Wafahamu wanawake watano tajiri zaidi duniani

March 10, 2025 6:28 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Alice Walton, Julia Koch na Jacqueline Mars.
  • Wengi wao wametokea katika sekta ya biashara na viwanda.

Dar es Salaam. Licha ya wanaume kuendelea kutamba katika orodha ya watu tajiri zaidi duniani, jarida la Forbes la nchini Marekani  mwaka huu limetoa  orodha ya wanawake watano tajiri zaidi duniani.

Jarida hilo linalotolewa kila mwaka huangazia masuala ya mbalimbali yanayohusu uchumi, uwekezaji, teknolojia, biashara, ujasiriamali, na maisha ya watu mashuhuri wa sekta ya kifedha, ambapo mwaka huu limeainisha wanawake watano tajiri zaidi kutoka katika sekta mbalimbali.

Sekta hizo ni pamoja na viwanda na madini vikijumuisha uzalishaji wa bidhaa kama chakula na vipodozi ambazo zimewafanya wang’are katika orodha hiyo tofauti na sekta maarufu zilizoeleka kutoa matarajiri ikiwemo teknolojia.

Kwa mujibu wa Forbes, kuna zaidi ya mabilionea 2,700 duniani kote, wakiwa na jumla ya utajiri wa Dola trilioni 14.2 za Marekani.

Katika mwezi huu wa wanawake Nukta habari imeangazia wanawake watano tajiri zaidi duniani kwa mwaka 2025 ambao baadhi yao utajiri wao umetokana na uwekezaji katika sekta mbalimbali.

5. Familia ya Savitri Jindal

Savitri Jindal (74) ni mwenyekiti mstaafu wa OP Jindal Group, kampuni inayojumuisha viwanda vya uzalishaji wa chuma, nishati, saruji, na miundombinu, iliyoanzishwa na marehemu mumewe, O.P. Jindal. 

Baada ya kifo cha O.P. Jindal mwaka 2005, biashara za kundi hilo ziligawanywa miongoni mwa wana wao wanne. 

Jindal ndio mwanamke tajiri zaidi nchini India, ameongeza utajiri wake kwa Dola bilioni 3.2 za Marekani sawa na Sh8.4 trilioni tangu Machi 2024. Picha | AN LANGSDON

Kwa sasa Jindal ndio mwanamke tajiri zaidi nchini India, ameongeza utajiri wake kwa Dola bilioni 3.2 za Marekani sawa na Sh8.4 trilioni tangu Machi 2024, na kufikia jumla ya Dola bilioni 35.8 za Marekani sawa na Sh93.7 trilioni.

Jindal pia aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Miji katika Serikali ya Haryana.

4. Jacqueline Mars 

Jacqueline Mars (85) anamiliki takriban theluthi moja ya Mars, Incorporated, kampuni kubwa ya pipi, chakula, na huduma za wanyama (pets).

Kampuni hiyo iliyanzishwa na babu yake, Frank Mars, mwaka 1911. Mars alirithi hisa zake baada ya kifo cha baba yake, Forrest Sr., mwaka 1999. Jacqueline alifanya kazi katika kampuni hiyo kwa karibu miaka 20 na aliwahi kuwa kwenye bodi ya kampuni hadi mwaka 2016.

Jacqueline Mars (85) anamiliki takriban theluthi moja ya Mars, Incorporated, kampuni kubwa ya pipi, chakula, na huduma za wanyama (pets). Picha | GETTY IMAGES

Katika safari yake ya kiuzalishaji Mars ameongeza Dola bilioni 3.2 za Marekani sawa na Sh8.4 trilioni kwenye utajiri wake tangu Machi 2024, na kufikia jumla ya Dola bilioni 41.7 za Marekani sawa na Sh109.2 trilioni.

Mwaka 2024, Mars iliinunua hoteli ya Hotel Chocolat, na kutangaza ununuzi wa Dola bilioni 35.9 za Marekani sawa na Sh93.9 trilioni wa kampuni ya Kellanova, ikiunganisha biashara hizo mbili na kupanua wigo wake wa kimataifa, huku muamala huo ukitarajiwa kukamilika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025.

