Spika Tulia awapeleka Gambo, Waziri Tamisemi Kamati ya Maadili

April 23, 2025 3:38 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya Gambo kutoridhishwa na ufafanuzi uliotolewa na Waziri Mchengerwa.
  • Spika asisitiza kamati kuleta ripoti na taarifa kuhusu jambo hilo kwa haraka.

Dar es salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ameitaka Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kusikiliza shauri la tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za mradi wa jengo la Halmashauri Arusha na kuwasilisha ukweli wa jambo hilo ndani ya wiki moja.

Agizo la Spika Tulia limekuja baada ya Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo aliyeibua tuhuma hizo kutoridhishwa na ufafanuzi uliotolewa na Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohamed Mchengerwa.

“Mheshimiwa Gambo anasema Waziri amedanganya kwenye taarifa yake. Kwa hivyo nalipeleka jambo hili kwenye kamati yetu ya kudumu ya maadili. Watakwenda kusikilizwa, kamati ituambie nani muongo hapa ndani na hatua zichukuliwe.” amesema Spika Ackson 

Kuibuliwa kwa tuhuma

Tuhuma za matumizi mabaya ya fedha ziliibuliwa na Gambo Aprili 16, 2025, wakati wa mjadala wa bajeti ya TAMISEMI kwa mwaka 2025/26 akidai kuwa baadhi ya vipimo vilivyowekwa kwenye makubaliano ya ujenzi wa jengo la utawala Halmashauri ya Arusha vilipotoshwa na kusababisha ongezeko la takribani Shilingi 2.8 bilioni kutoka kwenye gharama halisi.

“Gharama halisi zilitakiwa kuwa bilioni 3.4, lakini wameingia mkataba wa bilioni 6.2… kuna ziada ya zaidi ya bilioni 2.8. Kuna ‘teamwork’ ya baadhi ya watumishi wa umma wanaoshirikiana kulimaliza Jiji la Arusha,” alisema Gambo.

Mrisho Gambo ameonyesha kutoridhishwa na ufafanuzi uliotolewa na Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mohamed Mchengerwa. Photo by Merciful Munuo

Kutokana na uzito wa tuhuma hizo, Spika Tulia alimuelekeza Waziri Mchengerwa kuwasilisha taarifa fupi kuhusu mradi huo mara baada ya mjadala wa bajeti kumalizika.

Majibu ya Waziri Mchengerwa

Katika kikao cha Aprili 22 Wakati akihitimisha bajeti ya Wizara yake, Waziri Mchengerwa alibanisha kuwa hakuna fedha za umma zilizopotea na kuongeza kuwa tuhuma zilizotolewa ni cheche za siasa.

Hata hivyo, Spika Tulia alimtaka Mchengerwa kuwasilisha majibu ya kina ya uchunguzi wa tuhuma hizo leo Aprili 23, mara baada ya kipindi cha maswali na majibu. 

Akitoa mchanganuo kuhusu mradi huo Mchengerwa ameeleza kuwa ujenzi wa jengo hilo ulianza Aprili 2024 baada ya kusuasua kwa muda mrefu na kwa sasa umefikia ghorofa ya sita na kuongeza kuwa mkandarasi tayari ameshalipwa kadiri ya utaratibu unavyotaka

 “Mpaka sasa mkandarasi amelipwa jumla ya Shilingi 2.2 bilioni. Kilicholipwa ni kidogo kulinganisha na maendeleo ya jengo. Hakuna fedha ya Serikali iliyoibiwa.” amesema Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa alibanisha kuwa hakuna fedha za umma zilizopotea na kuongeza kuwa tuhuma zilizotolewa ni cheche za siasa. Picha | Mzalendo.

Hata hivyo, Mchengerwa amebainisha kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na wizara yake umebaini kuwepo kwa hitilafu za kiufundi kwenye mfumo wa ununuzi wa umma (NEST), ambapo vipimo vilichanganywa kimakosa, lakini mkandarasi tayari alishaarifiwa na tayari alikwisha kujibu.

Mara baada ya ufafanuzi wa Mchengerwa, Gambo hakuonekana kuridhishwa na baadhi ya majibu ndipo Spika Tulia akasema kwa kuwa Bunge linaendeshwa na kamati suala hilo analipeleka katika kamati husika.

Spika Tulia amesisitiza kuwa Bunge haliwezi kuvumilia tuhuma nzito zisizo na uthibitisho hivyo ili kutoleta taharuki kwa kwa wananchi Kamati ya Maadili itasikiliza pande zote na kutoa taarifa wiki ijayo kabla ya hatua kuchukuliwa. 

“Ikiwa litakuwepo jambo la ziada, mimi niko tayari kabisa, kwa sababu Bunge hili haliwezi kuvumilia ubadhirifu mahali popote.” amesema Spika Tulia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks