Matukio yaahirishwa, kifo cha mume wa Rais Samia
- Matukio hayo ni uzinduzi rasmi wa Mji wa Serikali Mtumba pamoja na uzinduzi wa Ramani ya Utekelezaji ya Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Uzazi, mama, mtoto mchanga, mtoto na vijana kwa mwaka 2026–2030.
Dar es Salaam. Matukio mawili makubwa yaliyokuwa yakitarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, yamesitishwa kufuatia kifo cha mume wake, Hafidh Ameir Hassan, aliyefariki dunia leo Jumatatu, Septemba 7, 2026.
Matukio hayo ni uzinduzi rasmi wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma, uliokuwa umepangwa kufanyika kesho Jumanne, Septemba 8, pamoja na uzinduzi wa Ramani ya Utekelezaji ya Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Uzazi, mama, mtoto mchanga, mtoto na vijana kwa mwaka 2026–2030, uliokuwa ufanyike Arusha Septemba 9.
Kabla ya kifo hicho, Serikali ilikuwa imetangaza kuwa Rais Samia angezindua Mji wa Serikali Mtumba katika hafla iliyopangwa kufanyika Uwanja wa Mashujaa uliopo ndani ya mji huo.
Uzinduzi huo ulitarajiwa kuhusisha majengo ya ofisi za Wizara 26, taasisi 11 za Serikali pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1.
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, ambayo imetoa taarifa ya kuahirishwa kwa tukio hilo mchana wa leo Septemba 7, 2026, imesema tarehe mpya ya uzinduzi itatangazwa baadaye.
Aidha, Rais Samia pia alikuwa anatarajiwa kuwa Arusha Septemba 9 kwa ajili ya kuzindua ramani ya utekelezaji ya ajenda yake kama Kinara wa Umoja wa Afrika katika Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Mtoto na Vijana kwa kipindi cha 2026–2030.
Uzinduzi huo ulipangwa kufanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) sambamba na Kongamano la Pili la Kimataifa la Huduma za Afya ya Msingi, kwa ushirikiano na Africa CDC.
Taarifa ya kifo cha Mzee Hafidh Ameir Hassan, imetangazwa leo Jumatatu, Septemba 7, 2026, baada ya kufariki dunia akiwa anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo Zanzibar.
Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, aliyetangaza taarifa za kifo chake amesema Mzee Hafidh alifariki majira ya saa mbili asubuhi katika hospitali alipokuwa akipatiwa matibabu.
Mzee Hafidh na Rais Samia walifunga ndoa mwaka 1978 na wamejaliwa watoto wanne. Kipindi cha uhai wake Mzee Hafidh Ameir Hassan alikuwa mtaalamu wa kilimo na aliwahi kulitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta hiyo.