Wanafunzi wasioona wanavyosaka elimu ya sayansi kama dhahabu Tanzania

March 3, 2020 12:57 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wakati baadhi yao wakiwa na ndoto za kusoma masomo ya sayansi, hali zao zinawakwamisha.
  • Wadau waelimu washauri walimu wajengewe uwezo na matumizi ya teknolojia katika ufundishaji.
  • Serikali yasema itaendelea kutoa elimu jumuishi inayozingatia mahitaji ya kila mwanafunzi.

Dar es Salaam. “Nina ndoto ya kuwa mwanasheria kwasababu ni masomo ambayo ninayamudu. Ningependa kuwa mwanasayansi, daktari na hata mhandisi lakini kutokana na hali yangu siwezi,” amesema Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Lugoba iliyopo Chalinze mkoa wa Pwani, Joyce Salum.

Joyce ambaye  ana ulemavu wa kutokuona ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa ndoto yake ya kuwa daktari huenda ikazimika kwa sababu miundombinu iliyopo shuleni siyo rafiki kwa yeye kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi.

 “Kipindi cha mitihani huwa nasikia wenzangu wakiambizana juu ya “practical” (mitihani ya vitendo) ambayo kutokana na hali yangu, siwezi kuifanya.”

Joyce (19) ni miongoni mwa wanafunzi wengi nchini wenye mahitaji maalumu ambao ndoto zao zinaishia hewani na wakati mwingine husomea masomo ambayo hali yao inawaruhusu.

Kama alivyo kwa Joyce,  mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Lugoba, Athuman Hassan pia amesema malengo yake yamegubikwa na giza kutokana na ulemavu wa macho alionao.

Hassan ambaye akiwa mtoto alisikia ndoto za watoto wenzake wakitaka kuwa marubani na madaktari hakuweza hata kujua wanamaanisha nini hadi pale alipoanza kujifunza juu ya kazi za watu.

“Ilikuwa vigumu hata kusema nataka kuwa nani. Ningewezaje na sijui vitu hivyo kwasababu nimezaliwa na hali hii?

“Lakini sasa nimeona niwe mwanasheria kwasababu ni kazi ambayo ninaweza kuimudu. Masomo ninaweza kuyaelewa kwa sababu hayahitaji ulazima wa kuona,” amesema Hassan.

Takwimu huru za Tanzania za mwaka 2012 (www.opendata.go.tz), zinaeleza kuwa Tanzania Bars ina wanafunzi wasiosikia na kuona  760 huku kati yao, asilimia 18.9 wakitoka mkoa wa Mwanza ukifuatiwa na Ruvuma yenye wanafunzi 92.

Mwalimu wa shule ya Lugoba, Fabian Simai ambaye anamfundisha Joyce na Hassan amesema kutokana na hali yao, waalimu wanafanya kazi kubwa ya kuwahimiza watoto hao kusoma masomo ambayo yanaendana na hali zao wakati wakisubiri Serikali iwaboreshee miundombinu ya kujifunzia.


“Kipindi cha mitihani huwa nasikia wenzangu wakiambizana juu ya “practical” (mitihani ya vitendo) ambayo kutokana na hali yangu, siwezi kuifanya.” Picha| Rodgers George.

Tunafanye nini kuwasaidia wafikie ndoto zao na zaidi kuendeleza vipaji vyao?

Mwandishi mashuhuri wa vitabu na mdau wa elimu,  Richard Mabala amesema uboreshaji wa sera ya elimu jumuishi ni muhimu lakini ipo haja ya kuwajengea uwezo walimu ili waweze kuwafundisha kwa urahisi wanafunzi wenye ulemavu.

Mabala ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi ya HakiElimu amesema siyo rahisi, inahitaji fedha, jitihada na dhamira thabiti hasa kuboresha miundombinu ya wanafunzi hao mashuleni.

“Inabidi waalimu waandaliwe, wajue cha kufanya ili hawa wanafunzi waweze kuendeleza vipaji vyao na kuwa wanasayansi kama wanavyohitaji,” amesema Mabala.

Kwa sasa kuna chuo kimoja cha Patange ambacho kipo Tengeru mkoani Arusha, kinachowawezesha walimu kufundisha wanafunzi wenye ulemavu.

Kati ya teknolojia zinazotumika kwenye kufundisha watoto wenye ulemvu a macho ni pamoja na maandishi ya nukta nundu. Picha| Rodgers George.

Hata hivyo, Mabala amesema ulemavu wa akili na jambo ambalo linahitaji kuangaliwa kwani ni suala ambalo limesahaulika.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Shule Direct, Iku Lazaro amesema ipo haja ya kuanza kuangazia namna teknolojia inavyoweza kusaidia katika ufundishaji wa wanafunzi wasioona.

“Ninaamini teknolojia inaweza kutusaidia. Wapo wanafunzi ambao wana changamoto ya kuona na kusikia, wao inabidi jitihada zaidi zifanyike lakini kwa ambao wana tatizo moja, teknolojia ipo na tayari imeanza kutumika,” amesema Lazaro.


Zinazohusiana


Mikakati ya Serikali

Hivi karibuni, Serikali imezindua vitabu vya nukta nundu kwaajili ya shule za sekondari na msingi ambavyo vinahusisha masomo ya sayansi, ikiwa ni hatua ya  kuwasaidia wanafunzi wasioona kubobea katika masomo ya sayansi.

Katika uzinduzi wa vitabu vya nukta nundu uliofanyika mwishoni mwa Februari, Kaimu Kamishna wa Elimu, Yesse Kanyuma aliwataka walimu kufanya kazi ya kuwaelekeza wanafunzi hao namna ya kutumia vifaa vya kusomea vikiwemo vitabu vya nukta nundu.

Amewataka kuendelea kuwahimiza wanafunzi hao kuwa na utamaduni wa kujisomea na kujiendelea kielimu kwa kutumia miundombinu rafiki ambayo Serikali inaboresha katika shule zao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW