Rais Samia ataja mambo manne yatayochochea uzalishaji wa umeme Tanzania
- Ni pamoja na kuongeza Megawati 2,463 za umeme katika gridi ya Taifa.
Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amebainisha mambo manne yatayoongeza upatikanaji wa umeme nchini kupitia utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa nishati (National energy compact) unaolenga kuongeza megawati 2,463 za umeme ifikapo mwaka 2050.
Ikiwa mkakati huo utatekelezwa kikamilifu Tanzania itakuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 5,894 lutoka 3,431 zilizopo hivi sasa jambo litakaloongeza upatikanaji wa nishati ya umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi ikiwemo uwekezaji kwenye viwanda na migodi.
Mkakati wa kitaifa wa nishati ni miongoni mwa matunda ya mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi wa Afrika uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam ukilenga kutengeneza njia ya Tanzania na nchi nyingine 11 kuongeza upatikaji wa umeme.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika mkutano leo Januari 28, 2025 amesema kuwa umeme huo unatarajiwa kuzalishwa kutoka vyanzo mbalimbali vitakavyohakikisha utoshelevu wa nishati hiyo nchini.
“Hadi sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha Megawati 3,431 za umeme zinazalishwa Tanzania ambapo asilimia 58 ni vyanzo vya maji, asilimia 35 gesi na asilimia 7 vyanzo vingine…Shabaha yetu ni kuongeza Megawati 2,463 za nishati kutokana na jua, gesi asilia, joto ardhi na vingine,” amesema Rais Samia.
Rais Samia Suluhu Hassan, Wakuu wa Nchi mbalimbali barani Afrika na Viongozi wengine wakishiriki Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Picha |Ikulu.
Kwa mujibu wa Rais Samia hadi kufikia Novemba 2024 mahitaji ya umeme nchini yalikuwa Megawati 1,888 wakati uzalishaji ukifikia Megawati 3,431 suala linaloiweka Tanzania kwenye nafasi nzuri ya kufanya biashara ya umeme nchi jirani ikiwemo Rwanda,Burundi, Kenya, Zambia na Uganda.
Itakumbukwa kuwa Januari 16 mwaka huu Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko alisema tayari maandalizi kwa ajili ya kuanza kuuza umeme huo yameanza kwa kujenga laini zitakazotumika kusafirisha umeme huo ikiwemo laini ya kutoka Iringa, Mbeya kwenda Tunduma, baadaye kuunganishwa na nchi ya Zambia.
“Nchi yetu tunao umeme wa ziada, kwa mitambo yetu yote tuliyonayo tukijumlisha, tuna zaidi ya megawati 740 ambayo ipo tu ambayo tungeweza kuitumia kama tungekuwa na mahali pa kupeleka,” alisema Dk. Biteko.
Katika hatua nyingine Rais Samia amesema mpango huo utasaidia kufikisha umeme kwenye vitongoji 11,532 ambavyo havijafikiwa na nishati hiyo baada ya kufanikiwa kufikisha umeme kwenye vijiji vyote nchini.
Awali Dk Biteko alisema kuwa vijiji vyote nchini 12,318 vimesambaziwa nishati ya umeme hivyo kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa mbalimbali zitokazo na nishati hiyo ikiwemo za kiuchumi.
Aidha, Mpango huo pia utasaidia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania hadi kufikia asilimia 80 kufikia mwaka 2030 kama ilivyoanishwa katika Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ulizozinduliwa mwaka 2024.
Trilioni 32.8 kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme Tanzania
Akizungumza katika mkutano huo Rais Samia amesema kuwa kupitia mpango huo Tanzania imelenga kufikia kasi ya usambazaji wa umeme kwa asilimia 72 huku Sh 32.8 trilioni zikihitajika.
Kati ya fedha hizo Rais Samia amesema Sh 12.6 trilioni inatarajiwa kutoka kwa wadau wa sekta binafsi waliopo ndani na nje ya nchi.
Mbali na fedha hizo wadau mbalimbali wa maendeleo Afrika wameutumia mkutano huo kuweka ahadi ya fedha zitakazosaidia kufikisha umeme kwa Waafrika milioni 300 kufikia mwaka 230.
Miongoni mwa wadau hao ni Benki ya Dunia (WB), Benki ya Afrika ya Maendeleo (AFDB) mfuko wa Opec na wengineo walioahidi Dola za Marekani bilioni 65.1 (Zaidi ya trilioni 166) kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo.