Wadau walaani kushambuliwa waandishi wa Mwananchi
- Wadau watoa wito kwa vyombo vya dola kuchukua hatua kali za kisheria kwa wahusika.
- MCL yasema tukio hilo linakinzana na falsafa ya Rais Samia ya 4Rs.
Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wa habari nchini vikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamelaani tukio la kushambuliwa kwa wanahabari na dereva wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wakieleza kuwa vinarudisha nyuma uhuru wa habari.
Waandishi na dereva wa MCL walishambuliwa, kujeruhiwa na kuporwa mali na watu wasiojulikana Julai 22 mwaka huu walipokuwa wakifuatilia maandalizi ya mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chadema uliofanyika jana Jumapili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na MCL waandishi waliokumbwa na kadhia hiyo ni Fortune Francis, Sunday George pamoja na dereva aliyekuwa akiwaendesha Omary Mhando.
Tukio hilo lililotokea katika uwanja wa Bulyaga, Temeke jijini Dar es Salaam wakati watumishi hao wakitimiza majukumu yao ya kihabari.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na CCM mapema leo Julai 24, 2023, chama hicho tawala kimelaani na kukemea kitendo hicho cha uvunjifu wa amani huku wakiagiza dola kuwachukulia hatua waliohusika kuwashambulia wanahabari hao.
“CCM ikiwa mdau mkubwa wa tasnia ya habari na vyombo vya habari, inatoa wito kwa jamii kutambua, kuheshimu na kulinda uhuru wa wanahabari. Wanahabari wana wajibu wa kuelimisha kuhusu masuala mbalimbali yanayohusua maendeleo ya uchumi, kijamii na kisiasa,” amesema Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema.
Mjema amevitaka vyombo vya dola kuwachukulia hatua kali za kisheria wote waliohusika na tukio lilolaaniwa na wadau mbalimbali wa demokrasia nchini.
Wakati CCM wakieleza hayo, Chadema kimesema tukio hilo linahatarisha amani na utulivu wa nchi.
“Tunavitaka vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria mara moja wote waliohusika ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa ya amani, utulivu na usalama,” amesema John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema.
Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta) kimesema tukio hilo ni kinyume na ibara ya 18 ya katiba ya Tanzania inayowapatia wanahabari haki na uhuru wa kukusanya taarifa na kuhabarisha umma.
“Tukio hili tunalihesabu ni kitisho kwa wanahabari na wadau wote ambao wana uhuru wa kupata habari na kujieleza,” amesema Mwenyekiti wa Jowuta Taifa, Mussa Juma.
MCL yanena
Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Victor Mushi amesema shambulio hilo dhidi ya waandishi wake linahatarisha ustawi wa tasnia ya habari kwa kutengeneza mazingira yanayozuia wanahabari kufanya kazi zao kwa weledi.
“Shambulizi hili la kusikitisha linakinzana na falsafa ya R4 ya Serikali ya Awamu ya Sita inayozungumzia Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya kama msingi wa siasa za kidemokrasia Tanzania,” amesema Mushi.
Mushi ameongeza kuwa MCL inatarajia vyombo vya ulinzi na usalama vitimize wajibu wake kwa kuchunguza suala hili kwa undani na kuwachukulia hatua wale wote waliohusika katika kuwashambulia waandishi wake.
Serikali yatoa neno
Jioni ya siku ya tukio Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari , Nape Nnauye kupitia ukurasa wake wa Twitter alilaani kutokea kwa shambulio hilo na kuongeza kuwa anaamini vyombo vya dola vitafanya kazi yake kwa kuwa ni rahisi kuwabaini wahusika.
“Nimestushwa na kitendo hichi. NALAANI utamaduni wa kuwashambulia waandishi wakati wakitimiza majukumu yao. Naamini vyombo vitachukua hatua zinazostahili, kwani sidhani kama ni ngumu kuwapata waliofanya tukio hili…,” amesema Nape.
Nimestushwa na kitendo hichi. NALAANI utamaduni wa kuwashambulia waandishi wakati wakitimiza majukumu yao. Naamini vyombo vitachukua hatua zinazostahili, kwani sidhani kama ni ngumu kuwapata waliofanya tukio hili kwasababu eneo na kazi walizokwenda kufanya Waandishi zinajulikana. pic.twitter.com/3wkyc7AVQF
— Nape Moses Nnauye (@Nnauye_Nape) July 22, 2023
Latest
