Viliba tumbo bado vyawatesa watanzania

May 7, 2019 12:41 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Kitambi (kiliba tumbo) ni tumbo kubwa ambalo linachomoza kwa mbele na wakati mwingi kuning’inia isivyo kawaida. Picha|Mtandao.


  • Serikali imesema zaidi ya asilimia 10 ya watanzania wana tatizo la lishe iliyopitiliza ikiwemo viliba tumbo. 
  • Mikoa yenye tatizo kubwa la lishe ni ile yenye uzalishaji mkubwa wa chakula.
  • Serikali itaendelea kutoa elimu sahihi kuhusu masuala ya lishe.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndungulile amesema Serikali itaendelea kutoa elimu ya lishe ili kupunguza changamoto ya lishe iliyopitiliza ikiwemo vitambi kwa watanzania.

Amesema zaidi ya asilimia 10 ya watanzania wana changamoto ya lishe iliyopitiliza kwa maana kuwa wana viliba tumbo (vitambi). 

Dk Ndungulile alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Iddi Mpakate ambaye amesema bado tatizo la utapimlo katika mikoa inayozalisha chakula kwa wingi bado linaendelea kukua. Je serikali ina mpango gani mkakati wa kuajiri watoa huduma za lishe katika vijiji?

“Zaidi ya asilimia 10 ya watanzania wana lishe iliyopitiliza kwa maana wana viliba tumbo, wakina mama wana vitambi na wakina baba wana vitambi, yote hiyo inaonyesha ni lishe ambayo siyo sahihi,” amesema Dk Ndungulile.

Amesema mikoa inayozalisha chakula kwa wingi nchini ndiyo mikoa inayoongoza kwa utapiamlo na hilo linatokana na changamoto ya watanzania kula chakula kuliko kula chakula bora.

Watu wengi hula vyakula vya wanga kwa wingi, kwa mfano, ugali ambao unapikwa kwa kutumia unga wa mahindi, unga wa mtama au muhogo, pia mchele, na vyakula vya jamii ya maharage. 

Milo mingi hukosa mchanganyiko wa protini ya wanyama, mimea, mbogamboga na matunda.


Soma zaidi:


Kutokana na hali hiyo, Dk Ndungulile amesema wanaendelea kutoa elimu kwa njia mbalimbali katika mikoa yenye kiwango kikubwa cha utapiamlo kuhakikisha watu wanapata elimu sahihi kuhusiana na masuala ya lishe

“Lakini tutaendelea kuajiri maafisa lishe kadiri uwezo wa Serikali utakapokuwa unaruhusu,” amesema Dk Ndugulile.

Mwaka 2017, Serikali ilizindua Mpango mkakati wa masuala ya lishe unaratibiwachini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo Wizara ya Afya ina nafasi yake kuhakikisha inapunguza udumavu kwa watoto wadogo lakini tunapambana na lishe iliyopitiliza kwa sababu nayo inahusiana na magonjwa yasiyoambukiza 

Kitambi (kiliba tumbo) ni tumbo kubwa ambalo linachomoza kwa mbele na wakati mwingi kuning’inia isivyo kawaida. Ni ugonjwa kama magonjwa mengineyo na huweza kuwakumba watoto, vijana na watu wazima.

Enable Notifications OK No thanks