Wanakijiji wajitosa kumwokoa mtendaji mwenye ‘ofisi’ chini ya mti
- Watafuta viwanja, wapeleka mawe na mchanga.
- Mtendaji wao wa kijiji atoa huduma chini ya mti kwa miaka miwili.
- Wanakijiji wahofia mambo yao kuvuja kijijini kwa kukosa faragha.
Maswa, Simiyu. Wakati anahamishiwa katika Kijiji cha Sulu wilayani Maswa alijua mambo yangekuwa rahisi tu.
Alifikiri angekuta ofisi nzuri na yenye vifaa vyote muhimu ambavyo vingemsaidia katika utoaji wa huduma za Serikali kama alipokuwa akifanya kazi awali.
La hasha, mambo si kama alivyotarajia. Kwa sasa Kulwa Daudi, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Sulu ana mwaka wa pili akitoa huduma chini ya mti mbele ya nyumba aliyopanga kama “ofisi” yake kuu.
“Sina ofisi ya kufanyia kazi, nafanya kazi katika mazingira magumu na makazi vilevile sina ndani ya kijiji hiki,” anasema Daudi ambaye hutoa huduma kwa watu wasiopungua 10 kwa siku.
“Nafanya kazi nje ya nyumba yangu, chini ya mti ila kipindi cha masika na kiangazi huwa nalazimika kufanyia kazi kwenye maghala ya pamba,” anasema Daudi huku akitikisa kichwa kwa huzuni.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Sulu, Kulwa Daudi akiwa ofisini kwake mara baada ya mahojiano Februari 24, 2022. Kutokana na ukosefu wa ofisi, kiongozi huyu hutoa huduma chini ya mti. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta.
Huduma kama kawaida chini ya mti
Chini ya mti huu, wakazi wa kijiji hiki kilichopo kata ya Mbaragane wanasema humfuata na kumweleza shida zao na hata wakati mwingine huzungumza naye ndani ya nyumba yake au kwenye eneo la Zahanati chini ya mti.
Kwa kuwa ana nyaraka muhimu za Serikali, Daudi anasema hulazimika kuzitunza ndani ya nyumba aliyopanga na hulazimika wakati mwingine kutoa fedha zake mfukoni kupiga chapa baadhi ya nyaraka ili kuwahudumia wakazi wasio na uwezo.
Kijiji hiki hakina huduma za haraka za kuchapisha au kidurufu nyaraka hivyo humlazimu kusafiri umbali wa kilomita takriban saba hadi Kijiji cha Mbalagane kupata huduma hizo kwa kuwa ‘ofisi’ yake haina printa wala mashine ya kudurufu nyaraka.
Kuchapa nyaraka hadi kilomita nane
“Gharama za mafuta tu ya pikipiki kwenda kuchapisha nyaraka huwa ni Sh35,000 kwa mwezi na uchapishaji huwa ni kama Sh10,000 hivi,” anasema Daudi na kubainisha kuwa fedha hizo hutoka mfukoni kwake.
Baadhi ya wakazi wanasema ukosefu wa ofisi unapunguza ufanisi katika upatikanaji wa huduma za Serikali jambo linaloathiri utawala bora.
Raheli Joseph, Mkazi wa Kijiji cha Sulu ni mmoja ya watu wanaoumia kuona mtendaji wao hana ofisi jambo ambalo anasema kuna wakati linapunguza faragha kati ya wakazi hao wenye shida ya huduma na kiongozi huyo.
“Kuna wakati una unamfuata pale kwake sasa wakati unatoa maelezo lazima familia yote itafahamu mambo yako na mtu mwingine anaweza kupiga hodi wakati mambo unayozungumza muda mwingine yanakuwa ya siri,” anasema Raheli huku akibainisha ni mara nyingi watu wamemkuta akifuata huduma za kiserikali kwa mtendaji huyo.
Hofu ya siri kuvuja
Raheli anahofu kuwa baadhi ya taarifa hata kama mtendaji atatoka nje kwenda kwenye mti kusikiliza shida za mwanakikiji bado kuna watu wanaweza kusikia na hata kuhatarisha kuvujisha mambo yao kijijini.
Mbali na suala la faragha, baadhi wanakijiji wanasema ukosefu wa ofisi unapunguza ufanisi katika utoaji wa huduma za kijamii kutoka katika ofisi hiyo.
Joseph Melchiarde, mkazi wa kijiji hicho anasema kuna wakati wanaenda kutafuta huduma lakini hukuta mtendaji ametoka kidogo na kwa kuwa hakuna ofisi inakuwa ni vigumu kumsubiria au kupata taarifa kutoka kwa wasaidizi.
“Kuna wakati unakuta ameenda kutoa huduma nyingine huko…sasa inakubidi umtafute mpaka umpate,” anasema Melchiarde na kuongeza kuwa hata msaidizi wake naye kwa kuwa hakuna ofisi huwa naye ni vigumu kumpata.
Hata hivyo, Daudi anasema wanajitahidi kutunza siri za wateja na inapotokea kesi yenye faragha viongozi wa kijiji hicho hutafuta eneo tulivu na lenye faragha kuhakikisha wanamhudumia ipasavyo.
