Wakulima wa korosho wameshaanza kulipwa – Majaliwa

November 17, 2018 11:37 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema korosho zimeshaanza kununuliwa kwa Sh3,300 kwa kilo na wakulima wameshaanza kulipwa.
  • Iwapo bei za mazao zitakuwa nzuri katika soko la dunia, Majliwa amesema Serikali itakuwa ikiwajulisha.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imeanza kununua korosho kwa Sh3,300 kwa kilo na tayari wakulima wameshaanza kulipwa malipo yao.

Kauli hiyo inakuja katika kipindi ambacho wakulima walikuwa wakisubiri uhakiki wa mazao yao waliyohifadhi katika maghala mbalimbali ya vyama vya ushirika hususan katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Mapema wiki hii, Rais John Magufuli alisitisha ununuzi wa zao hilo kwa wanunuzi binafsi na kuagiza kuwa korosho zote zilizosalia zitanunuliwa na Serikali kwa bei ya Sh3,300 kwa kilo, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya bei elekezi iliyokuwa imetolewa awali na kuagiza Jeshi la Wananchi kusimamia zoezi hilo katika usimamizi na usafirishaji. 

Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) awali ilikuwa imependekeza kilo moja ya korosho inanunuliwe si chini ya Sh1,550.

Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), kwa mujibu wa Rais, itatoa fedha hizo za ununuzi wa korosho. 

Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakiwemo maofisa wa juu, ambao wanahusika kulinda maghala na kusafirisha korosho katika mikoa hiyo, walianza kuwasili kuanzia Jumatatu ya wiki hii katika kufanikisha zoezi hilo, Godfrey Zambi Mkuu wa Mkoa wa Lindi amesema.

Katika hotuba yake ya kuahirisha Bunge leo (Novemba 16, 2018) iliyotumwa na ofisi yake, Majaliwa amesema kuyumba kwa bei za baadhi ya mazao ya kimkakati nchini kumesababishwa na kudorora kwa bei ya mazao hayo katika soko la dunia.

Hata hivyo, ameeleza kuwa Serikali itakuwa ikiwajulisha wakulima pale bei zinapokuwa nzuri ili kuwaokoa na hasara ambazo hutokana na kuporomoka na bei za mazao yao


Zinazohusiana:


“Tunampongeza mheshimiwa Rais kwa maamuzi yake ya kuokoa wakulima wa korosho kukosa masoko ya uhakika. Korosho hizo sasa zinanunuliwa kwa bei ya Sh3,300 na tayari malipo yameanza kulipwa,” amesema.

Amesema Rais ametoa maelekezo kwa taasisi zote za umma zinazohusika na masoko ya mazao zikiwemo TanTrade, Bodi ya Mazao Mchanganyiko na Kampuni ya Soko la Bidhaa Tanzania (Tanzania Mercantile Exchange -TMX) kutafuta masoko mapya ya mazao badala ya kutegemea wafanyabiashara pekee ambao baadhi yao si waadilifu.

Kufuatia maelekezo hayo, Majaliwa ameeleza kuwa “sasa sekta binafsi hasa wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia maslahi mapana ya wakulima na Taifa kwa ujumla.”

Kabla ya uamuzi wa Rais Magufuli kuagiza kununuliwa zao hilo, kulikuwa na msuguano kati ya wafanyabiashara na Serikali uliosababisha Majaliwa kutoa siku nne kwa wanunuzi binafsi kuwasilisha kiwango wanachotaka kununua na tarehe za kufanya ununuzi huo.

Hata kabla ya muda wa agizo hilo la Majaliwa kuisha Novemba 12 Saa 10:00 jioni, Rais Magufuli alifuatilia mbali uhusishaji wanunuzi binafsi akieleza kuwa huenda wakababaisha tena kununua shehena hiyo ya korosho inayokaridiwa kuwa tani 220,000 mwaka huu.

“Niwaombe wananchi wenzangu kuendelea kutoa ushirikiano na kutambua kuwa, dhamira ya Serikali ni kuona kila mkulima ananufaika sambamba na kupata tija ya mazao anayozalisha,” amesema Majaliwa.

Enable Notifications OK No thanks