Fahamu idadi ya majimbo na wapiga kura Uchaguzi Mkuu wa 2025

August 7, 2025 5:13 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Jumla ya wapiga kura 37,655,559 wamesajiliwa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2025.
  • Tanzania kwa sasa ina jumla ya majimbo 272 ya uchaguzi, majimbo 222 yapo Tanzania Bara na majimbo 50 yako Zanzibar. 

Dar es Salaam. Tanzania inaelekea katika kipindi muhimu cha kidemokrasia, ambapo Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unatarajiwa kufanyika tarehe 27 Oktoba 2025. Katika nyakati hizi , taarifa mbalimbali kuhusu uchaguzi zimekuwa zikisambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, baadhi zikiwa sahihi huku nyingine zikiwa za kupotosha.

Ni muhimu kwa wananchi na wapiga kura kupata taarifa sahihi na zinazotegemewa ili kukuza ushiriki wa kidemokrasia na kulinda amani ya nchi. Ili kufanikisha hilo, kila mtu anapaswa kufahamu kwa kina taarifa zote muhimu zinazohusiana na Uchaguzi Mkuu, ikiwemo idadi ya wapiga kura pamoja na majimbo ya uchaguzi. Ufahamu huu unasaidia kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa utulivu na kuepuka migogoro inayoweza kusababishwa na taarifa za upotoshaji.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa upande wa Tanzania Bara na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), jumla ya wapiga kura 37,655,559 wamesajiliwa kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba  2025. Kati yao wanaume ni milioni 18,712,104 huku wanawake wakiwa wengi zaidi  milioni hadi kufikia 18,943,455.

Tanzania Bara ina jumla ya wapiga kura milioni 36,929,683. Hii ni ongezeko la wapiga kura milioni 7.9 sawa na asilimia 26.6 kutokea wapiga kura milioni 29,754,696 waliosajiliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.Huku Zanzibar ikiwa na jumla ya wapiga kura 725,876 waliosajiliwa. 

Idadi ya majimbo 

Kwa upande wa majimbo ya uchaguzi, Tanzania ina jumla ya 272, kati ya hayo 222 yapo Tanzania Bara na 50 yako Zanzibar. Majimbo haya yamegawanywa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo idadi ya watu, jiografia na mahitaji ya uwakilishi wa kisiasa.

Katika orodha ya majimbo yenye wapiga kura wengi zaidi, Jimbo la Temeke linaongoza kwa kuwa na wapiga kura 560,788, likifuatiwa na Segerea 545,797, Kawe 532,173, Nyamagana 436,774, na Arusha Mjini 435,119. Majimbo haya yote yako Tanzania Bara.

Kwa upande mwingine, majimbo yenye idadi ndogo ya wapiga kura yapo zaidi visiwani Zanzibar. Majimbo hayo ni Chake Chake(1,942), Donge (2,050), Ziwani (2,379), Chumbuni (2,439) na Chonga (2,892). 

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, kila Mtanzania ana jukumu la kuhakikisha anatafuta taarifa kutoka kwenye vyanzo vinavyoaminika na kuepuka kusambaza habari za upotoshaji. 

Ni muhimu kuwa makini na kila taarifa unayoipokea kuhusu uchaguzi kwa kuhakikisha unatathmini chanzo chake.Je, taarifa hiyo inatoka kwenye chanzo rasmi na chenye mamlaka ya kisheria? Mifano ya vyanzo hivyo ni pamoja na Tume ya Uchaguzi kama INEC,/ZEC ofisi za serikali, vyombo vya habari vilivyosajiliwa, au vyama halali vya siasa. Utambuzi huu unasaidia kuimarisha uelewa sahihi wa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Taarifa hizi rasmi kuhusu idadi ya wapiga kura na majimbo ya uchaguzi ni msingi mzuri wa kuelewa namna demokrasia yetu inavyoendelea kukua, na kusaidia kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na uwazi.

Endelea kufuatilia Nukta fakti na Nukta habari kwa habari za kina na taarifa sahihi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks