Huyu ndiye Hafidh Ameir, mume wa Rais Samia Suluhu
- Mwenza wa kwanza wa Rais aliyefariki wakati Rais akiwa bado madarakani tangu uhuru.
Dar es Salaam. Mume wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Hafidh Ameir Hassan, amefariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Emilio Mzena Memorial, Zanzibar.
Taarifa ya kifo chake imetolewa leo Septemba 7,2026 na Makamu wa Rais wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ambaye amesema kuwa Hafidh Ameir alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo kabla ya kufariki.
“…Kilichotoke leo Septemba 7, 2026, majira ya saa mbili asubuhi katika Hospitali ya kumbukumbu ya Emilio Mzena Zanzibar, alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo,” ameeleza Ndejembi.
Hafidh Ameir ni nani?
Kwa mujibu wa wasifu wa marehemu uliowasilishwa baada ya maziko, yaliyofanyika leo Septemba 7, 2026 Kizimkazi, visiwani Zanzibar, safari ya maisha ya marehemu Hafidh Ameir Hassan ilianza Januari mosi mwaka 1946 katika kijiji cha Kisakasaka, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Tangu akiwa mdogo alionesha kiu ya elimu na dhamira ya kujifunza, jambo lililokuwa msingi wa safari yake ndefu ya mafanikio na huduma kwa jamii.
Alianza safari yake ya elimu katika Skuli ya Kombeni Shakani, Wilaya ya Magharibi B, ambapo alihitimu elimu ya msingi mwaka 1960. Baada ya hapo aliendelea na elimu ya sekondari katika Skuli ya Tumekuja, Mkunazini, na kuhitimu mwaka 1965.
Akiwa na mtazamo wa kuona elimu kama chombo cha mabadiliko, marehemu Hafidh hakuridhika na kiwango alichofikia, bali aliendelea kutafuta maarifa zaidi kupitia mafunzo mbalimbali ya kitaaluma, hususan katika sekta za ualimu na kilimo.
Mwaka 1970, alijiunga na Chuo cha Ualimu Zanzibar na kuhitimu mwaka 1973.
Hatua hiyo ilifungua ukurasa mpya katika maisha yake ya utumishi, ambapo alianza kazi ya ualimu na kuhudumu katika skuli mbalimbali Tanzania, akitoa mchango mkubwa katika kuwalea na kuwaelimisha vijana.
Mwaka 1980, alichaguliwa kujiendeleza katika masuala ya kilimo katika Chuo cha Kilimo Uyole, mkoani Mbeya, hatua iliyompa ujuzi mpana zaidi katika taaluma ya kilimo.
Mwaka 1982, aliteuliwa kuwa mkufunzi wa masomo ya kilimo katika Skuli ya Fidel Castro, Pemba, ambako aliendelea kutumia uwezo wake kuwaandaa vijana katika sekta muhimu ya kilimo.
Mwaka 1986, marehemu alipata fursa nyingine adhimu ya kuendeleza taaluma yake nchini Sri Lanka katika fani ya kilimo, ambapo alihitimu ngazi ya stashahada mwaka 1988 akiwa amebobea katika kilimo cha minazi.
Baada ya kurejea Zanzibar mwaka 1988, aliendelea kulitumikia Taifa kupitia Wizara ya Kilimo katika Wilaya ya Kaskazini Unguja.
Akiwa mtu mwenye kiu ya maendeleo ya kitaaluma, mwaka 1990 alisafiri kwenda nchini Uingereza kusomea Shahada ya Uzamili katika fani ya uhandisi wa mitambo ya kilimo (Agricultural Engineering).
Baada ya kurejea kutoka masomoni, aliendelea na majukumu yake katika Wizara ya Kilimo hadi alipostaafu mwaka 2005.
Hata hivyo, kustaafu kwake hakukuwa mwisho wa safari yake ya kutoa mchango kwa jamii, kwani aliendelea kufundisha katika Chuo cha Kilimo Kizimbani, Unguja.
Hafidh Ameir na Rais Samia walioana mwaka 1978, kabla ya Rais Samia kuanza safari yake ya siasa za kitaifa.
Katika maisha yake ya kifamilia, marehemu ameacha wajane wawili, watoto wanne na wajukuu kumi na watano, ambao wataendelea kuwa sehemu ya urithi wake wa upendo na maadili mema.
Katika jamii, marehemu Hafidha Amir Hassan atakumbukwa si kwa taaluma yake pekee, bali pia kwa utu wake.
Enzi za maisha yake Hafidh kwa kiasi kikubwa aliishi maisha ya faragha na hakujihusisha hadharani na shughuli za kisiasa, licha ya kuwa mume wa Rais wa nchi.
Alikuwa mtu wa watu, mwenye busara, upendo na moyo wa kusaidia wengine. Alijenga mahusiano mema na watu wa rika zote, wakiwemo wanafamilia, ndugu, jamaa, marafiki, majirani na wenzake wa kazi.
Maisha yake yalikuwa somo la kujituma, kujifunza na kuwahudumia wengine. Ameondoka duniani, lakini ameacha nyuma kumbukumbu ya mtu aliyotumia muda wake kujenga wengine na kuacha alama yenye thamani kwa jamii.
Urithi wa elimu, uadilifu na wema aliouacha utaendelea kuishi katika mioyo ya wote waliopata nafasi ya kumfahamu.