoro.
Mbali na umemejua huo kutumika katika shughuli za biashara baadhi ya familia wanautumia kwa matumizi ya nyumbani kama kupata mwanga hasa wakati wanafunzi wanaposoma, kujilinda na wizi na hatari ya kuunguza nyumba hasa inapotumika mishumaa au vibatari pasipokuwa na uangalizi wa kutosha.
Darina Abdallah anasema “sasa hivi watoto wanasoma vizuri hawatumii tena vibatari kama iliyokuwa siku za nyuma na wakati mwingine shuleni tulikuwa tunaagizwa mafuta ya taa kwa ajili ya watoto kusomea kwenye vibatari ambavyo kwa namna moja au nyingine vilichangia kuwaumiza macho lakini pia tunafahamu kinachoendelea Tanzania na nje kwa kuangalia televisheni.”
Soma zaidi:
- Umemejua kimbilio kwa waliopitwa na gridi ya Taifa
- Umemejua unavyoboresha, afya, elimu Bagamoyo
- Umemejua unavyoweza kuchangia upatikanaji wa maji safi vijijini
Changamoto zinazowakabili
Licha ya wanakijiji hao kufaidika na nishati hiyo wakati wakisubiri gridi ya Taifa, baadhi ya watumiaji wa umeme huo wameanza kudhibitiwa katika matumizi yao tofauti na awali walipounganishiwa huduma.
“Umeme wa viwanda vikubwa wanatuwashia saa 2 asubuhi na kuupa nguvu hadi saa 11 jioni baada ya hapo unapunguzwa nguvu hivyo akiwepo mteja wa zaidi ya muda huo kunakuwa hamna biashara kwa sababu wateja wengine wanatoka vijiji vya mbali, mfano akifika atahitaji kuchomelea na sisi kama wazalishaji hatujui ratiba ya mteja hivyo unatakiwa kuwa na nguvu saa 24,” anasema Ashura
Awali, kiundi cha Ashura kilikuwa na uwezo wa kuzalisha mikate 60 hadi 90 kwa siku kwa sababu umeme ulikuwa na ratiba ya kuwaka saa zote lakini sasa tunaweza kutengeneza mikate 30 tu kwa siku kwa sababu ikifika jioni wanaupunguza nguvu.
“Kipato tunachopata kwa sasa ni kidogo ambacho kinazunguka kwenye matumizi kama mtaji, lakini hali ya umeme ikiwa nzuri tunaweza kupata kipato zaidi na kutunza kwa ajili ya kutekeleza miradi mingine mikubwa,”anasema Tabia Mohamed, mnufaika mwingine wa umemejua kijijini hapo.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Mbaya kijijini hapo, Suleiman Hakimu anasema umemejua ni mzuri lakini kupanda kwa gharama kunaanza kuwaumiza.
“Changamoto ni gharama imeanza kuwa juu kuendesha biashara kwa sababu mtu anapohitaji umeme wa matumizi makubwa kama kuchomea anajitaji kulipa kiasi kikubwa zaidi,
“Lakini kwa matumizi ya kawaida nyumbani mtu ili aweze kuangalia video inabidi alipie Sh2,000 kifurushi cha wiki lakini pia kipo cha chini yake kulingana na matumizi,” anasema Hakimu.
Wakazi wa kijiji cha Lukumbule wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakiendelea na shughuli za uchomeleaji baada ya kupata nishati jadidifu ya umemejua. Picha|Haika Kimaro.
Nini suluhu ya changamoto hizo?
Mratibu wa Masoko na Mauzo wa kampuni ya PowerCorner kanda ya kusini, Jackson Lipanga anasema katika ukanda huo wana miradi ya umemejua katika vijiji mbalimbali katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambapo wanufaika wake wamekuwa wakiutumia kuendesha shughuli za kuwapatia kipato mbali na mwanga.
Anasema umeme huo huunganishwa kama ulivyo wa Tanesco na kwamba mteja ana uwezo wa kununua umeme kulingana na mahitaji yake kutokana na makundi yaliyopo na anaweza kubadili kundi wakati wowote kwa kulipia kifurushi anachotaka.
Anaeleza awali wateja wote walikuwa wanaunganishiwa umeme kwa kulipia ada mbalimbali na kununua umeme kwa wastani wa Sh1,200 hadi Sh3,100 kwa uniti moja kulingana na daraja alilopo na hali iliendelea kuwa hivyo mpaka Julai 2020 na ndiyo sababu sasa wanufaika wanaona kuna mabadiliko.
“Tulipata mwongozo kutoka serikalini kupitia Waziri wa Nishati wakati huo, Dk Medard Kalemani baada ya hapo kuna mabadiliko yalitokea ikiwa ni kuuza umeme Sh100 kwa uniti, kwa hiyo sisi katika vijiji wateja wetu wote karibu asilimia 70 wananunua umeme uniti moja kwa Sh 100,’ anasema Lipanga.
Anasema wateja wao wenye viwanda vidogo vidogo kama kuchomelewa, mashine za kuoka mikate, karakana za mafundi wa samani na wengine pia wananunua umeme kulingana na madaraja yao ambapo waliendelea na utaratibu huo hadi kufikia Julai mwaka huu ambapo utaratibu umebadilika.
Anasema sasa wateja wote wapo kwenye kundi la kununua uniti moja kwa Sh100 na baada ya hapo kuna makundi kadhaa kama jamii wanaonunua umeme Sh100 kwa uniti ambao watabaki na umeme wenye nguvu ya wati 40 kwa mchana na ifikapo jioni wanabaki na wati 15.
Kundi la pili wateja wa nyumbani ambao wana tozo kwa ajili ya maboresho wanalipia Sh6,500 kwa mwezi na watanunua umeme uniti moja Sh 350.
“Hivi vyote ni vifurushi vya hiari mteja asipolipia kifurushi chochote atarudi kwenye hali ya kawaida kununua uniti moja kwa Sh 100, kwa hiyo katika vijiji vyetu vyote tunaendelea kutekeleza maagizo ya kulipia uniti moja Sh100 isipokuwa mwenye mahitaji ya ziada atalipia gharama za ziada,” anasema Lipanga.
Latest
