Walimu sita mbaroni kifo cha mwanafunzi Mara
- Ni baada ya mwanafunzi kufia hospitalini mara baada ya adhabu ya viboko.
- Hii si mara ya kwanza mwanafunzi anafariki baada ya kupatiwa adhabu na walimu wake.
- Jeshi la Polisi lasema uchunguzi unaendelea.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi mkoani Mara linawashikilia walimu sita wa Shule ya Sekondari Makongoro kwa kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule hiyo aliyefariki baada ya kuchapwa viboko.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo leo Agosti 21, 2026 mwanafunzi huyo Petro Chisumo (23). alichapwa viboko na walimu hao na kusababisha kuishiwa nguvu hali iliyomfanya apelekwe Hospitali ya wilaya ya Bunda kwa matibabu.
“Agosti 19,2026 majira ya saa 05:00 asubuhi, wakati mwanafunzi huyo akitekeleza adhabu na wenzake ambao walikua na ufaulu wa chini kwenye mitihani ya kujipima, alichapwa viboko na walimu hao na kusababisha kuishiwa nguvu,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo, akiwa hospitalini hapo siku hiyo hiyo Chisumo alifariki dunia na mwili wake kuhifadhiwa katika hospitali hiyo iliyopo Kaskazini mwa Tanzania.
Hii si mara ya kwanza mwanafunzi anafariki baada ya kupatiwa adhabu na walimu wake nchini. Februari 26, 2025, Mhoja Maduhu, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwasamba mkoani Simiyu, alifariki baada ya kudaiwa kuchapwa viboko 10 na kukanyangwa kichwani na mwalimu wake.
Tukio hilo lilisababisha mjadala mkubwa kuhusu matumizi ya adhabu ya viboko shuleni, huku wazazi na wadau wa haki za binadamu wakitaka uchunguzi ufanyike kuhusu mazingira ya kifo hicho.
Hadi sasa, Kamanda Lutumo amesema, chanzo cha kifo cha Chisumo bado hakijathibitishwa, kutokana na kuendelea kwa uchunguzi wa kitabibu.
Kifo cha kijana huyo mkoani Mara kinaendelea kuibua mjadala juu ya adhabu za viboko na zinazofanana nazo katika uimarishaji wa tabia za watoto nchini.
Mwaka 2024, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Kiteme, mkoani Kagera aliripotiwa kulazwa hospitalini baada ya kudaiwa kujeruhiwa baada ya kukataa kusoma somo la Fizikia.