Wafahamu watu 10 tajiri zaidi duniani 2025
- Ni pamoja na Jensen Huang, Steve Ballmer, pamoja na Larry Ellison.
- Elon Musk aweka rekodi ya kuwa na utajiri wenye thamani ya zaidi ya Dola 400 bilioni za Marekani.
- Wengi wao wamewekeza kwenye sekta za ubunifu na teknolojia.
Dar es Salaam.Ukuaji wa teknolojia umeendelea kuchochea ongezeko la utajiri duniani jambo ambalo limesababisha watu waliowekeza katika sekta hiyo kuendelea kujikusanyia ukwasi na kutawala orodha ya watu wenye ukwasi mwingi zaidi duniani.
Orodha ya watu matajiri duniani ya mwaka 2025 inayotolewa na Jarida la Forbes la nchini Marekani inaonesha chanzo cha utajiri wa watu 10 matajiri zaidi ni uwekezaji katika teknolojia na biashara.
Kwa mujibu Forbes duniani kuna zaidi ya mabilionea 2,700 wakiwa na jumla ya utajiri wa Dola Trilioni 14.2 za Marekani wakitokea katika sekta mbalimbali kama teknolojia, biashara, na huduma za kifedha na makala hii inaangazia watu 10 tajiri zaidi.
10. Jensen Huang
Mfanyabiashara huyu raia wa Marekani mwenye asili ya Taiwan, ameuanza mwaka 2025 akishikilia nafasi ya 10 katika orodha ya watu 10 matajiri ulimwenguni.
Huang mwenye umri wa miaka 61 kwa sasa anautajiri wenye thamani ya Dola za Marekani 117.2 bilioni sawa na Sh305 trilioni ambapo chanzo chake kikuu cha utajiri huo kikiwa ni kampuni yake ya Nvidia aliyoianzisha mwaka 1993.
NVIDIA ambayo makao yake yapo Califonia nchini Marekani ni kampuni ya kimataifa inayobobea katika utengenezaji wa vifaa na programu za kiteknolojia, ikiwa ndiyo kampuni nguli na suluhisho katika masuala ya akili bandia (AI) ambayo imekuwa inatumika katika magari ya kujiendesha yenyewe sambamba na uundaji wa michoro ya filamu na michezo ya video yani Graphics Processing Units (GPUs).
9. Steve Ballmer
Steve Ballmer (68) mfanyabiashara na raia wa Marekani anashikilia nafasi ya tisa katika orodha ya watu 10 matajiri ulimwenguni akiwa na utajiri wenye thamani ya Dola za Marekani 124.3 bilioni sawa na Sh 348 trilioni.
Ballmer ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Microsoft kuanzia mwaka 2000 mpaka mwaka 2014 ambayo ndio chanzo cha utajiri wake pamoja na uwekezaji anaoufanya katika maeneo mengine.
Aidha, Baller anamiliki timu ya mpira wa kikapu ya Los Angeles Clippers inayo shiriki Ligi Kuu ya Mpira wa Kikapu Marekani maarufu kama(NBA), ambayo ni ligi maarufu zaidi duniani. Umiliki wa timu hii unatajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vya utajiri.
8. Warren Buffett
Warren Buffett (94) mfanyabiashara raia wa Marekani anatajwa kushikilia nafasi ya nane kati ya watu 10 matajiri zaidi ulimwenguni akiwa na utajiri wenye thamani ya Dola za Marekani 141.7 bilioni sawa na kiasi cha Sh365.5 trilioni.
Chanzo cha utajiri wa Buffett ni uwekezaji katika kampuni ya Berkshire Hathaway ambayo kwa sasa yeye ndiye Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji.
Kampuni ya Berkshire Hathaway inajihusisha na uwekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na bima, usafirishaji wa reli (BNSF Railway), nishati, rejareja, utengenezaji, na huduma za kifedha.
Berkshire Hathaway pia inamiliki hisa kubwa katika kampuni mashuhuri kama Apple, Coca-Cola, na American Express. Makao makuu ya kampuni hiyo yakiwa mjini Omaha, Nebraska, Marekani.
Kutokana na kuwa chanzo cha utajiri wa Buffett ni uwekezaji, Buffet anajulikana kama mwekezaji bora Duniani.
7. Sergey Brian
Sergey Brian (51) mfanyabiashara na mtaamu wa masuala ya kompyuta anashikilia nafasi ya saba katika orodha ya watu 10 matajiri ulimwenguni akiwa na utajiri wenye thamani ya Dola za Marekani 149 bilioni ,sawa na Sh383 trilioni.
Chanzo kikubwa cha utajiri wake ni kampuni ya Google ambayo aliachia madaraka ya kampuni hiyo mwaka 2019 lakini akibakia kuwa mwanachama wa bodi na mshika hisa wa kampuni.
Brian pia ndiyo mvumbuzi wa kampuni ya Google akishirikiana na Larry Page mwaka 1998 ambaye walikutana katika chuo kikuu cha Stanford nchini Marekani wote wakisomea shahada ya Sayansi ya Kompyuta.
6. Larry Page
Lawrance Page (51) ni mfanyabiashara maarufu raia wa Marekani, anayejulikana kwa utaalamu wake wa masuala ya sayansi ya kompyuta na mvumbuzi mwenza wa Google, anashikilia nafasi ya sita katika orodha ya watu 10 matajiri ulimwenguni akiwa na utajiri wa Dola 156 bilioni za Marekani sawa na Sh414.2 trilioni .
Chanzo kikuu cha utajiri wa Page ni kampuni ya Google ambayo walishirikiana na Sergey Brian kuivumbua walipokutana chuo.
Wewe na rafiki yako mnashirikiana kuvumbua nini?
5. Benard Arnault
Benard Arnault (75) mfanya biashara raia wa Ufaransa anatajwa kushikilia nafasi ya tano kwenye orodha ya watu matajiri ulimwenguni akiwa na utajiri wenye thamani ya Dola za Marekani 168.8 bilioni sawa na Sh414.2 trilioni.
Chanzo kikuu cha utajiri wa Arnault ni kampuni ya LVMH (Moët Hennessy Louis Vuitton) ambayo yeye ndiye mvumbuzi, mwenyekiti na Mkurugenzi wa kampuni hiyo.
LVMH (Moët Hennessy Louis Vuitton) ni kampuni kubwa ya kimataifa inayojihusisha na bidhaa za kifahari, ikiwa na makao makuu mjini Paris, Ufaransa.
Kampuni hii inamiliki chapa maarufu kama Louis Vuitton, Dior, Moët & Chandon, Hennessy, Givenchy, na Bulgari, ikihusisha sekta za mitindo, manukato, saa za kifahari, na pombe.
4. Mark Zuckerberg
Mark Zuckerberg (40) ni mfanyabiashara raia wa Marekani anayejulikana sana ulimwenguni hii ni kutokana na ugunduzi wa mtandao wa kijamii wa Facebook.
Mark Zuckerberg anatajwa kushika nafasi ya nne katika orodha ya watu 10 matajiri ulimwenguni akiwa na utajiri wenye thamani ya Dola bilioni 202.5 za Marekani sawa na Sh497.3 trilioni.
Chanzo kikuu cha utajiri wa Mark Zuckerberg ni kampuni ya meta ambayo ndiyo kampuni yenye umiliki wa mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram, na Whatsapp, pamoja na Threads.
Kwa sasa Mark Zuckerberg ndiye Mwenyekiti, Mkurugenzi na Mratibu wa hisa zote katika kampuni ya Meta.
03. Larry Ellison
Larry Ellison (80) mfanyabiashara raia wa Marekani anatajwa kushikilia nafasi ya tatu katika orodha ya watu 10 matajiri duniani akiwa na utajiri wenye thamani ya Dola za Marekani 209.7 bilioni sawa na Sh515 trilioni.
Chanzo kikuu cha utajiri wa Larry Ellison ni kampuni ya Oracle ambayo amekuwa mkurugenzi wake kwa miaka 37 mpaka alipoachia ngazi mwaka 2014, na sasa amebaki kuwa mkuu wa kitengo cha teknolojia na mwenyekiti wa kampuni hiyo.
Oracle Corporation ni kampuni kubwa ya teknolojia ya kimataifa inayojihusisha na maendeleo ya programu za biashara, pamoja na huduma za uhifadhi data (cloud), na mifumo ya usimamizi wa hifadhi data.
02. Jeff Bezos
Jeff Bezos (60) mfanyabiashara raia wa Marekani ndiye anatajwa kushika nafasi ya pili katika orodha ya watu 10 matajiri duniani akiwa na utajiri wenye thamani ya Dola za Marekani 233.5 bilioni sawa na Sh573.1 trilioni.
Utajiri wa mfanyabiashara huyo unachangiwa zaidi na umiliki wa kampuni ya Amazon ambayo Jeff Bezos ndiye mvumbuzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi kwa sasa ambapo pia amewai kushikilia nafasi ya urais, na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Amazon.
Amazon ni kampuni ya kimataifa ya teknolojia inayojihusisha na biashara mtandaoni, huduma za uhifadhi data (cloud computing), vifaa vya kielektroniki, na burudani ya kidijitali.
Inajulikana sana kwa soko lake mtandaoni linalouza bidhaa mbalimbali, kupitia Amazon Web Services (AWS), na vifaa kama Kindle, Echo, na Fire TV.
01. Elon Musk
Mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa mtandao wa X, Elon Musk (53) ameunza mwaka mpya akiwa sio tu mtu tajiri zaidi duniani, bali pia bilionea wa kwanza katika miongo minne kufuatiliwa na Forbes kuwa na utajiri wenye thamani ya zaidi ya Dola 400 bilioni za Marekani.
Kwa mujibu wa makadirio ya Forbes, Musk anaingia mwaka mpya akiwa na thamani ya Dola bilioni 421.2 za Marekani sawa na Sh1.03 quadrilioni,
Mabadiliko makubwa katika utajiri wake yalitokea baada ya SpaceX kukubali kununua hisa za wafanyakazi wa ndani kwa makubaliano yaliyoipatia kampuni hiyo thamani ya Dola bilioni 350 za Marekani ambapo awali, SpaceX ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani bilioni 210.
Musk alianzisha SpaceX mwaka 2002 na anaiongoza kama Mkurugenzi Mtendaji huku akiwa na umiliki wa takriban 42% ya hisa za kampuni hiyo.
Thamani mpya ya SpaceX imeifanya kuwa kampuni ya kibinafsi yenye thamani kubwa zaidi duniani, ikizidi ByteDance, kampuni mzazi wa TikTok, Stripe inayoshughulika na malipo, na OpenAI, watengenezaji wa ChatGPT.
Musk pia anaongoza kampuni ya magari ya umeme Tesla na ana hisa katika kampuni za mitandao ya kijamii X, kampuni ya akili bandia AI, na kampuni ya vichuguu Boring Co.
Musk ambaye utajiri na umaarufu wake umeongezeka zaidi baada ya Donald Trump kushinda uchaguzi wa urais wa Marekani ambapo yeye alikuwa mstari wa mbele kumnadi na Trump alimteua Musk kuwa mwenyekiti mwenza wa baraza jipya la ushauri, katoka Idara ya Ufanisi wa Serikali (DOGE), linalolenga kupunguza matumizi ya Serikali na kuongeza ufanisi.
Je, ni nani ulitegemea kumuona kwenye orodha hii lakini hujamuona ?
Vp kuhus Bill gates? Mana amekuwa akishikilia Nafas ya juu kwa muda mref imekuwaje sashiv??