Nani anamjali mwanamke wa kijijini na mapambano ya haki sawa?

December 23, 2021 2:26 pm · Jane
Share
Tweet
Copy Link
  • Wengi wao hawajuia kama kuna siku ya wanawake duniani.
  • Ukosefu wa huduma muhimu za kijamii ndiyo vitu vilivyo akilini mwao.
  • Nani anawasemea matatizo yao?

“Kinachotuponza sisi wanawake ni kuona kwamba hatuna haki na kwamba sisi ni watu wa kunyeyekea katika jamii.” 

Hayo ni sehemu ya maneno niliyoyasikisia kutoka kwa mwanamke mmoja miezi miwili iliyopita wakati mimi na wenzangu wa Twaweza tulipotembelea baadhi ya vijiji wilayani Maswa mkoani Simiyu.

Maneno haya yamenifanya nikumbuke kwamba ni miezi michache iliyopita tulikuwa tukisheherekea siku ya wanawake duniani. Siku hiyo ni maalumu kwa kuangalia ni wapi tumetoka na wapi tumefikia katika usawa wa kijinsia. Yaani usawa kati ya wanawake na wanaume. 

Hata hivyo, simulizi hii ya usawa wa kijinsia ni tofauti sana kwa wanawake wa vijijini. Wanawake hawa wengi hawajui chochote juu ya siku ya wanawake au mwezi wa historia ya wanawake au ‘ufeminist’ yaani uanaharakati wa haki za wanawake. Watajuaje kama hakuna anayewafikia kuwaambia kuwa kuna kitu kinaitwa siku ya wanawake na kinaamanisha nini? 

Inawezekana ufeministi na usawa ni kitu cha mwisho ambacho wanawake hawa wa kijijini wanaweza kukifikiria. Changamoto zinazowakabili wanawake hawa ndiyo vitu vilivyo akilini mwao. Changamoto kama ya ubovu wa barabara na umbali wa kupata huduma za afya katika maeneo yao. 

“Kitu ambacho mimi ningependa kuwa nacho ni barabara nzuri ambayo inaweza kunifikisha zahanati pindi nataka kujifungua. Nilipokuwa nakaribia kujifungua niliondoka na kwenda Lalago mapema ili nijifungue salama”, alituambia mama mwenye mtoto mmoja ambaye kwa kumuangalia alikuwa mdogo kwangu kiumri.

Nilishuhudia adha ya barabara ambayo wanawake hawa wanapitia katika maisha yao ya kila siku hasa wakati wa mvua. 

Ili kuweza kufikia kijiji hiki, tulitumia trekta la mikono maarufu kama Power Tiller kwa muda wa zaidi ya saa moja kutoka mahali ambapo usafiri wa gari unaweza kufika. Sehemu kubwa ya barabara imejaa maji na kuna wakati tukilazimika kushuka na kutembea kwa sababu haikuwa rahisi kuwa ndani ya usafiri wetu wa power tiller. 

Trekta ambalo tulitumia kufika katika kijiji cha kimoja cha Wilaya ya Maswa ambacho kinakabiliwa na tatizo la ubovu wa barabara. Picha | Jane Shussa.

Katika safari hiyo, kuna wakati tulilazimika kushuka na kutembea kwenye maji maeneo ambayo trekta lisingeweza kupita likiwa na watu. Madereva wetu, vijana watatu ambao walikuwa na hadithi nyingi sana, walishuka na kusukuma trekta katika maeneo hayo korofi na kuna maeneo walilazimika kuchimba udongo ili tuweze kupita. 

Wanawake hawa wanalazimika kutembea umbali huo mrefu ili kufikia huduma muhimu kama hospitali. Kupata maji safi na salama katika maeneo ya jirani na ndani ya muda kwao ni kama simulizi ya filamu za magharibi. Ni kama anasa tu. Wanahitaji kutembea kwa wastani wa dakika thelathini wakati mwingine zaidi ili kupata maji safi na salama. 

Tulitaka kufahamu kama wanajisikia huru kupaza sauti zao katika mikutano ambayo wengi wao walisema hawahudhulii kwa sababu waume zao ndiyo wahudhuliaji wa mikutano. 

“Uhuru wa kufanya hivyo upo. Lakini mazingira yetu hayaturuhusu. Mtu una jambo la kuongea lakini huwezi kuongea mbele za watu na Kiswahili pia ni tatizo. Katika mikutano hii tunatakiwa kuongea Kiswahili. Lakini kikubwa ni uoga wa wanawake kuongea mbele za watu,” alituambia mmoja wa wanawake hao.

Basi bwana, kesho yake tukatembelea kijiji kingine na akilini mwangu nilikuwa nikitaraji kukuta hali ya kuridhisha zaidi ya kijiji kilichopita. Kwa bahati mbaya hata kijiji ambacho awali nilitarajia kuwa kingekuwa na mabadiliko, hali ni hiyo hiyo. Hakuna nafuu juu ya fikra za kina mama na masuala hayo.

Nani yuko tayari kuwatua mzigo wa matatizo wanawake wa vijijini? Picha| Gift Mijoe.

Kijiji hiki kilinifanya niwasikitikie wanawake wanaoishi hapa. Manyanyaso yao si tu kwenye ukosefu wa huduma muhimu kama hospitali au barabara bali mpaka kupigwa na kudhalilishwa hadharani.

“Mimi hili jambo linanisikitisha sana. Naombeni samahani kama nitawakwaza ila lazima niseme,” alianza kutueleza mmoja ya wanawake tuliokuwa tukizungumza naye ambaye si mzaliwa wa kijiji hicho. Amehamia miezi kadhaa iliyopita kutoka mkoa mwingine na hakutaka kutajwa jina lake kwa kuhofia angetazamwa tofauti kijijini kwao. 

Aliendelea, “mwanamke hapa ukifanya kosa katika familia yako unaletwa hapa hadharani na sungusungu na unachapwa mbele za watu. Katika kijiji hiki wanawake tuko chini sana. Hatuwezi kutoa dukuduku zetu kwa uongozi.  Kuna sheria gani ya mtu kupigwa hadharani baada ya kufumaniwa au kutenda kosa lolote? Tunateseka sana,” alisema. 

Alidakia mwanamke mwingine, “dada sisi hapa wanawake hatuna sauti. Hata unapofanya kosa ukijaribu kujitetea hakuna anayekusikiliza tunaishia kukandamizwa. Hapa hakuna sheria zinazofuatwa. Ukifikisha matatizo yako katika uongozi unachukiwa na kila mtu hapa kijijini.”

Ni nani anayewasemea wanawake hawa? Ni nani anapaza sauti juu ya wanawake hawa? Au ufeministi wetu unaishia katika mitandao na mambo ambayo yanatugusa sisi wa “mjini” zaidi? 

Mbali na usawa na ufeministi, je wanawake hawa hawastahili kupata haki zao na mahitaji yao muhimu kama binadamu?

Kusimulia stori hii hakunitoi katika jukumu la kuhakikisha wanawake hawa wanapata haki zao za msingi kama binadamu. Lengo la kusimulia stori hii ni kuanzisha mjadala ambao kwa namna moja au nyingine umesahaulika na hivyo unakosa kupata suluhisho.

Makala haya ni maoni binafsi ya mwandishi na siyo msimamo wa tovuti ya habari ya Nukta na shirika la Twaweza analofanya nalo kazi.

Enable Notifications OK No thanks