3. Familia ya Françoise Bettencourt Meyers 

Françoise Bettencourt Meyers (71) ni mjukuu wa mwanzilishi wa kampuni ya L’Oréal na familia yake, wenye umiliki wa zaidi ya theluthi moja ya kampuni hiyo ya vipodozi.

Hata hivyo, Bettencourt Meyers amepoteza karibu Dola bilioni 28.9 za Marekani sawa na Sh75.2 trilioni tangu Machi 2024, na kushuka kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tatu katika orodha ya wanawake tajiri zaidi duniani, akiwa na utajiri wa Dola bilioni 70.6 za Marekani sawa na Sh184 trilioni. 

Bettencourt Meyers amehudumu kwenye bodi ya L’Oréal tangu 1997 na amekuwa mwenyekiti wa kampuni ya familia, Téthys, tangu 2012. Picha | IAN LANGSDON / POOL/ AFP.

Bettencourt Meyers amehudumu kwenye bodi ya L’Oréal tangu 1997 na amekuwa mwenyekiti wa kampuni ya familia, Téthys, tangu 2012. 

Kikundi hicho kiliripoti mauzo ya Dola bilioni 36.3 za Marekani sawa na Sh94.8 trilioni katika miezi tisa ya kwanza ya 2024. Mwaka huo huo, L’Oréal ilitangaza hatua mbili muhimu, ununuzi wa hisa zote za kampuni ya Uswisi, Gjosa, inayojihusisha na teknolojia ya kugawanya maji, na ununuzi wa asilimia 10 ya hisa katika Galderma Group kutoka kwa Sunshine SwissCo, Mamlaka ya Uwekezaji ya Abu Dhabi, na Auba Investment Pte. Ltd.

2. Familia ya Julia Koch 

Julia Koch (62) pamoja na watoto wake watatu, walirithi asilimia 42 ya hisa katika kampuni ya  Koch Industries baada ya kifo cha mumewe, David Koch, mwaka 2019. Utajiri wake umeongezeka kwa zaidi ya Dola bilioni 9.9 za Marekani sawa na Sh25.9 trilioni  tangu Machi 2024, na kufikia jumla ya Dola bilioni 74.2 za Marekani sawa na 194.8 trilioni. 

ulia Koch (62) pamoja na watoto wake watatu, walirithi asilimia 42 ya hisa katika kampuni ya  Koch Industries. Picha | Forbes.

Mwezi Februari 2024, taasisi yake ya Julia Koch Family Foundation, ilitoa Dola milioni 75 za Marekani sawa na Sh196.3 bilioni kuanzisha kituo cha huduma za wagonjwa wa nje cha Julia Koch Family huko West Palm Beach. Na kufikia mwezi Juni 2024, yeye na watoto wake walipata asilimia 15 ya hisa katika BSE Global ya Brooklyn Nets kwa takriban Dola milioni 700 za Marekani sawa na Sh1.83 trilioni. Kwa sasa Julia Koch anahudumu kwenye bodi za Koch Industries na Kituo cha Saratani cha Memorial Sloan Kettering.

1. Alice Walton 

Alice Walton (75) ni mwanamke pekee mwanzilishi wa kampuni ya  Walmart inayojishughulisha na uuzaji wa bidhaa za rejareja (retails). Walton alikuwa mwanamke tajiri zaidi duniani mnamo Septemba 2024, kwa mara ya kwanza tangu Mei 2022, kutokana na ongezeko kubwa la bei ya hisa za Walmart.

Alice Walton (75) ni mwanamke pekee mwanzilishi wa kampuni ya  Walmart inayojishughulisha na uuzaji wa bidhaa za rejareja (retails). Picha | Forbes.

Utajiri wake umeongezeka kwa Dola bilioni 28.6 za Marekani sawa na Sh74.8 trilioni  tangu Machi 2024, na kufikia jumla ya Dola bilioni 100.9 za Marekani sawa na Sh264 trilioni. 

Tofauti na ndugu zake, Walton amejikita zaidi katika fedha, sanaa, na shughuli za kijamii badala ya kushika nafasi kwenye bodi ya Walmart. 

Aliwahi kufanya kazi kama mchambuzi wa hisa, kuanzisha kampuni ya uwekezaji wa kibenki, na kuwa makamu mwenyekiti wa Arvest Bank Group.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks