Wafahamu wanafunzi 10 bora mtihani darasa la saba mwaka 2020

November 21, 2020 10:39 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Msichana kutoka Graiyaki awatakisa wavulana baada ya kuongoza kitaifa.
  • Shule ya Kwema Modern iliyopo mkoani Shinyanga yaingiza wanne kwa mpigo. 

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limemtangaza Herrieth Josephat kutoka Shule ya Msingi ya Graiyaki mkoani Mara kuwa ndiyo mwanafunzi bora kitaifa katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2020 uliofanyika mapema Oktoba mwaka huu.

Herrieth ndiyo mwanafunzi pekee wa kike katika orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa iliyotangazwa leo Novemba 21, 2020 jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa baraza hilo Dk Charles Msonde.

Herrieth anafuatiwa kwa karibu na Huma Huma kutoka Kwema Modern iliyopo mkoani Shinyanga pamoja na Gregory Alphonce kutoka Twibhoki mkoani Mara. 

Wanafunzi wengine katika 10 hiyo bora ya mwaka 2020 ni Nyambina Nyambina wa Graiyaki, Andrew Mabula wa Kwema Modern, na Jonas Ayubu wa Little Flower iliyopo pia mkoani Mara.


Soma zaidi: 


Katika orodha hiyo ya dhahabu wapo pia Emmanuel Paul na Emmanuel Marwa wa Kwema Modern, Prosper Tumbo na Yesaya Bendera wote wa God’s Bridge iliyopo mkoani Mbeya.

Shule ya Kwema Modern ndiyo imetawala zaidi katika orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa baada ya kuwa na wanafunzi wa nne katika kinyang’anyiro hicho cha juu ikifuatiwa kwa karibu na Graiyaki ya Mara na God’s Bridge ambazo zimeingiza wanafunzi wawili wawili kila moja.

Wanafunzi nane kati ya 10 walioingia katika orodha ya 10 bora mwaka huu wanatoka katika shule za msingi zilizopo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Mara na Shinyanga. Mbeya ndiyo mkoa pekee uliowakilishwa katika orodha hiyo yenye wanafunzi wenye ufaulu wa juu zaidi nchini.

Enable Notifications OK No thanks