Dk Gladness Salema achaguliwa na CCM kugombea ubunge EALA
- Atapigiwa kura Septemba 5, 2024 kuwania nafasi hiyo.
- Ni safari ya kumtafuta mrithi wa Dk Shongo Sedoyeka aliyefariki dunia Juni 13, 2024.
Dar es Salaam. Kamati ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) imemchagua Dk Gladness Salema kukiwakilisha chama hicho katika uchaguzi wa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) utakaofanyika Septemba 5, 2024 bungeni.
Dk Gladness ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amewashinda wapinzani wake wawili kwa kura 139 dhidi ya 53 za Lucia Pande na 52 za Queenelizabeth Makune.
Uchaguzi huo uliofanyika leo Jumatatu Septemba 2, 2024 katika ukumbi wa NEC White House, unalenga kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk Shongo Sedoyeka aliyefariki dunia Juni 13, 2024.

Wajumbe wa CCM wakiwa katika mchakato wa kumchagua mbunge wa kuwawakilisha chama hicho katika uchaguzi wa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.Picha l CCM
Kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi huo, Issa Haji Gavi alitangaza wabunge watapigia kura majina tisa kwa awamu ya kwanza, ili kupata washindi watatu.
Majina hayo tisa yaliyopigiwa kura ni kati ya wana CCM 10 walioteuliwa na chama hicho kugombea nafasi hiyo ambapo mmoja alijitoa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wengine waliokuwa wakigombea nafasi hiyo ni Maria Sebastian, Ester Chaula aliyejitoa, Prof Neema Kumburu, Fatma Kange, Hawa Mkwela, Fatuma Msofe na Theresia Dominic.
Wabunge wa EALA huchaguliwa kwa kipindi cha miaka mitano na wanaweza kuchaguliwa tena kwa kuteua wawakilishi wa nchi wanachama katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.