Uzalishaji wa kahawa kuimarika msimu wa 2019-2020?

Daniel Samson 0117Hrs   Januari 10, 2019 Biashara
  • Kwa miaka mitatu mfululizo tangu mwaka 2016, uzalishaji wa zao hilo umekuwa ukishuka kila mwaka.
  • Mabadiliko ya hali ya hewa, upatikanaji wa soko na magendo vyachangia kusuasua kwa uzalishaji wa zao hilo la biashara.
  • Serikali imejipanga kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 100,000 ifikapo 2021.

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kusisitiza kahawa kuuzwa katika minada ya pamoja, mikakati zaidi inahitajika kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili kuwanufaisha wakulima kwa bei na soko la uhakika. 

Utaratibu wa kuuza kahawa mnadani ulianza kutumika Julai mwaka jana (2018) na unafanyika chini ya usimamizi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) ambayo imepewa jukumu la kupanga bei kulingana na gharama za uzalishaji na upatikanaji wa soko. 

Juhudi hizo zinalenga kudhibiti biashara haramu ya kahawa ikiwemo wakulima kuuza kahawa kwa watu binafsi wanaowafuata mashambani au kupeleka nje ya nchi bila kufuata utaratibu uliowekwa. 

Wakati Serikali ikitafuta mbinu za kuboresha mauzo ya zao hilo, takwimu za Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa cha mwaka 2017 kinachopatikana katika tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa mwenendo wa uzalishaji wa kahawa umekuwa ukipanda na kushuka kila mwaka jambo linaloibua maswali mengi kuhusu mikakati ya kuboresha zao hilo la biashara nchini ili liendelee kupaa kila siku. 

Mathalani katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita uzalishaji umekuwa ukiporomoka kila mwaka ambapo mwaka 2018 uzalishaji ulikuwa tani 41,679.4 chini kidogo ya makisio yaliyotolewa na TCB ya tani 43,000. 

Hali haikuwa nzuri pia mwaka 2017 ambapo zilizalishwa tani 48,329 ikiwa ni anguko  la asilimia 20.7 ikilinganishwa na tani 60,201 zilizopatikana mwaka 2016. 

Kahawa ndiyo zao la biashara linaloshika nafasi ya tatu katika kulingizia Taifa fedha nyingi za kigeni baada ya korosho na tumbaku ambapo mwaka 2017 iliingiza Sh282.4 bilioni. 

Pamoja na umuhimu huo, bado linakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa na upatikanaji wa pembejeo za kilimo. 

“Hata hivyo, uzalishaji wa Pamba, chai, mkonge na kahawa ulishuka mwaka 2017 kutokana na uhaba wa mvua katika maeneo ya uzalishaji na matumizi hafifu ya pembejeo hususan mbegu bora na mbolea,” imeeleza sehemu ya Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa

Pia, baadhi ya wakulima wamekuwa wakiuza kahawa ikiwa bado shambani na  wengine kutorosha nje ya mipaka ya Tanzania ili kufuata bei nzuri ya zao hilo hasa katika nchi za Uganda na Burundi, jambo ambalo linakwamishwa upatikanaji wa takwimu sahihi za uzalishaji kila mwaka. 

Hata hivyo, TCB inaeleza kuwa uzalishaji wa kahawa katika msimu wa 2018/2019 walikuwa wanaratajia ongeongezeka kwa asilimia 44 hadi kufikia tani 60,000 kutokana na kuimarika kwa hali ya hewa. 

Pamoja na makisio hayo, bado kiwango hicho cha uzalishaji hakitaweza kufikia uzalishaji wa mwaka 2013 ambapo ulivunja rekodi ya kuzalisha tani 71,200, kikiwa ni kiwango kikubwa kuwahi kufikiwa ndani ya miaka nane iliyopita. 

Mkakati wa Maendeleo ya Sekta ya Kahawa (2011‐2021) unakusudia kuongeza  uzalishaji hadi kufikia tani 100,000 ifikapo mwaka 2021 lakini huenda ukatatizwa na tatizo la kuwepo kwa mibuni iliyozeeka pamoja na kutozingatia kanuni bora za kilimo cha kahawa miongoni mwa wakulima.


Zinazohusiana:


Serikali yajipanga kuboresha kilimo cha Kahawa 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha mikakati ya kukuza zao la kahawa ikiwemo kutoruhusu kuuzwa nje ya nchi kabla ya kukobolewa, kwa lengo la kuiongezea thamani kabla ya  kuingizwa sokoni.

Pia ameziagiza halmashauri zinazolima kahawa nchini kuwa na kitalu chenye miche zaidi ya 200,000 ifikapo mwishoni mwa Februari mwaka huu ili kuhakikisha msimu ujao miche inapatikana kirahisi.

"Hairuhusiwi kutoa kahawa nchini na kuiuza nje ya nchi ikiwa bado na maganda, ni lazima iongezewe thamani ndipo ipelekwe katika masoko ya nje ya nchi ili iuzwe kwa bei nzuri. 

“Hatua hii itasaidia kuongeza mnyororo wa thamani na kusaidia kulinda uwekezaji wa viwanda uliofanyika nchini,” alisema Majaliwa Januari 4, 2019 wakati akizungumza na wadau wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.

Katika kuhakikisha kunakuwa na taarifa sahihi, amevitaka vyama msingi vya wa wakulima (AMCOS) kuhakikisha wakulima wote wanasajiliwa na taarifa zao ikiwemo ukubwa wa mashamba, kiasi cha uzalishaji na mahali walipo zinatunzwa vizuri katika kompyuta. 

Related Post