Vita ya baba na mtoto inayoacha alama kwenye familia
- Ni katika filamu ya Shang Chi inayomhusu kijana anayetafuta uhuru wa maisha yake.
- Kijana huyo anatoroka nyumbani lakini anasakwa kila kona.
- Anaporejeshwa nyumbani, anaingia katika uwanja wa mapambano na baba yake.
Dar es Salaam. Katika jamii yetu inategemewa mtoto aishi kwa matakwa ya wazazi wake. Akue akiishi maisha ya kuwapendeza hao waliompatia jina lake la mwisho.
Kwa Shang-Chi, yeye anataka kuishi maisha yake na pale baba yake anapoingilia kati, anatorokea San Francisco nchini Marekani na kubadili hadi jina lake akitaka kuitwa Shaun.
Shang-Chi and the Legend of the Ten Rings
Filamu hii ya ‘Shang Chi’ inaanza katika ardhi ya Uchina ambapo tunakutana na Xu Wenwu, akiwa amegundua silaha za maajabu zinazojulikana kama pete 10 lakini kwa ukubwa wa pete hizi, huenda pete siyo jina sahihi la kuzipatia.
Pete hizo zinampatia Wenwu nguvu za maajabu na uwezo wa kutokufa. Kwa kufahamu nguvu zake, anaanzisha shirika lake na analiita “Ten Rings Organization” analolitumia kupindua na kutwaa mataifa mengine.
Wahenga walisema madaraka hulevya na hivyo Wenwu anaona kuwa aliyo nayo hayatoshi. Anaanza kutafuta kijiji kinachojulikana kama Ta Lo na huko, kuna viumbe ambao akiwapata, atakuwa mtu mwenye nguvu zaidi duniani.
Huenda akawa wa pili baada ya Mungu. Walau alidhani hivyo.
Hata hivyo, safari ya kuitafuta Ta Lo inabadirisha muziki aliokuwa akiusikiliza Wenwu. Kutoka muziki wa ugaidi hadi kuanza kumsikiliza Celine Dion, au kibongo bongo, Jux na kina Maua Sama.
Bila shaka upo gizani. Ninachotaka kusema ni kuwa, gaidi huyo anakutana na Ying Li anayefanikiwa kuupokonya moyo wake kutoka kifuani kwake.
Yule gaidi aliyetembea na kuteka dunia amedondokea kwenye huba ya mlinzi wa kijiji cha Ta Lo.
Shang Chi anakutana ana kwa ana na baba yake kupambania uhuru wake. Picha| The Wrap.
Huba inayopelekea usaliti
Katika kupambana na Li, Wenwu anadondoka kwenye huba ya mwanadada huyo na wote wanaacha majukumu yao na kwenda kujenga familia.
Li anaachana na kijiji cha Ta Lo baada ya wanakijiji kumkataa mpenzi wake hivyo kwa kutaka penzi liendelee, anamfuata mahbuba wa moyo wake kokote aendapo.
Ajabu zaidi ni kuwa, Wenwu naye anatupilia mbali majukumu yake kwenye shirika la Ten Rings.
Kama wewe ni mdau wa fasihi basi unakumbuka vile Mazoea alivyotoroshwa na Ngoswe lakini kwa Li, yeye wala hajatoroshwa, ameondoka mwenyewe kujenga familia na Wenwu bila kujali historia ya baba huyo.
Tabasamu linakolea pale wawili hao wanabarikiwa kuzaa watoto wawili wa kwanza akiwa Shang Chi na mdogo wake Xialing. Hata hivyo, huzuni inaanza kunukia kwenye maisha yao na kukatisha urefu wa tabasamu walizokuwa nazo.
Wakati Shang Chi anatimiza miaka saba, mama yake anauliwa na waliokuwa maadui wa baba yake. Maadui hao wanaitwa Iron Gang au ki kwetu kwetu wangekuwa wanaitwa Genge la chuma.
Huzuni, hasira na majuto yanamfanya Wenwu kuchochea moto wa kisasi huku kuni yake akiwa ni mtoto wake , Shang Chi. Wenwu anamtengeneza mwanaye kuwa silaha ya maangamizi.
Reli inayosafirisha treni kijana Chi
Chi anapitishwa kwenye mafunzo makali yakimwandaa kupambana na adui zake na anapofikisha miaka 14, baba yake anamwagiza kwenda kudai maisha ya kiongozi wa genge la chuma.
Ni majukumu mazito kwa kijana huyo ambaye kwakuwa hata miaka 18 hajafikisha, unaweza kusema bado ni mtoto.
Anapofanikiwa, Chi anaamua kukimbilia San Francisco moyo wake ukiwa umejaa majuto na maulizo. Kusahau kila kitu kwenye historia yake, anaanza maisha mapya na anachukua jina la Shaun na kuanza kazi kwenye hoteli.
Wanasema hauwezi kuikimbia historia yako wala kutanga mbali na reli iliyofumwa kwa maisha yako. Na hivyo ndivyo inavyokuwa kwa Chi.
Siku siyo nyingi, wajakazi wa baba yake wanamfuata huko aliko wakilazimisha arudi nyumbani kuchukua nafasi yake kama mtoto wa baba yake.
Kabla sijanywa chai yote na kukuacha na na kikombe kitupu, Shuhudia filamu hii inayoonyeshwa kwenye kumbi za filamu za Century Cinemax na sehemu za kuangalizia filamu katika miji mikubwa likiwemo la Dar es Salaam.
Mtoto kukimbia familia yake, kisasi kikiwa kitovu cha maisha, madaraka ya kulevya na huba kuzaliwa penye chuki ni sehemu ya filamu hii.
Kutana na Simu Liu, Awkwafina, Tony Leung na wengine kibao katika filamu hii inayoacha historia kwa kampuni ya uandaaji wa filamu kali ya Marvel aliyoandaa filamu nyingi ikiwemo Avengers, Thor, Captain America na nyingine Kibao.