Chukua hiyo: Ndizi haziongezi maji maji (ute) ukeni

July 15, 2024 5:25 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ukavu ukeni husababishwa na mabadiliko ya vichocheo mwilini. 
  • Faida nyingine za ulaji wa ndizi ni pamoja na kuimarisha mifupa.

Dar es Salaam. Siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa nyingi kuhusu vyakula na vinywaji vinavyoongeza maji maji ukeni ambazo zimekuwa zikiwavutia watu wengi hususani wanawake.

Miongoni mwa vyakula  hivyo ni ndizi ambapo wasambaji wa taarifa hizo kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo Instagram na mitaani wanadai zinaongeza maji maji au ute ukeni jambo ambalo si kweli.

Nukta Fakti (nukta.co.tz) imezungumza na madaktari pamoja na wataalamu wa lishe ambao wamethibitisha kuwa matumizi ya ndizi kama chakula au kama tunda hayana mahusiano ya moja kwa moja na kuongezeka au kupungua kwa maji maji ukeni.

“Hizo ni habari za kusadikika hazina uhalisia wowote katika sayansi hii labda izungumziwe na wataalamu wa mambo ya asili ila sisi watalaamu wa kisayansi hatuna mambo hayo,” amebainisha Daktari Living Kimaro kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.


Zinazohusiana:Tumia vyakula hivi kupunguza ukavu ukeni


Naye Mtaalamu wa Lishe wa kujitegemea Yusuph Mbaruk amelezea kuwa madai hayo hayana uhusiano kabisa na kuongezeka kwa maji maji ukeni.

“Hakuna ushahidi wowote kuwa ndizi inaweza kuongeza majimaji ukeni ingawa kuna vyakula vinaweza kuchochea hali hiyo kama vile nyaya chungu au ngogwe lakini sio ndizi hivyo watu waache kupotoshana .” amesema Mbaruk.

Nini chanzo cha kupungua au kuongezeka kwa maji maji ukeni?

Mtaalamu wa Lishe wa kujitegemea Sophia Lugome kutoka jijini Mwanza anasema kuwa mara nyingi ukavu ukeni husababishwa na mabadiliko ya vichocheo mwilini hususani kwa wanawake waliokoma kuona siku zao (Menopause).

Nayo tovuti ya masuala ya afya ya Medical News Today ya nchini Marekani inabainisha kuwa tatizo hilo pia linaweza kuwapata wanawake wa rika zote hata mabinti ambao wameshavunja ungo huku ikitaja upungufu wa homoni ya estojeni kama chanzo.

“Ukavu ukeni unasababishwa na kiwango kidogo cha homoni ya estojeni ambayo inahusika na kulainisha uke na kuufanya uwe nyumbufu,” imesema tovuti hiyo.

  Kwa mujibu wa wataalamu wa afya ndizi mbivu na mbichi zote zinafaida katika mwili wa binadamu.Picha|Organic Facts.

Faida za kula ndizi

Mbali na taarifa hizo za uzushi matumizi ya ndizi kama tunda yanaweza kuwa na faida nyingi kwa watu wa rika na jinsi zote.

Tovuti ya masuala ya lishe ya Healthline inabainisha kuwa ndizi zinavirutubisho lukuki ikiwemo protini, Vitamini B6, C, Potasiamu na nyuzi nyuzi zinazoweza kuimarisha mfumo wa chakula.

“Cha zaidi ni kwamba nyuzi nyuzi zilizopo katika ndizi mbichi na mbivu husaidia tatizo la kutokupata choo na kukilainisha,” imefafanua tovuti hiyo.

Faida nyingine za ulaji wa ndizi ni pamoja na kuimarisha mifupa, kupunguza sukari kwenye damu na kuimarisha afya ya ubongo kama ilivyoainishwa na tovuti ya  BBC swahili  katika chapisho la Julai 9,2024.

Enable Notifications OK No thanks