Serikali kuwapiga jeki wakulima mazao ya viungo

February 16, 2022 1:07 pm · Herimina
Share
Tweet
Copy Link
  • Itayapa kipaumbele mazao hayo kwa kuzalisha miche ya kisasa.
  • Pia itawatufutia masoko ya kimataifa. 

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inakusudia kuinua kilimo cha viungo ili kuwawezesha wakulima waliowekeza katika mazao hayo kunufaika kwa kuongeza uzalishaji na kupata masoko ya uhakika. 

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema amekiri kuwa hapo awali Serikali haikutoa kipaumbele kwa kilimo cha mazao ya viungo, lakini kwa sasa imeweka mipango ya kuinua kilimo hicho. 

“Kwanza nikiri kama nchi, kwa muda mrefu tumekuwa hatujayapa kipaumbele mazao haya ya viungo lakini nataka nilihakikishe Bunge lako tukufu kuwa kwanza tumeyacluster (tumeyaunganisha) kama mazao ya horticulture (mazao ya bustani). 

“Kwa hiyo yatasimamiwa kwa ukaribu na idara inayohusika na mazao hayo,’’ amesema Waziri Bashe.

Mazao ya viungo ambayo hutumika katika shughuli mbalimbali za viwandani na nyumbani hujumuisha hiriki, tangawizi, karafuu, mdarasini. 

Bashe alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Dunstan Kitandula leo Februari 16, 2022 Bungeni jijini Dodoma aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wakulima wa jimbo lake kuongeza uzalishaji wa mazao ya viungo. 

Waziri Bashe amesema kuwa Serikali inatekeleza mipango hiyo kupitia mkakati wa kuendeleza mazao ya bustani wa mwaka 2021-2031 wenye lengo la kuongeza uzalishaji kwa kutumia teknolojia bora.

Mipango mingine ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wakulima ili kuwasaidia  kujua kanuni bora za uzalishaji wa mazao ya viungo.


Soma zaidi: 


Aidha, Serikali kuwaunganisha wakulima na wanunuzi wakubwa na kuanzisha vitaru vya kisasa vya miche ya viungo ambapo wizara hiyo imesema tayari mpango huo umeanza kutekelezwa kupitia Chama Cha Usindikaji wa Viungo Tanzania (TASPA).

Mazao ya viungo ambayo yanalimwa kwa wingi katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Mbeya, Kilimanjaro, Kigoma na Ruvuma yamekuwa na tija ndogo kutokana na matumizi ya mbegu duni zinazotumiwa na wakulima.

Kutokana na hali hiyo Serikali imesema kuwa imeagiza Taasisi ya Mafunzo ya Wizara ya Kilimo ya Mlingano mkoani Tanga (MATI) kuhakikisha inafanya utafiti na uzalishaji wa miche na mbegu bora kwa ajili ya mazao ya viungo ili kutatua tatizo hilo.

Kwa mujibu wa Kitabu Cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020, uzalishaji wa mazao ya viungo kwa mwaka mwaka huo ulikuwa tani 123,508 ambapo uzalishaji wake umekuwa ukipanda kila mwaka.

Hata hivyo, uzalishaji huo unaweza ukaongezeka zaidi endapo Serikali itatekeleza kikamilifu mipango yake kwa kushirikiana na wakulima. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW