Bajeti ya Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora yapaa kwa asilimia 25.54
- Vipaumbele vya 2025/2026 ni pamoja na ajira mpya 41,500 na maboresho ya mifumo ya Tehama.
- Miradi ya maendeleo kupata Sh183 bilioni.
Dar es Salaam. Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imewasilisha bungeni ombi la kuidhinishiwa bajeti ya jumla ya Sh1.35 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni ongezeko la asilimia 25.54 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo bungeni jijini Dodoma leo Aprili 23,2025, Waziri wa Nchi George Simbachawene amesema bajeti hiyo inalenga kuimarisha utendaji wa taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo na kuandaa mazingira bora kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
“Bajeti ya mafungu yote yaliyo chini ya Ofisi ya Rais imelenga kuweka mazingira yatakayosaidia nchi kuingia katika uchaguzi na kuunda Serikali mpya kwa kuzingatia katiba, sheria na miongozo iliyopo ili kujenga imani kwa wananchi,” amesema Waziri Simbachawene.
Kwa mujibu wa waziri huyo jumla ya Sh1.17 trilioni zimetengwa kwa matumizi ya kawaida huku Sh183.3 bilioni zikiwa ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, licha ya bajeti ya wizara kuongezeka kwa asilimia 25 bajeti ya miradi ya maendeleo imeongezeka kiduchu mwaka na kufikia asilimia 2.81 ya bajeti nzima.
Ofisi ya Rais Utumishi inahusisha mafungu saba ya kibajeti ambayo ni Ofisi ya Rais Ikulu (Fungu 20 na 30), Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma (Fungu 33), Menejimenti ya utumishi na utawala bora (Fungu 32), Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma (Fungu 67), Tume ya utumishi wa umma (Fungu 94), na Idara ya kumbukumbu na nyaraka za taifa (Fungu 04).
Vipaumbele vya Ofisi ya Rais (Utumishi)
Katika mwaka wa fedha ujao, Ofisi ya Rais (Utumishi) imepanga kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushughulikia vibali 41,500 vya ajira mpya, kuhakiki madai ya malimbikizo ya mishahara kwa taasisi 425, kusafisha taarifa za watumishi katika mfumo wa e-Watumishi na kutekeleza miradi ya Tehama inayolenga kuboresha usimamizi wa rasilimali watu.

Shughuli nyingine ni pamoja na kukamilisha marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma (Toleo la nne), kufanya uchambuzi wa miundo ya wizara baada ya uchaguzi, kuboresha mfumo wa e-Utendaji, kuendeleza mifumo ya kushirikisha taarifa (Data sharing gateway), pamoja na kuanzisha scholarship portal kwa ajili ya fursa za ufadhili wa masomo.
Waziri Simbachawene pia ameongeza kuwa kuidhinishwa kwa bajeti hiyo kutaiwezesha Serikali kuimarisha uwajibikaji, kukuza maadili ya viongozi na watumishi wa umma na kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali za Taifa.
“Bajeti hii ni nguzo muhimu katika kuimarisha taasisi za kiutumishi, kuendeleza maadili na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi,” amefafanua Waziri Simbachawene.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Florent Kyombo aliyekuwa akiwasilisha mapendekezo ya kamati hiyo ameeleza kuwa bajeti hiyo imeongezeka kwa asilimia 25.54 kutoka Sh932.8 bilioni za mwaka wa fedha 2024/2025.
“Kamati imebaini ongezeko kubwa la bajeti ya matumizi ya kawaida, hivyo ni maoni yetu kuwa Serikali ipange bajeti inayoendana na mahitaji halisi ya Taifa,” amesisitiza Kyombo.
Hata hivyo, Kyombo amesema ongezeko hilo limechangiwa na kupanda kwa gharama za bidhaa, huduma na idadi ya watumishi wa umma.
Latest