Tangazo:
Jitihada za kijinusuru zaanza
Serikali ya kijiji kwa kushirikiana na waraghbishi wa eneo hili walilazimika kushawishi wakazi wa eneo hili kushiriki kikamilifu katika kutatua tatizo hilo.
“Nilihamishwa tu, nikafika mazingira ndiyo haya, ikabidi nipambane kwa kadri ya uwezo wangu kwa kuwashirikisha wanakijiji wa Sulu ili tuweze kuanzisha ujenzi wa ofisi ya kijiji,” anasema Daudi akieleza jitihada wanazofanya ili kuhakikisha wanaofisi.
Ili kutatua tatizo hilo, wakazi wa kijiji hicho baada ya kuhamasishana hawakuona sababu ya kuisubiria Serikali ambayo inakabiliwa na changamoto lukuki za kirasilimali kutimiza huduma zote za kijamii kwa wananchi.
Maduhu Jilingisila, Mraghbishi katika Kijiji cha Sulu anasema walianza kuhamasishana kupitia waraghbishi na viongozi wa Serikali ya kijiji kutafuta kiwanja na vifaa vya awali vya ujenzi.
“Mwamko ni mkubwa tangu tulivyoanza uraghbishi Septemba 2021 kama mlivyoona pale kuna mawe na mchanga…vyote hivyo ni matokeo ya ari ambayo haikuwepo kipindi kile na kwa kuwa tunaenda msimu wa kuvuna choroko naamini watu watachangia na tatizo litaisha,” anasema Jilingisila.
Uraghbishi ni mbinu ya kuwahamasisha wananchi kuibua, kuchambua na kubaini vipaumbele vyao vya kimaendeleo na kutatua matatizo yao katika eneo husika.
Hadi sasa Jilingisila anasema wameshapata viwanja viwili vinavyokana ambavyo wataamua kimoja wapo wajenge ofisi.
Wakazi wa Kijiji cha Sulu wilayani Maswa wameanza jitihada za kuanza kujenga ofisi ya Mtendaji wa Kijiji ili kuepusha kadhia zinazowakumba. Tayari wameshasomba mchanga na mawe kwa ajili ya ujenzi. Picha|Nuzulack Dausen\Nukta.
Wananchi wajitosa kutatua tatizo
Baadhi wakazi wa kijiji hiki wanaeleza kuwa wanaunga mkono juhudi hizo na kueleza kuwa pamoja na ukata na majukumu walio nayo hawana budi kujitoa kwa kuwa ukosefu wa ofisi unamuathiri kila mtu.
“Kwa sasa tunataka kumshika mkono mtendaji, mwezi wa 11 mwaka jana (Novemba, 2021) tulianza kusomba mawe na mchanga ila baadaye mvua ilitutatiza na tukasimama kidogo, “anasema Raheli.
Hadi sasa, Daudi anasema wameshasomba tripu 10 za mchanga kwa ajili ya kufyatua tofali na wamesogeza mawe mikokoteni isiyopungua mitano yatakayotumika kujenga msingi.
Daudi anasema wameshindwa kuanza ujenzi haraka kwa sababu walikuwa wanakamilisha ujenzi wa shule ya sekondari uliofanya nguvu zote za wanakijiji kuhamishiwa kule kwa kuwa ilikuwa ni muhimu kuliko ofisi yake.
Katika moja ya viwanja wanapopanga kujenga ofisi hizo, Nukta Habari ilishuhudia malundo ya mchanga na mawe katika eneo lilopita mita chache kutoka barabarani kuelekea Sulu Centre.
Soma zaidi:
- Mfugaji anayeongoza safari ya ufugaji wa kisasa Simiyu
- Tutatoboa: Wakazi wa Geita wanavyopambana kuung’oa ujinga
Hati hati kukamilika kwa wakati
Hata hivyo, bado kuna hati hati iwapo ofisi hiyo itakamilika ndani ya miaka mmmoja licha ya Daudi kueleza kuwa wanaamini ndani ya mwaka wa fedha 2022/23 itakuwa imekamilika huku wakitegemea kuongezewa nguvu na Serikali pamoja na wahisani kutoka mashirika binafsi na asasi za kiraia.
“Kama watu watajitokeza kupaua na kutuwekea milango tutashukuru,” anasema Daudi.
Katika kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi, Serikali inakiri kuwa baadhi ya maeneo kuna changamoto ya miundombinu kama uhaba wa madarasa na ofisi za viongozi wa vijiji ila kwa sasa inaweka kwenye bajeti miradi yote iliyoanzishwa na wananchi ili kuimalizia.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Maswa Vivian Christian anasema miradi yote ikiwemo ya madarasa ambayo wanachi wameijenga na kufikia kwenye lenta itamaliziwa kupitia bajeti ya halmashauri hiyo.
Hata hivyo, swali ni je, ofisi hiyo itaishi lini kuwaeupusha wanakijiji hao na kadhia za kuhudumiwa kwenye mti?
