Vyandarua zaidi ya 200,000 kukabiliana na Malaria Misungwi, Mwanza

July 12, 2024 3:23 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Mkuu wa Wilaya aonya wanaotumia vyandarua kufugia kuku, kuvua samaki.

Mwanza. Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya imegawa zaidi ya vyandarua 200,000 kwa ajili ya dhidi ya ugonjwa wa maralia unaowashambulia hususani kwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi aliyekuwa akizungumza kwenye zoezi la kugawa vyandarua hivyo lililofanyika wilayani humo leo Julai 12, 2024 ameonya tabia ya baadhi ya wakazi katika wilaya hiyo kuvitumia vyandarua hivyo kufugia kuku au kuvulia Samaki hali inayosababisha wilaya hiyo kuwa na ongezeko kubwa la watu  wanaougua ugonjwa huo.

“Kama wewe ni mfugaji wa kuku tafuta namna nyingine itakayokusaidia kufuga kuku na sio kutumia vyandarua ambavyo vinagawiwa kwa lengo la kutokomeza malaria, halikadhalika kwa wavuvi hizi sio nyavu za kuvulia Samaki,” amesema Samizi

Mkuu huyo wa Wilaya amesema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita  wilaya hiyo imerokodiwa kuwa na asilimia 27.9 ya wagonjwa wa malaria na ni wilaya ya kwanza kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa hao.

“Lengo la Taifa hadi kufikia mwaka 2025 maambukizi ya ugonjwa huo yanatakiwa kuwa chini ya asilimia 3.5 na ifikapo mwaka 2030 yawe chini ya asilimia 1 sasa unapochukua chandarua na kwenda kukibadilishia matumizi matokeo yake hatutakuwa  tumefikia malengo hayo ya kitaifa ya kutokomeza ugonjwa huo,” amesema Samizi

Awali Afisa Afya wa Wilaya ya Misungwi, Dismas Milyongo amesema jumla ya vyandarua 292,179 vitagawiwa kwenye kaya 74, 000 zilizopo wilayani humo ambazo zimesajiliwa.


Soma zaidi:Chukua hiyo: Ndizi haziongezi maji maji (ute) ukeni


Ametaja malengo mahususi ya kugawa vyandarua hivyo ni hamasa kwa wananchi waweze kuvitumia katika kukabiliana na ugonjwa huo ambao takwimu zake zipo.

Baadhi ya wakazi wilayani humo wamekiri kuvibadilishia matumizi vyandarua hivyo kwakuhofia kuwa vinaweza kuwasababishia magonjwa hususan kwa akina baba ambao hupoteza nguvu za kiume.

Pius Mahundi ni Mkazi wa mtaa wa Misungwi amekiri kuwepo kwa imani hiyo lakini baada ya kupatiwa elimu amelazimika kwenda kuchukua ili kujikinga na ugonjwa huo.

“Mwanzoni niliamini kweli vyandarua hivyo vinavyosababisha upungufu wa nguvu za kiume hasa kutokana na dawa iliyowekwa lakini kwa sasa ninaelewa na nina washauri watu wote watakaochukua vyandarua hivi kuvitumia kwani havina madhara, na wasibadirishe matumizi yake,” amesema Mahundi.

Mkazi mwingine, Yunis Kimila amesema mbali na kujifunika vyandarua pia wanapaswa kufukia mashimo na kufyeka nyasi ili kuondoa mazalia ya mbu ambayo yapo karibu na nyumba zao.

Enable Notifications OK No thanks