“My Name”: Filamu ya kuchangamsha wikiendi yako

October 22, 2021 8:56 am · Herimina
Share
Tweet
Copy Link

Yoo Ji Woo. Picha| Cheatsheet.com


  • Ni filamu inayomhusu binti anayepambana kulipiza kisasi.
  • Safari ya kulipiza kisasi inamfanya kuwa polisi msaliti.

Unaweza kusikiliza pia uchambuzi wa filamu hiyo hapa

                                                 


Dar es salaam. Katika filamu hii  ya “My name”, yaani jina langu, tunakutana na binti mrembo Yoo Ji Woo, ambaye katika maisha yake amekuwa akilelelewa na baba yake tu.

Kwa jinsi baba yake alivyokuwa akimpenda sana, basi Jiwoo anaweza kujiita “dad’s daughter” kama vile wadada huwa wanajigamba.

Maisha ya Jiwoo na baba yake siyo mazuri sana, kwani baba yake hakuwa na kazi rasmi ya kuwaingizia kipato zaidi ya kuwa mtu tuanayejihusisha na kazi haramu au tunaweza kumuita ‘gangstar’.

Licha ya umaskini wao, maisha ya upendo na  furaha yalikuwa ni kila kitu.

Maisha ya Jiwoo yanakuja kubadilika siku ambayo anatimiza miaka 17, kwani siku hiyo baba yake anaaga dunia kwa kupigwa risasi tena mbele ya macho yake.

Sidhani kama unaweza kuvaa viatu vya Jiwoo, yaani siku muhimu ya kufurahi ndiyo siku inayogeuka kuwa msiba, mshtuko, huzuni na hasira ni miongoni mwa mambo mengi yanayomkuta Jiwoo siku hiyo.

Jina langu

Maisha anayoanza kuishi Jiwoo baada ya baba yake kuuwawa ndiyo yanayoipatia filamuu hii jina la ‘My Name’, maana Jiwoo anahakikisha Korea Kusini yote inalijua jina lake.

Dada huyu anakuwa rasmi ‘gangstar’ kama baba yake na zaidi  anakuwa ni ‘ganstar’ asiye na huruma wala kumuogopa yeyote.

Maisha hayo yanakuja kuchochewa zaidi na  Choi Mu-jin, kiongozi wa genge kubwa la wahuni wanaojihusisha na kuuza madawa ya kulevya.

Mujin anamsajili rasmi Jiwoo katika genge lake na kuahidi kufanya lolote analoweza ili kumsaidia kulipiza kisasi cha kifo cha baba yake.  

Nikuambie tu usajili ninaozungumzia hapa siyo wa makaratasi, bali ni mashindano ya kupigana na kuuana bila huruma na mshindi anakuwa amefanikiwa kujiunga rasmi na genge hilo la hatari.

Jiwoo anavyozidi kuua watu na kupigana na kiu ya kisasi ikawa inazidi kila siku, huku Mujin akiongeza petroli kwenye moto  kwa kumuonyesha bastola iliyotumika kumuua baba yake na kuthibitisha kuwa bastola hiyo inamilikiwa na kiongozi mkubwa wa jeshi la polisi.

Hasira inayowaka kwenye moyo wa Jiwoo  ni zaidi ya moto wa kichaka, na anapambana kujiunga na jeshi la polisi akisaidiwa na Mujin.

Anapofanikiwa kujiunga na jeshi la polisi , kibarua chake siyo tu kumuua adui yake bali kupeleka taarifa zote za jeshi la polisi kwa Mujin.

 Tunaweza sema maisha ya Jiwoo yanakuwa hatarini zaidi, tena ikizangatiwa jeshi la polisi linaanza kumuhisi kuwa ni kibaraka anayetoa siri za kambi.

Safari ya kulipiza kisasi iliyojaa chuki na hasira itamfikisha wapi Jiwoo? Ni nani muhusika halisi wa kifo cha baba yake?. Majibu yako katika filamu ya muendelezo ya ‘My Name’, unakosaje?

Unaweza kuitazama filamu hii kupitia jukwaa la filamu la mtandaoni la Netflix.

                               

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW