Dk Gladness Salema ashinda kwa kishindo ubunge wa Eala

September 5, 2024 12:47 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Apata kura za ndiyo 254 kati ya kura 274 zilizopigwa.
  • Anaungana na wabunge wengine nane wanaoiwakilisha Tanzania katika bunge la EALA.

Arusha. Bunge la Tanzania limemchagua Dk Gladness Salema kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kuziba nafasi ya Dk Shogo Mlozi aliyefariki dunia Juni 13 mwaka huu.

Dk Salema ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anaingia kwenye orodha ya wabunge wa EALA kwa kupata asilimia 97 za kura za ndio kati ya wabunge waliopiga kura leo Agosti 5, 2024 bungeni Dodoma.

Kwa mujibu wa Naibu Spika wa Bunge Mussa Azzan Zungu aliyekuwa akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Dk Salema alipata kura za ndio 254 kati ya kura 274 zlizopigwa huku kura za hapana zikiwa 18 na mbili zilizoharibika.

“Sasa namtangaza rasmi ndugu Gladness Salema kuwa ndiye mbunge wetu kutoka bunge letu kuiwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki,” amesema Zungu.

Kwa ushindi huo Dk Salema anakuwa sehemu ya wabunge wa bunge la tano Eala katika miaka mitatu iliyobakia hadi kufikia mwaka 2027 uchaguzi mwingine utakapofanyika.

Wabunge wa EALA huchaguliwa kwa kipindi cha miaka mitano na wanaweza kuchaguliwa tena kwa kuteua wawakilishi wa nchi wanachama katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akizungumza baada ya ushindi huo Dk Salema amewashurukuru wabunge wa CCM, kamati kuu ya chama cha CCM, wabunge wa upinzani, familia pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo amekuwa akifanya kazi kwa miaka kadhaa.  

“Naomba nimshukuru Rais wangu wa kwa kuniamini pamoja na chama changu cha mapinduzi (CCM) na viongozi wote, katibu mkuu, naibu Katibu mkuu, kamati kuu, sekretarieti na wabunge wa upinzani naamini pia nao wana imani na mimi,” amesema Dk Salema.

Dk Salema anaenda kuungana na wabunge wengine nane wanaoiwakilisha Tanzania katika bunge la Eala akiwemo Nadra Mohame, Mghembe Ngwaru, Dk Abdula  Makame, James Millya, Mashaka Ngole, Machano Machano, Angela Kizinga na Ansar Kashwamba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks