Wagonjwa watano wa Corona wapona Tanzania, wagonjwa wakifika 24
- Wizara ya Afya imesema wagonjwa wengine wawili wamepona leo na kufanya idadi ya waliopona kufikia watu watano mpaka sasa.
- Watu 72 wamewekwa karantini kwa uchunguzi zaidi.
- Serikali yawataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuwa wagonjwa wengine wawili waliokuwa na maambukizi ya ugonjwa virusi vya Corona wamepona na kufanya idadi ya waliopona kufikia watu watano mpaka sasa.
Amesema wagonjwa waliopona ugonjwa huo wa COVID-19 unaosambaa kwa kasi duniani, mmoja anatoka jijini Dar es Salaam na mwingine Arusha.
“Hivyo sasa Mkoa wa Arusha hauna mtu mwenye maambukizi ya COVID19,” amesema Ummy katika ukurasa wake wa Twitter leo (Aprili 7, 2020).
Licha ya Tanzania kuwa na visa 24 vya wagonjwa wa Corona, Waziri huyo amesema leo Aprili hakuna kisa kipya cha mgonjwa wa ugonjwa huo kilichothibitishwa leo.
Kati ya wagonjwa hao waliothibitishwa kuwa na Corona, mmoja kati yao ambaye alifariki dunia wiki iliyopita kikiwa ni kifo cha kwanza Tanzania.
Zinazohusiana
- Jinsi ya kujikinga na virusi vya Corona kwenye mikusanyiko ya watu
- Magufuli aagiza safari za nje zipunguzwe kujikinga na virusi vya Corona
Katika ukurasa huo, Ummy ameeleza kuwa watu 72 wamewekwa karantini kwa ajili kuchunguzwa huku wengine 366 wanaendelea kufuatilia kwa karibu.
Hata hivyo, wananchi wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari ya kunawa mikono mara kwa mara, kutokugusa pua, mdomo au macho, kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Habari njema – wagonjwa 2 wa COVID19 wamepona. Dar es Salaam – 1 na Arusha – 1. Hivyo sasa Mkoa wa Arusha hauna mtu mwenye maambukizi ya COVID19. Tuendelee kuzingatia maelekezo ya Wataalam wa Afya ikiwemo kuepuka mikusanyiko n/misongamano isiyo ya lazima. #JikingeWakingeWengine
pic.twitter.com/6BS2wm4hSe— Ummy Mwalimu, MP (@umwalimu) April 7, 2020
Latest