Vodacom, TPB kuwawezesha wanachama wa Vicoba kutunza fedha kidijitali

March 1, 2019 11:37 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Wamezindua huduma ya  mtandaoni ya M-Koba iliyounganishwa na M-Pesa inayotoa fursa ya kuhifadhi fedha kwa usalama na uwazi.
  • Inatarajia kuondoa changamoto za upotevu wa fedha na kuimarisha mitaji ya vikundi hivyo.

Dar es Salaam. Wanachama wa vikundi vya kifedha vya kijamii (Vicoba), vikundi rasmi na visivyo rasmi maarufu kama ‘upatu’ sasa wamepata suluhu ya kuhifadhi fedha zao baada ya kampuni ya mawasiliano ya simu ya Vodacom kwa kushirikiana na benki ya Posta Tanzania (TPB) kuzindua huduma ya mtandaoni inalotoa suluhisho la utunzaji fedha kidijitali.

Huduma hiyo, iliyopewa jina la M-Koba, iko chini mfumo wa huduma za kifedha kwa njia ya simu wa M-Pesa, itawezesha vikundi hivyo kutunza fedha kidijitali kwa usalama na uwazi zaidi.

Kaimu Mkurugezi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi huo leo (Februari 28, 2019) jijini Dar es Salaam, amesema huduma hiyo itakuwa endelevu na kukidhi mahitaji ya vikundi vya kifedha kupata eneo salama la kutunza fedha na kuimarisha mitaji yao.

“Huduma hii ya kidijitali inalenga kutoa huduma endelevu ambayo itatumiwa na kufikia vikundi vilivyopo maeneo mbalimbali nchini kwa njia ya mtandao mkubwa wa Vodacom, “amesema Hendi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Vodacom, inakadiriwa kuwa asilimia 16 ya watanzania (zaidi ya watu milioni 4.4) wengi wao wakiwa wanawake, ni wanachama wa vikundi zaidi ya 50,000 vya kuweka akiba na mikopo (Vicoba) ambao huhifadhi akiba zaidi ya Sh100 bilioni kwa mwaka.

Pia kuna vikundi visivyo rasmi zaidi ya 50,000 visivyo rasmi vya wahitimu wa vyuo, wafanyakazi na wanafamilia ambao wanatumia mitandao ya kijamii kuweka akiba na kukopa.  

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi wa kwanza kulia akishirikiana na viongozi wengine kuonesha jarida la M-Koba wakati wa hafla ya kuzindua huduma ya M-Koba, huduma ya kwanza na ya kipekee nchini kwa ajili ya vikundi vya kuweka akiba nchini Tanzania.Picha|Vodacom.

Afisa Mtendaji mkuu wa TPB,  Sabasaba Moshingi amesema huduma hiyo inalenga kuongeza theluthi moja ya idadi ya watu waliosajiliwa katika mifumo rasmi ya kifedha na zaidi kuwafikia wanawake wa vijijini ambao wanajihusisha na shughuli hizo. 

“Kama taasisi ya kifedha, tunatambua umuhimu wa vikundi hivi na ndiyo sababu tumeshirikiana na vinara hawa wa sekta ya simu kuleta suluhisho hili la kidijitali ambalo litarahisisha kutunza akiba na kuwezesha watu kufikia malengo yao,” amesema Moshingi.


Soma zaidi: NMB yaingiza sokoni huduma tatu za kidijitali kwa mpigo


Naye Mwenyekiti wa mojawapo wa Vicoba aliyehudhuria uzinduzi huo, Abdallah Mkenga amesema huduma hiyo limekuja wakati mwafaka kwa sababu itawasaidia kutatua changamoto za utunzaji fedha. 

“Sasa tuna mfumo salama zaidi wa vikundi vyetu na tunachanga kwa uwazi kwani mfumo huu unaruhusu kuonekana kwa shughuli za kikundi,” amesema Mkenga.

Kutokana na umuhimu wake katika jamii, Vicoba vimejumuishwa katika Sheria mpya ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 ambapo sheria hiyo imeweka utaratibu wa kuiwezesha Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma ndogo za fedha hususan vikundi vya kijamii kwa lengo la kunufaika na fursa zilizopo.

Vicoba,wakopeshaji binafsi na asasi za kijamii vinaingia katika daraja la nne la sheria hiyo ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango wakati wa kupitisha sheria hiyo bungeni mwaka jana alisema vikundi hivyo viitaandaliwa kanuni na miongozo mahsusi kwa ajili ya kusimamia daraja hilo.

Enable Notifications OK No thanks