Walioomba ajira Jeshi la Polisi Tanzania waitwa kwenye usaili
- Zoezi la usaili litaanza rasmi tarehe 28 Aprili hadi 11 Mei 2025.
- Kila msailiwa anatakiwa kufika na vyeti halisi vya taaluma, cheti cha kuzaliwa, pamoja na kitambulisho Taifa au namba ya NIDA.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limetangaza kuanza kwa zoezi la usaili kwa vijana waliotuma maombi ya kujiunga na Jeshi hilo kupitia mfumo wake wa maombi ya ajira (Tanzania Police Force Recruitment Portal) .
Usaili huo utafanyika kuanzia tarehe 28 Aprili hadi 11 Mei 2025 katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Camillus Wambura, wasailiwa wenye elimu ya Shahada, Stashahada na Astashahada watafanyiwa usaili jijini Dar es Salaam katika uwanja wa gwaride uliopo kambi ya polisi, barabara ya Kilwa nyuma ya kituo cha Polisi Kilwa Road.

Kwa upande wa wasailiwa wenye elimu ya kidato cha nne na sita, usaili utafanyika katika mikoa waliyoweka kama chaguo wakati wa kutuma maombi, chini ya usimamizi wa Makamanda wa Polisi wa mikoa husika.
Aidha, kwa wasailiwa wa Zanzibar wa elimu zote kuanzia kidato cha nne hadi Shahada usaili utafanyika kwenye maeneo yaliyopangwa kulingana na mikoa.
Kwa walio Unguja, usaili utafanyika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar (Ziwani), wakati walio Pemba watafanyiwa usaili katika Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Chakechake.
Jeshi la Polisi limeelekeza kuwa kila msailiwa anatakiwa kufika na vyeti halisi vya taaluma, cheti cha kuzaliwa, kitambulisho cha Taifa cha NIDA au namba ya NIDA, pamoja na mavazi ya michezo.
Hata hivyo taarifa hiyo imeonya kuwa wasailiwa watakaofika baada ya tarehe 28 Aprili 2025 hawatapokelewa.
Latest



