Wabunge 17 wachaguliwa kuwa wenyeviti kamati za kudumu za Bunge
- Hatua hiyo inayolenga kuimarisha usimamizi, uwajibikaji na ufanisi wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.
Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limechagua viongozi wa Kamati za Kudumu za Bunge la 13, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi, uwajibikaji na ufanisi wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yake.
Uchaguzi wa wenyeviti na makamu wenyeviti wa kamati hizo umefanyika kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za Bunge, ambapo wabunge walioteuliwa wanatarajiwa kusimamia kwa karibu sekta mbalimbali za maendeleo na matumizi ya fedha za umma ndani ya miaka mitano.
Taarifa iliyotolewa leo Januari 14, 2025, na Bunnge inabainisha kuwa miongoni mwa waliochaguliwa ni Dk Damas Ndumbaro ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria akisaidiwa na Edwin Swale.
Masuala ya uzalishaji na uchumi yanayoratibiwa na Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, yaongozwa na Deodatus Mwanyika na Mariam Mzuzuri, huku Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) ikiwekwa chini ya Najma Murtaza Giga na Paschal Chinyele.
Kwa upande wa Kamati ya Tamisemi, Florent Kyombo ndiye aliyechaguliwa kuiongoza akisaidiwa na Jafari Wambura huku Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ikiwa chini ya Hawa Mchafu na Regina Malima.
“Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Maji na Mazingira wamemchagua Jackson Kiswaga kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo na Profesa Pius Yanda amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti,” imesema taarifa ya Bunge iliyochaishwa katika mtandao wa Instagram..
Husna Sekiboko na Cornel Magembe wamechaguliwa kuongoza Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo huku Timotheo Mnzava na Mary Masanja wakisimamia pamoja Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Wengine waliochaguliwa ni Dk Johannes Lukumay na Zeyana Hamidi ambao wataongoza Kamati ya Afya na Masuala ya Ukimwi, wakati Kamati ya Miundombinu ikiongozwa na Seleman Kakoso pamoja na Abubakari Asenga inasimamia usafiri na ujenzi.
Kamati ya Nishati na Madini imewekwa chini ya Subira Mgalu na Simon Songe, Kamati ya Bajeti chini ya Mashimba Ndaki na Ally Omar King, na Kamati ya Sheria Ndogo chini ya Cecilia Paresso na Mfaume Zuberi.
Aidha, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imewekwa chini ya Masanja Kadogosa na Douglas Massaburi. Devotha Minja na Khalfan Aeshi, wamechaguliwa kuongoza Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC). huku Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)ikiwekwa chini ya Ado Shaibu na Abdallah Chikota.
Mlolongo huo wa uongozi bungeni unakamilishwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Anne Kilango Malecela akisaidiwa na Christina Mndeme.
Uteuzi wa viongozi hawa unatarajiwa kuzipa kamati uwezo wa kufanya kazi kwa karibu, kwa mshikamano na kwa ufanisi, ili kuhakikisha Serikali inawajibika kikamilifu mbele ya Bunge na wananchi katika kipindi cha Bunge la 13.
Latest