Wafahamu wagombea watakaochuana na Samia nafasi ya Urais 2025

August 16, 2025 1:22 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Luhanga Mpina, Salum Mwalimu na Doyo Hassan Doyo

Dar es Salaam. Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu Tanzania utakaofanyika Oktoba 29 yanaendelea kushika kasi.

Hivi sasa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo,vinaendelea na michakato ya uteuzi wa wagombea kwa baadhi ya nafasi hususan ubunge na udiwani, huku uteuzi kwa nafasi ya urais ukiwa umeshakamilika na wagombea wateule wameshachukua fomu.

Aidha, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) nayo imemaliza zoezi la utoaji wa fomu kwa nafasi ya Urais na makamu wake kwa wagombea wa vyama vyote jana Agosti 15,2025.

Nukta Habari imekuandalia orodha ya wagombea wa watakaochuana na Samia Suluhu Hassan wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mgombea urais anayeomba ridhaa ya kuendelea kubaki madarakani baada ya mtangulizi wake John Magufuli kufariki.

Samia  anagombea pamoja na Dk Emmanuel Nchimbi  ambapo kama CCM itashinda nafasi hiyo basi atakuwa Makamu wa Rais wa Tanzania akichukua mikoba ya Dk Philip Mpango aliyeomba kustaafu siasa.

Chama cha upinzani ACT Wazalendo kimethibitisha kuingia ulingoni kwa kumsimamisha Luhaga Mpina kuchuana na Samia kuwania nafasi ya urais.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mbunge huyo wa zamani wa jimbo la Kisesa kujiunga na chama hicho kufuatia kukosa nafasi ya kutetea nafasi yake ya ubunge ndani ya CCM. 

Mpina atagombea pamoja na Fatma Fereji kama mgombea mwenza ambapo wote wanawania nafaso hiyo ya juu kimadaraka kwa mara ya kwanza.

Salum Mwalimu anatarajia kuchuana na Samia katika mbio za urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) ambapo wajumbe walimpa dhamana hiyo Agosti 7,2025 pamoja na Devotha Minja mgombea mwenza katika nafasi ya Makamu wa Rais. 

Chaumma ni moja kati ya vyama vya siasa ambavyo vimepata umaarufu mkubwa hivi karibuni kufuatia mamia ya waliokuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao hawakuunga mkono uamuzi a chama chao kutoshiriki uchaguzi mkuu wa 2025 kuhamia ndani ya chama hicho.

Kwa upande wa Chama Cha Alliance for African Farmers Party (AAFP) kimemsimamisha Kunje Ngombale Mwiru akishirikiana na mgombea mwenza wake Chumu Abdallah Juma kuwania urais.

Wagombea wengine ni Hassan Kisabya Almas akiwa na mgombea mwenza Hamis Ali Hassan kutoka Chama Cha National Reconstruction Alliance (NRA) Chama cha Makini (Makini Party) kimemuingiza Coaster Kibonde katika ulingo na National League for Democracy (NLD) itawakilishwa na Doyo Hassan Doyo. 

Aidha, Twalibu Kadege kupitia United Peoples’ Democratic Party (UPDP) ataingia katika pambano kuchuana na Samia katika Uchaguzi Mkuu 2025. 

Chama Cha Kijamii (CCK) kikiwakilishwa na David Daud Mwaijojele, akiwa na Masoud Ali Abdalla kama mgombea mwenza wake nacho kinatarajia kupimana ubavu na CCM Oktoba mwaka huu.

Tanzania Labour Party (TLP), imempeleka ulingoni Yustas Mbatina Rwamugira kama mgombea wake wa Urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Gabriel Bussungu atakiwakilisha  Chama cha Tanzania Democratic Alliance (TADEA), ambacho pia kinajulikana kama African Democratic Alliance Party (ADA-TADEA), kumwaga sera zake kuwania kiti ambacho kwa sasa kinakaliwa na Samia Suluhu Hassan. 

Wagombea wengine watakao mvaa Samia katika uchaguzi ni Haji Ambar Khamis wa Chama cha NCCR Mageuzi akiwa na mgombea mwenza Joseph Roman Selasini, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho.

Wengine ni Majaliwa Kyara atayeingia ulingoni kukiwakilisha Chama Cha Sauti ya Umma (SAU), Samandito Gombo atawakilisha Chama cha Wananchi (CUF), Naima Salum Mohamed akiwakilisha Chama Cha UDP, Mwajuma Noty Mirambo wa Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), na Abdul Mluya wa Chama cha Democratic Party (DP) 

Wagombea hawa wote watakwenda kunadi sera zao katika majimbo 272 ya uchaguzi nchini ili kuwashawishi wapiga kura zaidi ya milioni 37 ambao wamesajiliwa na INEC kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025.

Ikumbukwe kwamba, mpaka sasa chama kikuu cha upinzani, Chadema kimesema hakitashiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 wakitaka yafanyike kwanza mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na INEC, kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Tanzania Bara zinatarajiwa kuanza Agosti 28, 2025 na kumalizika Oktoba 28, mwaka huu, huku kwa upande wa Zanzibar, kampeni zitaanza Agosti 28, 2025 na kumalizika Oktoba 27.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks