Makonda: Watumishi Wizara ya Habari fungeni mkanda
- Awataka kutekeleza majukumu yao kwa kasi.
- Sh2 bilioni kuwawezesha vijana waliojiajiri sekta ya habari.
Arusha. Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Paul Makonda amewataka watumishi wa wizara hiyo pamoja na idara zilizo chini yake kutekeleza majukumu yao kwa kasi na weredi.
Makonda aliyekuwa akizungumza kwa mara kwanza baada ya kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuiongoza wizara hiyo leo Januari 13, 2026 amesema hatavumiliia kiongozi yeyote mzembe asiyefanya majukumu yake ipasavyo.
“Naomba watendaji wote katika wizara zote na idara zote kila mtu akae kwenye kiti chake na aenee…tabia yangu inajulika siwezi kukuchekea wakati moyoni nimekununia,” amesisitiza Makonda.
Makonda anakabidhiwa wizara hiyo wakati ambapo bado kuna vuguvugu na sintofahamu iliyotokea kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 iliyopelekea baadhi ya Watanzania kususia vyombo vya habari vya ndani kwa madai ya kutoripoti yaliyotokea wakati huo.
Pamoja na kutwishwa zigo hilo Makonda ametangaza mwelekeo mpya wa wizara hiyo akinia kuwawezesha vijana waliojiajiri katika sekta ya habari kupata mitaji ya kununua vitendea kazi ikiwemo kamera.
“Mtaenda (vijana) kumlilia Rais Samia atupate fedha kiasi cha Sh1 bilioni mpaka Sh2 bilioni tuwakopeshe vijana kwenye mtandao wawe na vifaa vyao wenyewe…
…Ili unaporekodi usirekodi kwa simu uwe na kamera ya maana uwe na kompyuta yako halafu tengeneza maudhui ambayo dunia itaiona Tanzania kwa uzuri wake,” amesisitiza Makonda.
Latest